KWA KIFUPI: Sababu za mvi kuota mapema
Na PAULINE ONGAJI
TUNAVYOZIDI kuzeeka, ni kawaida kwa nywele kubadili rangi na kuwa za kijivu au nyeupe.
Kwa kawaida, watu wa asili ya kizungu huanza kuota mvi wakiwa katika awamu yao ya mwisho ya miaka ya thelathini.
Wale wa asili ya Asia huanza kushuhudia haya mwanzoni mwa umri wa miaka ya 40, huku Waafrika wakianza kuota mvi kati kati ya miaka ya arubaini.
Nini kinachozipa nywele zako rangi?
Vifuko vidogo vya vinyweleo vilivyo na seli maalum za rangi huzingira nywele. Seli hizi za rangi zinaitwa melanini. Melanini huipa ngozi na nywele zako rangi. Muda unavyozidi kusonga, vinyweleo hivi vya nywele hupoteza rangi na kusababisha mvi.
Nini kinachosababisha mvi kuota mapema?
• Jeni
Kwa baadhi ya watu suala la nywele kubadili rangi huwa la kiukoo. Ikiwa wazazi au babu zako walikumbwa na tatizo hili, basi kuna uwezekano mkubwa kwamba wewe pia utashuhudia haya. Kwa bahati mbaya, hakuna jambo ambalo laweza kufanywa kuepuka.
• Upungufu wa virutubisho vya vitamini
Ukosefu wa virutubisho vya kutosha vya vitamin B12 mwilini pia waweza sababisha ngozi na nywele kubadili rangi. Aidha, upungufu huu waweza kusababisha anemia (ambapo seli za damu hazina himoglobini ya kutosha, kiungo muhimu kinachobeba oksijeni mwilini kote). Kwa kawaida, Vitamin B12 hupatikana kwenye nyama ya ng’ombe, mayai na bidhaa zingine zinazotokana na wanyama.
• Masuala ya kihomoni
Iwapo tezi dundumio (thyroid gland) haifanyi kazi ipasavyo, huenda uwezo wa mwili wako kuzalisha melanini ukapungua, na hivyo kusababisha nywele zako kubadili rangi mapema. Tezi dundumio ni kikoromeo kidogo kinachopatikana katika sehemu ya mbele ya shingo lako.
• Maradhi yanayotokana na mwitiko wa kinga usio wa kawaida sehemu fulani ya mwili (Auto-immune disease)
Katika hali hii, mfumo wa kinga mwilini hushambulia seli zake. Kuna aina mbili katika kitengo hiki; alopecia areata na vitiligo ambazo zaweza sababisha nywele kubadili rangi mapema. Mhusika akiwa na vitiligo, mfumo wa kinga mwilini hushambulia seli zinazozalisha melanini mwilini. Hii husababisha kuchipuka kwa madoa meupe kwenye ngozi na kuota kwa mvi mapema. Endapo mhusika anakumbwa na alopecia areata, nywele hutoweka ghafla na kuota tena na ni hapa ndipo mhusika anagundua kwamba nywele nyeupe zimechipuka.
• Uvutaji sigara
Uvutaji sigara una madhara mengi ikiwa ni pamoja na kansa, maradhi ya moyo na mapafu. Aidha, uvutaji sigara waweza kuhusishwa na kuota kwa mvi.
• Rangi za kemikali na bidhaa zingine za nywele
Bidhaa za nywele zilizoundwa kwa kemikali ya ‘hydrogen peroxide’ zimeonekana kuwa na madhara kwa nywele na zaweza kusababisha kuota kwa mvi.
• Sababu nadra
Neurofibromatosis (Von Recklinghausen’s disease) na tuberous sclerosis ni hali za kiafya za kiukoo na ambazo zaweza kusababisha kuchipuka kwa uvimbe usiosababisha kansa mwilini kote. Aidha, maradhi haya yaweza husishwa na kuota kwa mvi.
• Sababu zinazopelelezwa
Kuna utafiti unaohusisha tatizo la nywele kubadili rangi mapema na wembamba wa mifupa (osteopenia) na maradhi ya moyo, lakini upelelezi zaidi unahitajika hapa.
Je, mfadhaiko husababisha mvi kuota mapema?
Watu wengi hugundua kwamba mvi huanza kuota mapema miongoni mwa watu wanaofanya kazi zilizo na shinikizo sana kama vile miongoni mwa marais, maafisa wakuu watendaji, maafisa wakuu wa fedha na hata uzazi. Hata hivyo hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha kwamba mfadhaiko huchochea kuota kwa mvi. Lakini tatizo hili limeonekana kuchangia kutoweka kwa nywele.
Je, uotaji mapema wa mvi waweza kuzuiwa?
Ikiwa hali hii inatokana na jeni, basi jibu ni la. Itakubidi kuzoea mabadiliko ya rangi ya nywele zako. Unapaswa kuelewa kwamba hata rangi za kudumu sharti zipakwe mara kwa mara kwani kwa kawaida haziingii kwenye seli za rangi. Ikiwa una mvi kisha upake rangi, itakubidi kurudia utaratibu huu zikiota tena.
• Shughulikia matatizo ya kiafya yanayokukumba: Ikiwa hauna uhakika iwapo matatizo yako ya kiafya yanasababisha kuota mapema kwa mvi, basi enda ufanyiwe uchunguzi wa mwili wote. Ikiwa kuna hali yoyote ya kiafya inayosababisha tatizo hili, basi litahitajika kuangaziwa.
• Dumisha lishe bora hasa chakula kilicho na viwango vingi vya Vitamin B12: Vyakula kama vile mboga za kijani na vyakula jamii ya kunde kama vile maharagwe vitakufaa. Ikiwa upungufu wa Vitamin B12 mwilini mwako umekithiri, utahitajika kumeza vijalizo vya tembe (supplements). Aidha, mbinu zingine ni pamoja na kuacha kuvuta sigara mara moja. Pia, utahitajika kuchagua bidhaa za nywele kwa busara huku ukiepukana na kemikali zinazoathiri ngozi ya kichwani. Lakini ikiwa tayari una mvi, ni vigumu kurejelea hali ya kawaida.