Kupitishwa kwa ripoti ya Nadco kwatoa nafasi ya marekebisho ya Katiba
MCHAKATO wa marekebisho ya Katiba kwa lengo la kubadili mfumo wa uongozi wa Kenya kupitia kubuniwa kwa afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani na Mkuu wa Mawaziri, sasa unatarajiwa kuanza rasmi.
Hii ni kufuatia kupitishwa kwa Ripoti ya Kamati ya Kitaifa ya Mazungumzo (Nadco) mnamo Alhamisi katika Bunge la Kitaifa na Seneti.
Ripoti hiyo ambayo ni zao la mazungumzo ya maridhiano kati ya mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio La Umoja-One Kenya imependekeza kubuniwa kwa nyadhifa hizo, miongoni mwa mapendekezo mengine.
Kupitishwa kwa ripoti hiyo katika mabunge hayo mawili sasa kunatoa nafasi kubuniwa kwa miswada ya kufanikisha utekelezaji wa mapendekezo yakiwemo kuwekwa kwa Hazina ya Ustawi wa Maeneobunge (NG-CDF) katika Katiba.
“Hoja hii imepitishwa katika bunge hili sawa na katika Seneti na makarani wa mabunge haya mawili wataandaa kikao na maafisa wa idara husika na kuchanganua mapendekezo yanayohitaji kutekelezwa kupitia Miswada ya Kikatiba na ile ya kawaida. Kamati hiyo ndogo inatarajiwa kuendeshwa mchakato huo haraka ili miswada hiyo iwe tayari wakati ufaao,” akasema Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.
Alisema hayo baada ya wabunge wa mirengo ya Kenya Kwanza na wenzao wa Azimio kupitisha ripoti hiyo bila kuifanyia marekebisho yoyote baada ya kuijadili kwa muda wa saa tatu, tangu Jumatano.
Kando na miswada ya kufanikisha kubuniwa kwa Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani, mswada wa marekebisho ya Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), ya 2012 pia inalengwa.
Hatua hiyo itafanikisha kuundwa kwa jopo jipya la kuteua mwenyekiti na makamishna sita wa tume hiyo.
Ripoti hiyo ya Nadco inapendekeza kuvunjwa kwa jopo la sasa lenye wanachama saba, linaloongozwa na Dkt Nelson Makanda, na kuundwa kwa jopo jingine la wanachama tisa.
IEBC imesalia bila mwenyekiti na makamishna tangu Januari 17, 2023, baada ya muda wa kuhudumu kwa aliyekuwa mwenyekiti Wafula Chebukati na makamishna Abdi Guliye na Boya Molu kukamilika.
Kabla ya wao kuondoka afisini, makamishna wengine wanne kuanzia kwa Juliana Cherera (aliyekuwa Naibu Mwenyekiti), Justus Nyang’aya, Francis Wanderi, na Irene Masit walitimuliwa kwa kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais yaliyomtawaza Rais William Ruto kama mshindi.
Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani inayopendekezwa katika ripoti ya Nadco itashikiliwa na kiongozi wa chama au muungano ulioshikilia nambari mbili katika uchaguzi wa urais wa Agosti 9, 2022.
Mshikilizi wa afisi hiyo atasaidiana na manaibu wawili huku afisi hiyo ikifadhiliwa kwa pesa za umma.
Kiongozi Rasmi wa Upinzani pia atakuwa na nafasi ya kuunda baraza lake la mawaziri sambamba almaarufu ‘Shadow Cabinet’ ambalo litahakiki utendakazi wa mawaziri wote wa serikali iliyoko madarakani.
Mapendekezo mengine kwenye ripoti ya Nadco yanahusu kupunguzwa kwa mzigo wa ulipaji mishahara ya watumishi wa umma kwa kima cha asilimia 30.
Aidha, ripoti hiyo inapendekeza kuwa Wizara ya Kawi ipunguze ada ya utunzaji barabara na ile ya kudhibiti kuvurugwa kwa thamani ya mafuta (anti-adulteration levy) kwa kima cha Sh5 na Sh3, mtawalia.
Mirengo ya Kenya Kwanza na Azimio pia ilielewana kuziweka kwenye Katiba hazina za NG-CDF, Hazina ya Kukagua Utendakazi wa Serikali za Kaunti (SOF) na Hazina ya Maendeleo katika Wadi (WDF).
Isitoshe, ripoti ya Nadco inapendekezo kuwa muda wa kusikilizwa kwa kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais katika Mahakama ya Upeo uongezwe kutoka siku 14 hadi siku 21.
Ripoti hiyo pia inapendekeza kutatua kabisa suala la usawa wa kijinsia katika mabunge na serikalini.
Suala hilo sasa linashughulikiwa na Kamati ya Maalum Shirikishi inayoongozwa na Waziri wa Jinsia Aisha Jumwa.