Choo ambacho landilodi Kirinyaga alitumbukia. PICHA|MWANGI MUIRURI
NA MWANGI MUIRURI
MWANAMKE wa miaka 60 ambaye ni mmiliki wa nyumba ya kukodisha katika Kaunti ya Kirinyaga alinusuriwa kifo baada ya choo alichokuwa akijisaidia kuporomoka.
Mwanamke huyo anamiliki nyumba ambazo zinatumiwa na wanafunzi wa chuo kikuu cha Kirinyaga, katika Kijiji cha Gitwe.
Kwa mujibu wa ripoti ya polisi iliyoandaliwa kuhusu mkasa huo, mwathiriwa alikuwa ameenda kutii msukumo wa haja kubwa ambapo akijikunyata ndani choo kiliporomoka na kumrusha ndani ya mkusanyiko wa mkojo na kinyesi.
“Harakati za majirani na maafisa wa kiusalama zilichukua dakika 36 kumnusuru,” ripoti hiyo yasema.
Inaongeza kwamba alikuwa amezirai lakini baada ya kupepetewa hewa safi akarejelewa na fahamu zake.
Alikimbizwa hadi hospitali ya Kerugoya kutibiwa na akapewa ruhusa ya kurejea nyumbani.
Bw Geoffrey Miano ambaye ni mwanafunzi alisema kwamba “hatuombei yeyote mabaya lakini tunashukuru Mungu kwamba mmiliki wa choo hicho ambacho hata sisi hukitumia ndiye alipata ajali ndani yacho”.
Alisema kwamba wanafunzi na wapangaji wengine wamekuwa wakiteta kuhusu hali mbovu ya vyoo ndani ya ploti yake lakini hawakuwa wakisikizwa.
“Tuna matumaini tele kwamba landilodi wetu sasa atawajibikia hali ya vyoo. Amegundua kwamba hata yeye anaweza akaangamia katika hatari za wapangaji,” akasema.