• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 5:50 AM
Kutana na wanakijiji ambao ndoto yao kubwa ni kuzuru miji kuona gorofa, uwanja wa ndege

Kutana na wanakijiji ambao ndoto yao kubwa ni kuzuru miji kuona gorofa, uwanja wa ndege

NA OSCAR KAKAI

KIJIJI chenye sifa si haba cha Long’urukau katika wadi ya Suam, katikati ya mazingira yenye joto jingi, mimea mikavu na misitu, panaishi wawili wapendanao.

Licha ya kuwa wakongwe, Akalile Rutale na kipenzi chake cha roho Chepkuo ni watu wakarimu tena wa kupendeza. Wawili hao wameoana  kwa miaka 40 sasa na kujaliwa na watoto wa wanne.

Wapenzi hao wawili kutoka eneo la Kacheliba, Pokot Magharibi hawakufanikiwa kusoma na tunapata ugumu wa kuzungumza nao na kuna haja ya mkalimani.

Akalile ambaye alizaliwa miaka 70 iliyopita katika eneo la Alale kwenye mpaka wa Kenya na Uganda anakumbuka jinsi wazazi wake waliuawa na majangili kisha wakalazimika kuhamia eneo la Kacheliba ambapo wanaishi hadi leo.

Mzee huyo ambaye hana ajira anasema kuwa tangu azaliwe amefaulu tu kuenda kwenye maeneo ya karibu kama Alale, Amudat, Nauyapong, Loree, Losam, Amakuriat, Kasei na  Losam kwa miguu.

Anaongeza kuwa yeye husikia tu kuhusu miji kama Kapenguria, Kitale na Nairobi lakini hawajawahi kufika huko.

Akalile anasema kuwa sababu ya yeye kutosafiri ni kuwa hana sababu na kuenda eneo ambalo hajui.

“Sina sababu ya kuenda huko. Pengine nipelekwe tu kuchunga ng’ombe na nipewe pesa,” anasema.

Ana matumaini ya kuwa kama aliyekuwa Gavana Pokot Magharibi John Lonyangapuo, ambaye anamuenzi akisema kuwa siku moja atazunguka kote ulimwenguni.

Naye mkewe Chepkuo ambaye pia alizaliwa eneo la Alale hawezi kukumbuka mwaka ambao alizaliwa huku akibahatisha kuwa alizaliwa wakati wa kifaru.

Anakumbuka jinsi mwanawe aliuawa na watu wasiojulikana.

“Mwanangu alikatwa katwa kwa vipande. Mifugo wetu wote waliibiwa. Walichukua mali yetu yote. Ninasikia uchungu,” anasema.

Aidha Chepkuo naye, hajaenda mbali tangu azaliwe.

Anasema kuwa eneo la mbali ambalo ni Lomsuk kwenye shamba.

“Sijawahi kufika Kapenguria. Mimi husikia tu,” anasema.

Anasema kuwa pia amewahi kuenda eneo la Kiwawa na Amudat umbali wa kilomita 30 penye wanawe wameolewa.

“Sijawahi kupanda gari kwa maisha yangu. Ninaomba wafadhili wanisaidie nitoke kutoka kwa kijiji changu hata kama ni kwa siku moja tu,” anasema.

Anasema kuwa angependa sana kufika katika mji wa Kapenguria.

Jirani wao David Wanyonyi Nandasaba kwa jina la utani Wanyoike wa Kache anasema kuwa wakazi wengi hasa katika kaunti ndogo ya Pokot Magharibi hawajawahi kutoka eneo hilo na kuenda mbali.

Anasema kuwa wengi wanahitaji mwangaza ili waweze kuelewa masuala ya kisasa.

“Hawasafiri popote sababu hawajui pa kuenda,” anasema.

Katika kijiji cha Chesra, tunakutana naye Evelyn John Lokwapale ambaye ni mzee wa mtaa wa  Simotwo Chiroi; yeye naye hajawahi kutoka kwenye kijiji chake.

Bi Lokwapale anasema kuwa hawajawahi kupita eneo la Kacheliba.

“Ningependa kuenda Nairobi ili nione kiwanja cha ndege na gorofa,” anasema.

Mkazi mwingine kutoka kijiji cha Puruo, Monica Komolika, ambaye ni mchungaji wa mifugo na mama wa watoto 12, ambaye anazungumza Kiswahili kidogo anasema kuwa hajawahi kusafiri mbali na mji Kacheliba. Mama huyo anasema kuwa kazi yake ni kuchunga mifugo na kutafuta maji.

“Sijawahi kupita mji wa Kacheliba,” anasema.

Bi Komolika anasema kuwa angependa kuenda mbali kuona jinsi Kenya imepiga hatua kimandeleo.

“Ningependa kuona jinsi watu wamejenga nyumba safi safi,” anasema.

Karibu na mji wa Kapenguria, tunampta Milka Cheyech kutoka kijiji cha Katilok aliyemaliza shule mwaka wa 1990, yatima na mama wa watoto watatu.

Bi Cheyech anasema kuwa yeye hushughulika na kazi za vibarua katika kijiji chake.

“Nina watoto watatu na wanne wa ndugu yangu. Mke wa ndugu yangu alienda na kuwacha nyuma watoto. Ndugu yangu alipata ajali na wazazi wangu walifariki. Ninategemea vibarua. Maisha ni magumu. Mimi hulimia watu mashamba ama kuosha nguo ili nilishe watoto wangu. Wakati mwingine sisi hulala njaa,” anaeleza.

  • Tags

You can share this post!

Miaka 30 ya balaa tupu: Simulizi za vijana watatu...

Ifahamu densi ghali yenye nidhamu ya juu ambayo ukichafua...

T L