Makala

Kupigwa risasi mguuni kutaleta ushindani usiofaa wa huduma kwa walemavu – Sankok

Na FRIDAH OKACHI July 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

USEMI wa Rais wa kuwapiga risasi kwa mguu vijana wanaopora na kuharibu biashara wakati wa maandamano nchini umechangia kutengeneza picha za akili unde (AI) za watu walemavu wakifanya maandamano.

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki David Sankok sasa anasema amri hiyo itasababisha idadi ya watu wenye ulemavu kuongezeka na hata kuondoa nafasi ya kunufaika na haki za watu wenye ulemavu kama uteuzi, msamaha wa ushuru kupitia AGPO, kuingiza magari bila ushuru, na manufaa mengine.

“Sitaki ushindani mimi. Idadi hii itaniondolea uteuzi kwenye serikali na nitagharamika kununua magari bila ushuru,” alisema Bw Sankok.

Kulingana na Bw Sankok, gharama ya kununua viti vya magurudumu, viatu maalum na magongo kwa wote itaongezeka na hivyo kuwa ndoto kwa serikali,” aliongeza Bw Sankok.

Alimtaka Rais William Samoei Ruto kutoa amri ya kuwakamata wahalifu hao na kuwapeleka moja kwa moja mahakamani wakiwa na afya na uwezo wa mwili.

Pia, aliwataka polisi kuwa makini wanapolenga wakati wa kupiga waandamanaji risasi kwa kuwa baadhi ya wanachama wake wana kimo kifupi na hivyo kuna hatari ya kupigwa risasi vichwani na kupoteza maisha yao.

“Mheshimiwa Rais, hatua hii itagharimu zaidi kwa sababu ya risasi zitakazotumika na ushuru ambao hawa wenye ulemavu wapya hawatalipa,” akasema.

Haya yanajiri baada ya vijana wa Gen Z kuchapisha picha za akili unde zikionyesha jinsi wataelekea mahakamani wakiwa na mikongojo, huku wengine wakielekea maandamano wakiwa kwenye viti vya magurudumu.