• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 2:00 PM
KVDA yawaondolea hofu wakazi ikisema ni vigumu bwawa la Turkwel kutapika maji

KVDA yawaondolea hofu wakazi ikisema ni vigumu bwawa la Turkwel kutapika maji

NA OSCAR KAKAI

KUFUATIA mvua kubwa inayoendelea kunyesha nchini, kiwango cha maji katika bwawa la Turkwel katika kaunti ya Pokot Magharibi, kinaendelea kuongezeka huku wakazi wakianza kuingiwa na hofu.

Wakazi hao wanahofu kuwa huenda bwawa hilo likajaa na kutapika maji, hali inayoweza kusababisha mafuriko ya madhara Pokot Magharibi.

Kwa mara ya kwanza mnamo Oktoba 2020, kiwango cha maji kwenye bwawa hilo kilipanda zaidi hadi mita 11.48.4 ambapo zilisalia tu mita 1.6 maji kuanza kumwagika lakini wakazi wakaponea.

Lakini Mamlaka ya Kustawisha eneo la Bonde la Kerio (KVDA) ambayo huwa na wajibu wa kutunza bwawa hilo imewahakishia wakazi kuwa hakuna hatari ama tahadhari kuhusu suala hilo.

Meneja Mkurugenzi wa KVDA Sammy Naporos alisema Jumanne kuwa kiwango cha maji kufikia Jumanne saa kumi na moja asubuhi kilikuwa mita 11.33.85 kulinganisha na kina cha bahari na bado kuna nafasi kubwa.

Meneja Mkurugenzi wa mamlaka ya ustawi wa eneo la Bonde la Kerio (KVDA) Sammy Naporos akiongea na wanahabari kwenye bwawa la Turkwel, Kaunti ya Pokot Magharibi. PICHA | OSCAR KAKAI

Alisema kuwa kiwango cha maji kwenye bwawa hilo kimeongezeka kwa sentimita 75 kwa muda wa saa 24.

Bw Naporos anasema kuwa bwawa hilo hupata maji yake kutoka nchini Uganda na eneo la Mlima Elgon—maeneo ambayo kwa sasa yanashuhudia kiwango cha chini cha mvua.

Anasema kuwa bwawa hilo lina miundombinu ya kuondoa maji zaidi yarudi kwenye mto ikiwa yamejaa.

Bw Naporos anasema kuwa uchafu kwenye maji ni changamoto kubwa kulingana na vile bwawa hilo lilijengwa na uchunguzi wa mazingira unaashiria kuwa changarawe imekula jumla ya ujazo wa Cubic 10 milioni katika bwawa hilo.

Uchafu huo umefanya maji kupanda juu kuliko jinsi inavyofaa.

“Tumepanda miche ya miti kwenye nasari. Tunafanya uhifadhi wa mazingira juu ya mto eneo la Kacheliba. Ni gharama kubwa kuondoa uchafu huo kutoka kwenye bwawa,” anasema Bw Naporos.

Mhandisi wa masuala ya maji katika mamlaka ya KVDA Daniel Kimtai anasema kuwa itachukua mwezi mmoja bwawa hilo kumwaga maji ikiwa kutakuwa na mvua ya mfululizo.

Anasema kuwa bwawa hilo linaweza kubeba kiwango cha maji hadi mita 1150.

“Tunatarajia kiwango cha maji kupanda lakini itachukua muda kujaa. Bwawa linaweza kutapika maji kwa kipindi cha mwezi mmoja ujao ikiwa mvua itaendelea kunyesha takriban kila siku. Lakini sio rahisi,” akasema Bw Kimtai.

Alisema kuwa kiwango cha maji kinaongezeka kwa mita 0.75 kila siku na ikiwa hali hiyo itaendelea, maji ya bwawa hilo yatamwagika chini ya mwezi mmoja.

Anasema kuna bado mita 15 ambazo zinasalia ndiposa maji hayo yaanze kumwagika.

“0.75 kwa siku 10 ni mita 7.5, kunaamanisha kuwa maji hayo yanaweza kumwagika kwa siku 20 zijazo. 0.75 mara 20 ni mita 15 ikiwa hali ni hiyo. Lakini mvua hainyeshi kwa kiwango sawa kila siku,” akasema Bw Kimtai.

Aidha, Bw Kimtai amewataka wakazi ambao wanaishi nyanda za chini kuwa na utulivu akisema kuwa bwawa hilo ni thabiti na limejengwa vyema na hakuna haja kuwa na kiwewe.

“Ikiwa kutakuwa na dharura, bwawa hilo limejengwa vyema na linaweza kuondoa maji kupitia kwa njia za maji,” akafafanua.

Alieleza kuwa ni jambo la kawaida bwawa kumwaga maji na wakazi hawafai kuwa na hofu.

Alisema kuwa bwawa la Turkwel ni mojawapo ya mabwawa thabiti zaidi nchini, yenye kiwango cha maji umbali wa kilomita 60 na maji lita 1.2 bilioni.

“Haliwezi kupasuka na wakazi wanafaa kuwa watulivu sababu tuko chonjo,” akasema.

Alisema kuwa bwawa kumwaga maji pia kuna manufaa kwa wakazi.

“Kwa miaka mitatu bwawa hili linaweza kuzalisha kilowati 106 kunufaisha Wakenya. Wakulima wa Loyapat na Katilu watapata maji mengi ya kunyunyuzia mimea maji,” akasema.

Alisema kiwango cha sasa cha maji kitachukua muda wa miaka mitatu hadi mine kuwezesha uzalishaji umeme kupitia kwa kampuni ya kuzalisha umeme nchini-KenGen.

Alisema kuwa wanafutilia bwawa hilo kila wakati jinsi linavyofanya kazi.

“Bwawa hilo hufanya kazi zote za kuzalisha umeme, kunyunyizia maji mashamba, uvuvi na hata utalii. Haliwezi kutingika hata kama kuna mtetetemko wa ardhi,” akasema.

Mhandisi huyo alisema kuwa kumwagika kwa maji ni suala la polepole na sio kitu cha ghafla.

“Ni jambo la kawaida hata bwawa la Masinga humwaga maji kwa wakati mwingine.  Nafasi ya maji ikijaa, linamwaga– hiki kikiwa kiwango kinachotumika kuzalisha umeme,” akaeleza.

Alisema kuwa wanafutilia bwawa hilo kuhusu presha a miganda na vile maji inatembea.

“Kiwango cha maji kinaogezeka sababu ya uchafu unaotokana na matumizi ya ardhi kwqa kilimo maeneo ya Mlima Elgon, Kacheliba na Moroto, Uganda. Kiwango cha uchafu ni milioni kiubiki 10 kila mwaka,” anaongeza kusema.

Mwenyekiti wa wanachama wa bwawa eneo la Riting Bw Lopuo Lotelwekwa alisema kuwa ongezeko la maji limefanya baadhi ya wakazi eneo hilo kuhama.

“Samaki wamepungua, nyumba zimefunikwa na maji, wakazi wamehama na hata wengine wanaishi kwenye mapango,” akasema.

Alisema kuwa wadi tatu za Endough, Kapchok na Kasei zimeathirika.

Bi Jackline Lokiru ambaye ni mkazi wa soko la Riting, alitoa wito kwa serikali kuwahamisha hadi maeneo salama.

“Maji yanaongezeka na hatuna pa kuenda. Vitu vyangu vinaharibikia kwenye maji,” akasema.

Maeneo ya Kalemnyang, Loyapat, Lodwar, Nakwamoru na mengine yanayopakana na Ziwa Turkana yanatajiwa kuathirika.

Likijaa, maji hayo yataelekea kwenye Ziwa Turkana.

Naibu Chifu wa kata ya Kostei, Joseph Siwa, alisema kuwa wakazi sasa wanaishi kwa hofu.

Mafuriko yameathiri maeneo ya Reresi, Konoso, Chepkachin, na Kudulongole. Mazao ya mahindi na mifugo imeathiriwa na mafuriko na wakazi wanalazimika kuhamia maeneo salama.

Ikiwa bwawa hilo litamwaga maji, hali hiyo inaweza ikaathiri mto wa Turkwel kwa kuwa na maji mengi kupindukia. Pia maeneo ya Loyapat, Katilu na Turkwel katika mji wa Lodwar pamoja na Lokesheni za Sitei pamoja na Kopul yataathirika.

Zaidi ya wakazi 3,000 wanaoishi eneo hilo wataathirika.

Kumwagika kwa maji hayo kutawandoa wakazi wa nyanda za juu ambao wengi wanasemekana kunyakuwa ardhi ya bwawa hilo.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Askari jela aliyemwaga unga akitibiwa aomba arudishwe kazini

Mzozo watokota shule ya kifahari ya Mang’u High baina...

T L