Makala

Likizo ya EPL yaamsha hisia za siasa

June 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

KUTAMATIKA kwa michuano ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) katika msimu wa 2023-24 kumewafanya Wakenya wengi mashabiki wa soka kuingilia mijadala ya kisiasa, wakazi wa Mlima Kenya wakiathirika zaidi.

Kwa sasa, wengi na mapenzi walio nayo kwa EPL, hugeuza safu za mijadala kuhusu kabumbu nchini kuwa na taswira kwamba ni kama ndio tu ligi duniani.

Kwa kukosa ya kutaniana nayo wakingoja likizo hiyo iishe, mashabiki wengi wameingia kwa karata ya siasa.

“Mpira huunganisha Wakenya wengi hasa vijana. Hata ingawa kuna ligi nyingi duniani, hii ya EPL ndio maarufu zaidi hapa nchini huku nyingine kama za Uhispania, Ujerumani na Ufaransa zikiwa za wachache. Hata ligi yetu ya Kenya kwa mtazamo wa mashabiki, haina umaarufu,” asema Seneta Maalum Karen Nyamu.

Bi Nyamu anasema kwamba kwa sasa utaona maajabu ya Wakenya mitandaoni wakizidisha utani wa kisiasa na labda sarakasi za mapenzi ili kujaza pengo la EPL.

Askofu matata Yohana Gichuhi anasema kwamba licha ya kwamba dimba la Euro 2024 linakuja kuanzia Juni 14, 2024, hadi Julai 14, 2024, sio wengi nchini wanaelewa ratiba za michuano hiyo.

“Kwa sasa mitandaoni unaona tu Wakenya wakitaniana kuhusu makali ya EPL msimu ujao wa 2024-25 ambao utaanza rasmi Agosti ijayo. Kando na hilo, mijadala ni siasa za ushuru, uongo, utapeli, ubabe wa kisiasa na ufisadi,” asema Bw Gichuhi.

Mbunge wa Kiharu Bw Ndindi Nyoro anasema kwamba ingekuwa vyema ikiwa Wakenya wangesaka ufahamu wa kuunda bajeti ya nchi sawa na vile wao huzingatia masuala ya EPL.

“Mimi ni mwenyekiti wa Kamati ya kuunda bajeti hivyo ningefurahi kuona vijana wakijihusisha kikamilifu na suala hili jinsi ambavyo huwa ninakumbana nao ugani au katika kumbi za starehe wakati nikishabikia Manchester United yangu. Hili lingekuwa taifa bora zaidi katika mijadala ya kuunda hata Mswada wa Fedha,” asema Bw Nyoro.

Anasema mashabiki wa Manchester United, Manchester City, Liverpool, Chelsea na Arsenal wangekuwa na uzalendo wa kushabikia utawala bora nchini, hakungekuwa na dhana kwamba vijana wametengwa.

Hali ni tete kiasi kwamba mwanasiasa wa Laikipia Bi Cate Waruguru amemtaka mbunge wake wa Laikipia Mashariki Bw Mwangi Kiunjuri “akome kumchukulia Naibu Rais Bw Rigathi Gachagua kama wa ligi yake ndogo”.

Soma Pia: Sakaja, Nyoro na Kiunjuri walengwa wakiambiwa wamkome Gachagua

Anasema kwamba ikiwa Bw Kiunjuri hatamkoma Bw Gachagua, “tutamshinikiza aondoke kwa siasa na badala yake aingie kwa EPL akashabikie Man United”.

Mashabiki wa Man United wamekuwa wakirejelewa na wapinzani wao kama ‘Kiburi FC’.

Seneta wa Murang’a Bw Joe Nyutu anasema kwamba mijadala ya kisiasa imezidi mashinani na “uchunguzi wangu umebaini kwamba hali hiyo inachangiwa na pengo la EPL”.

“Kusema ukweli, hata mimi niko kwa mataa kiasi… Kuna vile timu yangu ya Arsenal hunipa sababu ya kuchangamkia wikendi. Kwa sasa wikendi muda mwingi utanipata ama kwa marafiki, kwa nyumba au kanisani,” asema Bw Nyutu.

Anaongeza kwamba kwao Murang’a, mijadala ni kuhusu siasa za 2027, 2032, Rais mstaafu Uhuru Kenyatta, ushuru na mafuriko huku katika hayo yote, kukipenyezwa siasa kali.

Kwa upande mwingi, Bw Nyutu anasema mpira wa EPL huwalinda wanasiasa dhidi ya mashambulio ya watu mitandaoni.

“Kusema ukweli, hata sisi wanasiasa hupenda jinsi mpira unavyowaweka na kuteka nyara muda wa Wakenya wengi na hasa vijana kiasi kwamba furaha yao ya ushabiki huwanyima yale makali ya kutushambulia kwa mitandao,” asema seneta huyo.

Bw Nyutu anasema kwa sasa ukiangalia mitandao utapata siasa zimeamka kwa kiwango kikuu na cheche ni nyingi na moto.