Kusitishwa kwa ujenzi wa barabara ya Sh30bn kulivyozima matumaini ya wakulima
NA WANDERI KAMAU
WAKATI Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alitangaza uzinduzi wa ujenzi wa Barabara ya Mau Mau mnamo 2019, ilikuwa ni furaha kubwa kwa wakazi wa kaunti za Nyandarua, Nyeri, Kiambu na Murang’a.
Wengi waliamini kwamba hatimaye wangepata barabara ambayo ingewaunganisha na kukuza maendeleo, hasa sekta ya kilimo.
Kilimo ndicho kitegauchumi katika kaunti hizo nne.
Alipotangaza uzinduzi wa ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa zaidi ya kilomita 500, Bw Kenyatta alisema lengo lake lilikuwa ni kusuluhisha matatizo ambayo yamekuwa yakiwakumba wenyeji kwenye usafirishaji wa mazao yao.
Kulingana na tangazo la Bw Kenyatta, ujenzi wa barabara hiyo ungeigharimu serikali Sh30 bilioni.
Baada ya tangazo la Bw Kenyatta, shughuli za ujenzi wake zilianza kwa kasi.
Ikizingatiwa barabara hiyo inapitia katika maeneo ya milima na vichaka, kama vile Mlima wa Aberdare, hatua ya kwanza ilikuwa kukata baadhi ya miti ili kutoa nafasi kwa ujenzi wake.
Pia, barabara zilizopangiwa kuunganishwa zilipanuliwa.
Taswira hizo, bila shaka, zilijenga na kuimarisha matumaini ya wakazi wa kaunti hizo.
Katika Kaunti ya Nyandarua, wakazi wa maeneo ya Kinangop, ambako barabara hiyo iliratibiwa kupitia, walieleza furaha yao.
Wengi walieleza matatizo ambayo wamepitia kwa miaka mingi kwenye usafirishaji wa mazao yao kutoka mashambani mwao.
“Ikiwa kuna jambo la maana ambalo (Uhuru) atatufanyia, ni kutujengea barabara hii. Atakuwa ametutoa Misri na kutupeleka Kanani,” akasema Bw Benjamin Theuri, ambaye ni mkazi wa eneo la Njabi-ini.
Hata hivyo, furaha waliyokuwa nayo wakazi wa kaunti hizo nne sasa imeanza kugeuka matumaini yaliyopotea.
Kwa mwaka mmoja uliopita, hakuna shughuli zozote za ujenzi ambazo zimekuwa zikiendelea katika barabara hiyo.
Mbunge wa eneo la Kigumo, Bw Munyoro Kamau, sasa anamrai Rais William Ruto, kufikiria upya kuhusu mustakabali wa barabara hiyo.
“Kama wenyeji wa Mlima Kenya, tunamrai Rais Ruto na serikali yake kuitengea barabara hii fedha za kutosha ili ujenzi wake ukamilike haraka,” akasema Bw Kamau.
Bw Kamau pamoja na mwenzake wa Kangema, Bw Peter Kihungi, wanaitaka serikali kutenga angaa Sh2 bilioni ili kuharakisha kukamilika kwa ujenzi wa sehemu ya barabara hiyo, iliyopitia katika Kaunti ya Murang’a.
“Kwenye bajeti ya mwaka 2023/2024, barabara hiyo Murang’a ilikuwa imetengewa jumla ya Sh200 milioni. Hata hivyo, fedha hizo zilipunguzwa kwa zaidi ya Sh100 milioni. Wito wetu kwa serikali ni kuzingatia vilio vya wakazi, kwa kuhakikisha kuwa ujenzi huo umekamilika,” akasema Bw Kihungi.
Mnamo Jumanne, viongozi kadhaa kutoka Kaunti ya Nyandarua pia walimrai Rais Ruto kufufua tena ujenzi wa barabara hiyo, walipohudhuria mazishi ya babake Seneta wa kaunti hiyo, Bw John Methu.