KWA KINA: Jowie alipiga na kupokea simu zaidi ya mara 100 usiku wa kuuawa kwa Monica
Na BRIAN WASUNA
BAADA ya Joseph Irungu (Jowie) ambaye ni mshukiwa mkuu katika mauaji ya mfanyabiashara Monica Kimani, kunyimwa bondi na Mahakama Kuu mnamo Jumanne, sasa imebainika kuwa wachunguzi wa kesi hiyo wanafuatilia mawasiliano yake ya simu kati ya Septemba 19 na 20 kupata ushahidi.
Tayari wachunguzi wamebaini kuwa kati ya siku hizo mbili, mshukiwa alitumia simu yake kuwasiliana mara takriban 108, kwa kupiga ama kupigiwa na kutuma jumbe fupi.
Vilevile, wachunguzi wamefuatilia mienendo ya Bw Irungu kwa karibu, hadi sasa ikionesha kuwa alikuwa akitembelea karibu na alipokuwa akiishi marehemu Bi Kimani aliyeuawa usiku wa Septemba 19, katika mtaa wa Kilimani, Nairobi.
Ripoti za wachunguzi ambazo zimefika kortini zinasema kuwa Bw Irungu aliondoka Lang’ata kuelekea Kilimani dakika chache kabla ya saa kumi mnamo Septemba 19 na alipokuwa katika eneo la Ngei, karibu na Lang’ata alipokea simu iliyodumu kwa muda wa sekunde 52.
Dakika 12 baadaye, mshukiwa huyo alipiga simu kwa sekunde 14 alipokuwa akipita Uchumi Ngong Hyper, katika barabara ya Ngong Road. Dakika nane baadaye, mshukiwa alikuwa barabara ya Dennis Pritt ambapo tena alipiga simu kwa muda wa sekunde 29.
Wachunguzi sasa wanatumia simu hizi kujua mahali alipokuwa wakati fulani na namna mienendo hiyo inaweza kuchangia mauaji yaliyotokea. Wachunguzi wamesema kuwa kati ya saa moja na dakika sita asubuhi ya Septemba 19 na saa nne usiku mnamo Septemba 20, Bw Irungu alipokea simu na jumbe 108.
Hadi sasa, upande wa mashtaka ambao ulipinga kuwachiliwa kwa dhamana kwa Bw Irungu unasema kuwa uchunguzi wao umeonyesha kuwa mshukiwa huyo alikuwa katika eneo la tukio la mauaji wakati yalipotokea. Hata hivyo, uchunguzi huo haujamweka moja kwa moja katika nyumba ya Bi Kimani.
Akimnyima dhamana mnamo Jumanne, Jaji James Wakiaga alisema kuwa hali ya Bw Irungu kukosa makazi yanayofahamika wala mali anayomiliki humu nchini inamweka katika hatari ya kutoroka na kukwepa sheria.
Jaji huyo aidha alikosoa tabia ya mshukiwa ya kuishi kwa wanawake kuwa isiyo ya maadili na kumtupa rumande kwa miezi tisa, alipomwachilia kwa dhamana mshukiwa mwenzake ambaye ni mwanahabari wa runinga ya Citizen, Jacque Maribe.
“Picha inayojitokeza kutoka upande wa mashtaka kupitia ushahidi na ripoti ya kumpa dhamana mshukiwa inamwonesha kuwa ‘Slayqueen’ aina ya kiume, mtu anayechukiwa kwa tabia zisizo za maadili; na ambaye kwa kukosa namna nyingine bora ya kumweleza, nitamwita mlaji wa wanawake. Alikuwa akiishi katika nyumba ya mshukiwa wa pili, akiendesha gari lake na bila kazi iliyomlipa tangu 2017 alipotoa huduma za ulinzi kwa wanasiasa fulani wa Jubilee,” akasema Bw Wakiaga.
Maelezo haya yalifuatia ushahidi wa upande wa mashtaka ambao umempaka tope Bw Irungu kuwa jamaa wa kuogopwa, na ambaye kuachiliwa kwake kutawahofisha mashahidi.
Na japo Bw Irungu alijaribu kujitetea kuwa alikuwa tayari kupeana pasipoti yake kortini na kuwa ndugu zake wangemsaidia apate pa kuishi wakati akiwa nje kwa dhamana, mahakama ilitupilia mbali ombi lake.
Bi Kimani aliuawa usiku huo ambao wachunguzi wamenakili mienendo ya Bw Irungu, huku ripoti ya upasuaji wa maiti yake ikionyesha kuwa alikatwakatwa shingoni na kujeruhiwa vibaya.
Hata hivyo, daktari aliyepasua maiti yake bado hajawasilisha ripoti kamili kortini.
Kwa upande wao, wachunguzi nao kupitia nakala zilizoko kortini wamesema kuwa kati ya saa kumi na nusu jioni na saa nne na nusu usiku wa Septemba 19, Bw Irungu alikuwa katika barabara ya Dennis Pritt. Hapa ndipo ilipo nyumba ya Bi Kimani katika mtaa wa Kilimani, Lamuria Gardens.
Mnamo saa 4:35 usiku huo, Bw Irungu anasemekana kupokea simu ya dakika tatu, iliyodumu kwa kipindi kirefu zaidi siku hiyo. Baada ya kukatika aliondoka kuelekea mtaa wa Lang’ata. Saa 4:52 usiku, mshukiwa huyo alikuwa akipita karibu na makao makuu ya Idara ya Ulinzi katika mtaa wa Hurlingham ambapo pia alipiga simu ya sekunde 40.
Simu yake ya mwisho ilipigwa katika sehemu iliyopo nyumba ya kampuni ya Nairobi Housing Corporation, eneo la Madaraka. Simu hiyo haikupokelewa. Hapa ilikuwa dakika tatu baada ya usiku wa manane.
Kati ya wakati huo na saa 4:01 usiku uliofuata (Septemba 20), vilevile muda ambao Bi Kimani tayari alikuwa ameuawa, Bw Irungu anasemekana kupiga simu 70.
Tayari upande wa mashtaka umehakikishia korti kuwa umewaweka mashahidi wote wa kesi hiyo katika mpango wa kuwapa usalama kutokana na hatari wanayokumbana nayo, hasa ikizingatiwa uzito wa kesi hiyo.
Hii ilikuwa baada ya kiongozi wa mashtaka Catherine Mwaniki kuiomba korti kuwazuilia Bw Irungu na Bi Maribe kwa wiki kadha, ili kuwaweka mashahidi katika mpango huo wa ulinzi.
Bi Mwaniki awali alikuwa amemweleza Jaji msimamizi wa kesi hiyo Jessie Lesiit kuwa “kuna uwezekano mkubwa kuwa washukiwa wataingilia ushahidi na kuwatishia mashahidi umuhimu iwapo wataachiliwa kwa dhamana.”
Ukipinga haswa kuachiliwa kwa Bw Irungu, upande wa mashtaka ulisema japo umefanikiwa kumweka katika eneo la tukio wakati mauaji yalipotendeka, bado polisi hawajamkamata mtu anayeaminika kuwa na Bw Irungu baada ya mauaji kutendeka.
Alipouawa, Bi Kimani anadaiwa kuwa alikuwa ametoka Sudan Kusini na kuwa alipanga kurudi huko siku iliyofuata.
Vilevile, wachunguzi wanasema kuwa kuna uwezekano kuwa kuna pesa zilizoibiwa kutoka nyumba ya marehemu na wanachunguza ni nani aliye nazo kwani bado hazijapatikana.
Baadhi ya mashahidi wakuu wanaotegemewa na upande wa mashtaka ni mtu anayedaiwa kumwona Bw Irungu akichoma mavazi, usiku ambao Bi Kimani aliuawa. Kulingana na ripoti, nguo hizo zilichomewa nyuma ya nyumba ya Bi Maribe katika mtaa wa Lang’ata, na shahidi huyo amedaiwa kuziona na kuzitambua kwamba zilikuwa za Jowie.
Upande wa mashtaka umeshikilia kuwa nyumba hiyo ya Lang’ata bado ni eneo la mauaji, na hivyo Bi Maribe hafai kufika huko. Korti iliamrisha kuwa Bi Maribe aandamane na wachunguzi kila atakapohitajika katika nyumba yake hiyo ya Lang’ata.
“Mshukiwa wa pili ni mama asiye na mume na ambaye ana mtoto anayehitaji ulezi wake. Shtaka linalomkabili lina kifungo cha miaka mingi ama kifo akipatikana na hatia. Hivyo, ni vyema achukue muda na mwanawe wakati huu wa kesi ili amlee na kumfunza kuwa raia mwema katika siku za usoni,” Jaji Wakiaga akasema alipokuwa akimwachilia Bi Maribe.
Jaji huyo alisema upande wa mashtaka haukutoa ushahidi wa kutosha kudhihirisha kuwa Bi Maribe alifaa kuzuiliwa. Tayari Bi Kimani alizikwa takriban mwezi mmoja uliopita na japo familia yake haijakuwa ikijitokeza hadharani, wakili wa familia hiyo alikuwa amepinga kuachiliwa kwa washukiwa hao kwa dhamana.
Bw Irungu naye japo alijitetea kuwa hataathiri ushahidi wala kutoroka, alinyimwa bondi na sasa anazuliwa rumande hadi kesi hiyo itakapoanza kusikizwa kuanzia Juni 18. Korti ilimtaja mshukiwa huyo kuwa mtu anayehitaji kusimamiwa kwa karibu.
“Ni mwanamume anayehitaji kusimamiwa kwa karibu sana, hali ambayo inawezekana tu katika jela iliyolindwa,” akasema Jaji Wakiaga.