• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 5:50 AM
Lango maalum la kuingia mji wa Lamu ambalo usipolipitia ‘kitakuramba’

Lango maalum la kuingia mji wa Lamu ambalo usipolipitia ‘kitakuramba’

NA KALUME KAZUNGU

MJI wa Kale wa Lamu unatambulika ulimwenguni kote kutokana na jinsi wakazi wa eneo hilo walivyofaulu kuhifadhi mila, tamaduni na desturi zao.

Ni kutokana na sifa hizo ambapo mwaka 2001 Shirika la Umoja wa Mataifa Kuhusu Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO) liliuorodhesha mji huo kuwa miongoni mwa maeneo machache duniani yanayotambulika kwa historia zao za kipekee-yaani Unesco World Heritage Site.

Unapoingia kwenye mji wa kale wa Lamu utakaribishwa na lango maalum ambalo liko na mianya miwili.

Mwanya mmoja ni mpana, ambapo huwezesha watu wengi kupita kwa wakati mmoja.

Mpenyezo huo mpana pia huwezesha waja waliobeba mizigo, iwe ni kutumia miguu, mikokoteni au punda kupita bila kuweweseka.

Kwenye lango hilo, kuna sehemu ya pili nyembamba ambayo imetengwa kumwezesha mtu mmoja au wawili kupita kwa kupishana.

Kulingana na wazee wa Lamu, lango hilo kuu la kuingilia mji wa kale wa Lamu limekuwepo tangu miaka kabla ya ukoloni.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Lamu na Mwanahistoria, Mohamed Mbwana, anasema wasichokifahamu wengi ni kwamba lango hilo siyo sehemu ya kupitia tu bali limebeba majukumu mengi si haba.

Punda wakibeba mizigo kupitia lango kuu la kuingilia mji wa kale wa Lamu. Picha|Kalume Kazungu

Bw Mbwana anasema lango hilo kuu ndilo lenye kuutambulisha rasmi mji wa kale wa Lamu na historia yake.

Utapata sehemu ya juu ya lango hilo ikiwa imeandikwa kwa maandishi makubwa, ‘Welcome to Lamu, a UNESCO World Heritage Site,’….yaani karibu Lamu, Eneo la Kihistoria Litambuliwalo na UNESCO.

“Lango letu kuu limekuwepo tangu jadi, yaani zama kabla ya ukoloni. Limekuwa likitumika kama mdomo au mlango wa pekee kwa wanaoingia na kutoka kwenye mji wetu wa kale. Baada ya mji kupokea hadhi ya UNESCO mnamo 2001, hapo ndipo lango letu lilipofanyiwa ukarabati. Likajengwa na kupewa sura ya kuvutia zaidi. Pia maandishi ya kukaribisha wenyeji, wageni na watalii mjini yalichorwa,” akasema Bw Mbwana.

Isitoshe, lango hilo kuu ndilo linalotumika kuwaingiza wageni, iwe ni mashuhuri au wa kawaida na watalii, hasa wale wanaoingia Lamu kwa mara ya kwanza.

Kulingana na mzee wa Lamu, Omar Hassan, ni rahisi kwa mgeni au mtalii anayezuru eneo hilo kuuelewa vyema mji wa kale wa Lamu anapoingizwa kupitia lango hilo kuu kinyume na yule anayepitishwa kupitia vishorobani, vichochoroni au kwenye vipenyezo vya mji huo wa kihistoria.

“Mgeni au mtalii anayetaka kuufahamu kwa urahisi mji wetu wa kale lazima atembezwe na kupitishwa kwa kutumia lango letu kuu. Wanaotumia vishoroba vya mji wetu wa kale huishia kumchanganya mgeni au mtalii huyo,” akasema Bw Hassan.

Naye Bw Zubeir Alwy alifichua kuwa kutumia lango hilo kuu pekee humpa mja hadhi ya kuwa mwenye nidhamu na heshima kuu.

Bw Alwy anasema wanaokaidi kupitia lango hilo na badala yake kukimbilia kutumia mbinu ya mkato, ikiwemo vichochoro kuingia na kutoka mji huo wa kale  huoneana kuwa watovu wa nidhamu au waja waliopotoka kabisa kimaadili.

Anasisitiza kuwa endapo mtu atafaulu kuingia ndani ya mji wa kale na wa kihistoria wa Lamu bila kutumia lango hilo, basi yeye huzingatiwa au kutazamwa kuwa aliyepenya mjini kinyume au vivi hivi tu.

Sehemu mojawapo ya lango la kuingilia mji wa kale wa Lamu. Picha|Kalume Kazungu

“Na ndiyo sababu wageni mashuhuri, iwe ni Rais William Ruto, Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, Mawaziri, Wabunge, Maseneta na wengineo, wote hupitishwa kwenye lango hili kuu kuingia ndani ya mji wa kale wa Lamu. Ni maajabu endapo utaona watu hao wa hadhi kubwa wakitumia vichochoro kuingia Lamu,” akasema Bw Alwy.

Afisa Msimamizi wa Makavazi na Turathi katika Halmashauri ya Usimamizi wa Makavazi na Turathi za Kitaifa nchini (NMK) tawi la Lamu, Bw Mohammed Mwenje aliyataja malango hayo ya kuingilia na kutoka mji wa kale wa Lamu kuwa kiungo muhimu kwa eneo hilo.

Bw Mwenje aliwataka wananchi kulinda mwonekano wa malango hayo usiharibiwe, hasa na wale ambao wamekuwa na hulka ya kubandika makaratazi ya matangazo au ya kuuza sera, hasa kila msimu wa kampeni za kisiasa unapowadia.

Alishikilia kuwa malango hayo makuu ya kuingilia na kutoka mji wa kale wa Lamu ni mali ya NMK.

“Ukitazama utapata hata ujenzi wa malango hayo ulifuata kanuni au ramani za ujenzi zinazoambatana na hadhi ya mji wetu wa kihistoria. Utapata malango hayo yakiwa yamejengwa na kuwekewa nakshi sawasawa na ramani za nchi ya Omani zinazoshabihiana na misikiti. Tunakataza watu kuweka vibandiko vya aina yoyote kwenye malango hayo,” akasema Bw Mwenje.

  • Tags

You can share this post!

Ongezeko la wahuni wa ‘Marachi Boys’ kwenye mikutano ya...

Jinsi video ya ubakaji ya genge la wanaume saba ilifichuka

T L