Kutoka pangu pakavu tia mchuzi hadi kuwa mwalimu
Na SAMMY WAWERU
ALIPOFANYA mtihani wa kitaifa wa kidato cha nne (KCSE) mnamo 2007 hakuwa na budi ila kutafuta kazi kusukuma gurudumu la maisha.
Bi Mary Wanjiru anasema wazazi wake hawakuwa na uwezo kifedha kumlipia karo kuendelea na masomo katika taasisi ya elimu ya juu.
“Ndugu wazawa wangu walikuwa wadogo, wengine walikuwa katika shule ya upili na msingi, hivyo basi sikuwa na lingine ila kutafuta kazi ili nijisimamie,” aelezea Wanjiru ambaye ni mzaliwa wa Kirinyaga.
Kaunti anayotoka ni miongoni mwa zilizojaaliwa kuimarika kilimo, na Wanjiru anaiambia Taifa Leo alifanya vibarua vya kulimia watu mashamba.
Kulingana naye, kwa siku angepata kadri Sh150, kwenye pato hilo anatumia Sh50 na kuweka akiba ya Sh100.
“Chakula nilikipata shambani na pia nilijukumika kusaidia wazazi wangu kukimu familia kwa riziki,” asema.
Wanjiru anadokeza kwamba mwishoni mwa 2009 alikuwa ameweka akiba kiasi cha pesa zilizomuwezesha kuwekeza kwenye biashara ya nguo za mitumba.
Alikuwa akiendea nguo katika katika soko maarufu la Gikomba, lililoko jijini Nairobi. Alifanya mauzo kwa njia ya uchuuzi, ambapo angezungusha katika maboma ya watu na kwenye masoko.
Kazi yenyewe haikuwa rahisi, kwa anachotaja siku kukamilika bila kufanya mauzo.
“Katika biashara ukipata shukuru Mungu, ukikosa siku inayofuata jipe moyo na matumaini hutakosa kufanya mauzo,” asema Wanjiru.
Charles Gathogo mhasibu na mjuzi wa masuala ya uchumi anasema biashara inahitaji uvumilivu na ustahimilivu wa hali ya juu. Kulingana na mtaalamu huyo, kinachofilisisha wawekezaji wengi ni kuwa na matarajio yasiyowezekana kwa kipindi kifupi, kinyume na mazingira ya biashara.
“Uwekezaji unahitaji kupewa muda ili kuanza kupata faida. Ni muhimu kufahamu kwamba faida huambatana na hasara. Kuna biashara zinazochukua hata zaidi ya mwaka mmoja kabla kuimarika, ili kuanza kufurahia matunda yake,” afafanua Bw Gathogo, akihimiza muhimu ni kuimarisha uhusiano mwema na wateja.
Bi Mary Wanjiru, 30, anasema licha ya changamoto alizopitia, hakufa moyo na badala yake alijikaza kisabuni akifahamu fika kuwa ipo siku maisha yatamuendea shwari.
Miaka miwiki baada ya kuingilia biashara, mwanadada huyo anasema alikuwa ameweka akiba ya kumuwezesha kusomea kozi aliyoitamani na kumezea mate tangu akiwa mchanga. Katika mtihani wa KCSE alikuwa amezoa alama C.
“Nilitamani sana kuwa mwalimu, 2012 nilijiunga na Chuo cha Ualimu cha Narok, kinachotoa mafunzo ya shule za msingi,” afichua.
Wanjiru ambaye ni mama wa mtoto mmoja anasema aliendelea kufanya uchuuzi wa nguo, wakati wa ziada na likizo, akilenga mavazi ya wanafunzi hususan wa kike.
“Nilijisomesha hadi nikafuzu kupitia uuzaji wa nguo,” aeleza. Taaluma ya ualimu wa shule za msingi huchukua muda wa miaka miwili.
Kwa neema ya Mungu, baada ya kuhitimu kozi, Wanjiru alipata nafasi ya kazi katika shule moja ya binafsi Kirinyaga.
Hata ingawa hajapata nafasi kuajiriwa na tume ya kuwaajiri walimu nchini, TSC, mwalimu huyo anasema hajakata tamaa kuingia serikalini. TSC ni tume inayoajiri walimu kujiunga na orodha ya watumishi wa umma serikalinu, kitengo cha walimu wanaolipwa na serikali.
Kila mwaka hujaribu bahati yake, kuona iwapo atasajiliwa. Ni mwalimu gwiji wa Somo la Hesabu na Sayansi.
Wakati wa mahojiano alisema bado anaendelea kuuza nguo, ingawa kupitia mitandao.
“Nikileta nguo, hufikia wateja wangu kupitia mitandao. Hupiga picha ya bidhaa nilizonazo na kuzipakia mitandaoni,” akasema. Kujiri kwa Facebook, WhatsApp na Instagram kumeimarisha baadhi ya biashara, hasa kwa wanaotumia mitandao hiyo ipasavyo kujiimarisha.
Hata hivyo, unashauriwa kuwa makini, kwa kuwa mumo humo kuna matapeli wanaoweza kukufyonza.