• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 3:21 PM
Mwanamume asema kutojaliwa mtoto kumezidisha moyo wa kuwatetea watoto wote

Mwanamume asema kutojaliwa mtoto kumezidisha moyo wa kuwatetea watoto wote

NA KALUME KAZUNGU

“NILIVYO Mwafrika halisi ninaamini kabisa kwamba inachukua kijiji kizima katika malezi ya mtoto. Licha ya kukosa bahati ya kuzaa maishani mwangu, watoto bado wamesalia kipenzi changu cha moyo. Nitatetea haki zao hadi kifo.”

Hayo ni maneno ya Bw Abdulaziz Abdu Swadik.

Akiwa na miaka 50, Bw Swadik anafahamika ndani na nje ya kaunti ya Lamu kwa jinsi alivyolivalia njuga suala au kampeni zinazofungamana na utetezi wa haki za watoto.

Kwa Bw Swadik, adui yake mkuu maishani ni yeyote anayenyanyasa watoto kwa njia yoyote ile, iwe ni kimalezi, kielimu, kimavazi, chakula, malazi na masuala mengine mengi ya kimsingi ambayo mja anapaswa kumkimu mtoto kwayo.

Amekuwa mwanaharakati wa maslahi ya watoto kwa karibu miaka 25 sasa.

Msimamo wa Bw Swadik kuhusu malezi bora ya watoto ni kuwa mbali na familia zao, watu wengine wanaowazunguka, kama yeye, pia ni kiungo muhimu katika kuyahamasisha na kuyafaulisha hayo.

Bw Swadik anaweka wazi kuwa hakuna mzazi au mlezi mwenye kusudi au atakayefurahia kuona mtoto wake anaharibika kimalezi au kitabia.

Aidha anashikilia imani yake kuwa katu hakuna mfumo maalum katika malezi ya watoto ila familia na jamii nzima ina jukumu kubwa katika malezi ya watoto hao, ikiwemo kuwalea kwa mapenzi makubwa.

“Licha ya kutojaliwa mtoto hadi kufikia sasa, hilo huwa halinipigi mshipa. Nikiona watoto nafsi yangu huhisi ni wangu kabisa na linipasalo kufanya kwa wakati huo ni kuona haki zao zikiheshimiwa. Mdomo wangu huwa haunyamazii wakiukaji wa haki za watoto,” akasema Bw Swadik.

Ni kutokana na mapenzi yake kwa watoto ambapo mnamo 2016, Bw Swadik alianzisha Shirika La Kutetea Haki za Watoto Lamu kwa jina-Lamu Child Protection Initiative (LCPI).

Kwa sasa ndiye Katibu Mtendaji wa shirika hilo ambalo tayari limekita mizizi ndani na nje ya Lamu.

Kupitia LCPI, Bw Swadik amefaulu kuwakomboa watoto wadogo kutoka kwa dhuluma, ikiwemo zile zinazotokana na wazazi wao, hasa wale ambao huishia kutengana au kutalakiana katika ndoa.

Isitoshe, amekuwa mstari wa mbele kupiga vita ulawiti wa watoto, unajisi au uchafuzi wa watoto, ndoa za mapema, utelekezaji miongoni mwa maovu mengine.

Anashikilia kuwa hamu yake ni kuona ndoto za watoto katika maisha yao zinatimia kikamilifu.

Anawasisitizia wazazi, jamii ya Lamu, Pwani, Kenya na ulimwenguni kote kuhakikisha watoto wanapokea malezi mazuri, wanapewa heshima, elimu bora na mwishowe kazi bora, hivyo kupata familia na jamii bora ya siku za mbeleni.

“Tusiwe wanajamii wa kupuuzilia mbali au kumwacha mtoto, hata ikiwa si wako, akipotoka kimaadili au kudhulumiwa. Tusinyamaze. Ni jukumu letu kuwa wazazi, walezi, ndugu, marafiki au wanajamii wenye kiu na ndoto ya kuona kwamba tunawaandaa watoto kuwa baba au mama bora katika familia zao za kesho,” anasisitiza Bw Swadik.

Afisa huyo aidha anaonya wazazi au walezi wenye hulka ya kuwaachilia watoto kupotoka huku wakikua hadi ukubwani ndipo waanze kuwaelekeza njia zifaazo.

Bw Swadik anasema kufanya hivyo kutakuwa ni sawa na kuipigia mbuzi gitaa.

Anagusia methali ya wahenga kwamba ‘Samaki mkunje angali mbichi’.

“Huwezi kumwacha samaki akauke, kugeuka ng’onda na kisha utarajie kumkunja. Ukifanya hivyo tarajia atavunjika. Hivyo malezi bora ya awali ni muhimu sana kwa maendeleo na afya ya watoto. Katu hawatayaacha au kuyasahau hadi ukubwani na uzeeni mwao,” akasema Bw Swadik.

Lakini je, jamaa huyu amepambana vipi na kuyashinda mawimbi ya vidudu watu ambao mara nyingine hujipata wakimkejeli?

Mwanaharakati wa Haki za Watoto Lamu, ambaye pia ni Afisa Mtendaji wa Shirika la Lamu Child Protection Initiative (LCPI), Bw Abdulaziz Abdu Swadik,50. Anasema kukosa kuzaa maishani kumezidisha moyo wa kuwapenda na kuwatetea watoto. PICHA | KALUME KAZUNGU

Anakubali kushuhudia bezo kutoka kwa baadhi ya watu katika shughuli au safari yake ya kutetea haki za watoto.

Anasema siri kuu iliyomfaulisha na kumfanya kupiga hatua moja na nyingine kila siku ni kujitia hamnazo, hasa kwa wanaoleta madharau hayo.

“Mara nyingine ninapopita mitaani husikia watu wakinikejeli kwamba sina mtoto ilhali kila kuchao niko mbioni kutetea haki za hao watoto. Yaani kuna wanaokereka na misimamo yangu mikali kuhusu watoto. Kamwe hilo halinishtui. Nimejifunza kutia masikio yangu pamba ilmradi nitetee hizo haki za watoto vilivyo,” akasema Bw Swadik.

Baadhi ya changamoto anazokumbana nazo kwenye harakati zake ni ukosefu wa fedha kwani shirika lake halina mfadhili yeyote.

Anasema licha ya shirika lake kutekeleza majukumu sufufu, bado hajaweza kujisimamia kiasi cha kupata ofisi.

Shirika hilo kwa sasa lina wanachama 25 ambao wote ni wa kujitolea.

Bw Swadik anasema kutokana na ukosefu wa hela, mara nyingi imewawia vigumu kuandaa mikutano na makongamano ya kuwahamasisha wanachama na pia umma wenyewe kuhusu haki za kimsingi za watoto na jinsi gani zitaheshimiwa.

Pia anataja kukosekana kwa kituo maalum cha kuwaokoa watoto wanaodhulumiwa Lamu kuwa changamoto nyingine inayowakabili.

Kituo cha karibu cha kuwatorosha na kuwahifadhi watoto waliodhulumiwa kutoka Lamu ni kile cha Malindi ambako ni mbali.

Anawasihi wafadhili kujitokeza ili kusaidia kufaulisha harakati na ndoto yake kuhusu watoto.

Watoto wakiogelea kwenye sehemu moja ya ufukwe wa Bahari Hindi kisiwani Lamu. Bw Swadik anawahimiza wazazi kuwapa watoto wasaa wa kucheza na pia kuwaangalia kwa makini wasidhuriwe. PICHA | KALUME KAZUNGU

Hulka ya baadhi ya wanajamii wa Lamu, ambao mara nyingi hawako tayari kusimama tisti kuwatetea watoto hasa punde wanapopitia dhuluma pia ni kizingiti kingine.

“Twahitaji jamii isimame imara kutetea watoto. Utapata mtoto amedhulumiwa lakini jamii, hasa wazazi, wakidinda kabisa kusimama mahakamani kutoa ushahidi. Wanapendelea kusuluhisha mambo kienyeji (maslahi) ambalo kamwe si jambo zuri. Kufanya hivyo ni kumdhulumu mtoto,” anasema Bw Swadik.

Pia anaomba mashirika yanayofungamana na masuala ya watoto kama vile lile la Umoja wa Mataifa La Kuhudumia Watoto (Unicef), Save the Children International, National Child Protection Authority na mengine mengi kufungua matawi yao Lamu.

Anasema endapo matawi ya mashirika hayo yatafikishwa Lamu, utendakazi wa wanaharakati wa haki za watoto kama yeye utarahisishwa.

Bw Swadik hata hivyo anapongeza ofisi ya idara ya usalama, ikiongozwa na Kamishna wa Kaunti na manaibu wao, machifu na wazee wa mitaa kwa kufanya kazi kwa karibu na yeye kufaulisha harakati zake.

Pia anaishukuru Ofisi ya Kiongozi wa Mashtaka ya Umma (ODPP) na mahakama ya Lamu kwa jumla kwa kushirikiana naye katika kuwalinda watoto.

Bw Swadik alizaliwa kisiwani Lamu mwaka 1974.

Ni kitindamimba katika familia ya watoto wanane.

Alisomea katika Shule ya Msingi ya Wavulana ya Lamu.

Baada ya kuhitimu elimu yake ya msingi, hakuweza kujiunga na sekondari kutokana na umaskini uliogubika familia yake.

Hali hiyo ndio ilimsukuma kuingilia masuala ya utetezi wa haki za watoto, harakati ambazo anaziendeleza hadi leo hii.

Bw Swadik ameoa lakini hajafanikiwa kupata mtoto.

  • Tags

You can share this post!

Ruto ziarani TZ, Zimbabwe nyuma akiacha mafuriko, mgomo wa...

Wilson Lemkut: Shujaa aliyewaokoa watoto 16 ziwani Baringo

T L