Jamvi La SiasaMakala

Kwa nini Kingi anapuliza parapanda ya umoja wa pwani

Na PHILIP MUYANGA September 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

SPIKA wa bunge la Seneti Bw Amason Kingi amekuwa katika mstari wa mbele kupigia debe suala la umoja wa viongozi wa siasa katika ukanda wa pwani kwa muda mrefu.

Kila anaposiamama jukwaani ni nadra sana Bw Kingi kukosa kuzungumzia suala hilo na uwezekano wa viongozi kuungana na kutumia chama kimoja kama njia yao ya kisiasa katika ukanda wa pwani.

Bw Kingi amenukuliwa akisema kuwa kuwepo kwa umoja wa wanasiasa na viongozi wa pwani ndio njia ya kuondoa umateka wa kisiasa.

Kulingana na Bw Kingi iwapo viongozi wa ukanda wa pwani wataendelea kuwa katika vyama tofauti, basi itakuwa vigumu sana wao kujadiliana masuala kwa pamoja kwani kila chama kitakuwa na mambo yake.

Hivi majuzi akiwa katika hafla ya kuadhimisha miaka ishirini tangu aliyekuwa mwanasiasa mashuhuri wa pwani marehemu Karisa Maitha kuaga dunia, Bw Kingi alisisitiza sana umuhimu wa umoja wa kisiasa baina ya viongozi wa ukanda wa pwani.

Licha ya kauli mbiu ya Bw Kingi ya kutaka umoja wa kisiasa, maswali kadhaa yameulizwa iwapo lengo lake ni umoja wa viongozi wa ukanda wa pwani au yeye ndiye anayetaka mamlaka ya uongozi wa pwani.

Swali lingine linaloulizwa ni iwapo viongozi wengine wa ukanda wa pwani wataunga mkono wito huo wa Bw Kingi wa kutaka kuwepo na umoja.

Baadhi ya wachanganuzi wa siasa wanadai kuwa Bw Kingi kupigia debe suala la umoja wa viongozi katika ukanda wa pwani ni la kimaslahi wala sio kwa minajili ya wakazi.

Hata hivyo, madai hayo yanapingwa na baadhi ya washikadau katika mchakato mzima wa kisiasa wakisema kuwa kwa sasa Bw Kingi ndiye kiongozi wa ngazi ya juu serikalini kwa hivyo ana haki ya kupigia debe suala la umoja wa pwani.

Mchanganuzi wa siasa Bw Shukrana Mwabonje alisema kuwa kabla ya Bw Kingi kuanzisha chama cha Pamoja African Alliance (PAA), maswali yaliulizwa ni kwa nini alikuwa anakiunda chama hicho ilhali kulikuwa na vingine vyenye asili ya pwani ambapo angeweza kujiunga navyo kuendeleza umoja huo.

“Hata kama si yeye wa kwanza kusema kunahitajika umoja wa viongozi wa pwani kupitia chama kimoja huo wito wake si kwa maslahi ya wananchi,” alisema Bw Mwabonje.

Alidai kuwa Bw Kingi anataka kuwa kiongozi au msemaji wa ukanda wa pwani na kwamba suala la umoja wa pwani ni jambo zuri lakini Spika huyo wa seneti bado hajatosha kuendeleza mjadala huo.

Bw Mwabonje alidai kuwa maslahi ya Bw Kingi ya kisiasa ndiyo yanayomuondoa katika nafasi ya kuchukua uongozi katika mchakato huo mzima wa umoja wa pwani.

Mchanganuzi mwingine wa siasa Bw Sammy Rua alisema kuwa wito wa Bw Kingi wa kutaka umoja wa viongozi wa pwani ni jambo ambalo viongozi wanafaa kuliunga mkono.

“Nitafurahi sana iwapo ukanda wa pwani utafuata mkondo mmoja wa kisiasa ndiposa masuala yetu yatajadiliwa kupitia chombo kimoja,” alisema Bw Ruwa.

Aliongeza kusema kuwa Bw Kingi ndiye kiongozi mkuu kati ya viongozi wa pwani nchini kwani yeye ni nambari nne kutoka kwa Rais.“Kwa hivyo, yeye ndiye sauti ya pwani, Bw Joho na Bw Mvurya wao ni mawaziri, kwa sasa yeye ndiye kiongozi mkuu wa kisiasa katika ukanda wa pwani na kando na kuwa Spika yeye ni kiongozi wa chama ambacho kina wawakilishi bungeni,” alisema Bw Ruwa.

Bw Ruwa aliongeza kusema kuwa kwa sasa Bw Kingi ndiye kiongozi wa ukanda wa pwani katika siasa za nchi.

Mnamo Oktoba 2023, Bw Kingi akizungumza katika kaunti ya Tana River alisema kuwa wakati ulikuwa umefika kwa wakazi wa Pwani kujiuliza kuwa baada ya rais Ruto kumaliza awamu zake mbili mwaka wa 2032, watakuwa wapi?

“Safari ya kesho hupangwa leo, shida kubwa ambayo tumekuwa nayo sisi watu wa pwani ni kwa sababu hatujipangi na safari zinazokuja na kwa sababu hatujipangi saa zote tunabebwa. Wakati umefika pwani ikae na ipange safari yake ya kisiasa kwa safari inayokuja,” alisema Bw Kingi wakati huo.

Mwezi wa Aprili 2024 katika hafla moja jijini Mombasa, matamshi ya Bw Kingi kusema kuwa umoja wa ukanda wa pwani kisiasa utaendelea iwapo viongozi wataacha kuwa vikaragosi wa kisiasa yalikuwa yamezua mjadala mkali huku baadhi ya wakazi wakiunga mkono kauli hiyo.

“Tatizo kubwa sisi ni vikaragosi wa kisiasa na kama vikaragosi kuna mwenyewe anaivuta. Viongozi wa pwani lazima tuache kuwa vikaragozi wa kisiasa,” alisema Bw Kingi.