Makala

LISHE: Jinsi ya kupika wali wa nazi

June 16th, 2020 Kusoma ni dakika: 1

Na MISHI GONGO

Vitu vinavyohitajika

Idadi ya walaji ni watu 6

Mchele pishori kilo moja

Kijiko kidogo cha chumvi

Nazi moja kubwa

Jinsi ya kutayarisha

Osha mchele wako kisha uweke pembeni.

Anza kwa kukuna nazi yako kisha iweke katika kifumbu.

Chicha za nazi baada ya kukuna nazi. Picha/ Mishi Gongo
Chicha za nazi ndani ya kifumbu. Picha/ Mishi Gongo

Chukuwa sufuria kisha ujaze maji ujazo wa robo tatu.

Minya kifumbu ulichokiweka ndani ya dishi kwa kiganja na dole gumba ili kupata tui nzito. Weka pembeni tui hilo.

Tui nzito. Picha/ Mishi Gongo

Kutumia maji uliyoyatenga katika sufuria, teka kidogo kidogo ukiongezea kwa kifumbu huku ukiendelea kuminya ili kupata tui jepesi.

Bandika sufuria iliyo na tui jepesi motoni, subiri hadi lianze kuchemka kisha tia mchele.

Tui jepesi. Picha/ Mishi Gongo

Mchele unapoanza kutokota, tia chumvi ukikoroga.

Unapoanza kuona maji yamesalia kidogo ongeza tui nzito halafu koroga hadi lichanganyike na mchele.

Funika sufuria kwa kifuniko bapa, weka makaa kiasi ya moto juu ya kifuniko hicho na ubakishe makaa kiasi katika jiko, kama unavyofanya ukioka keki.

Subiri muda wa dakika tano ili wali wako uvute maji kisha pakuwa.

Unaweza kuandaa wali wa nazi kwa mchuzi wa kuku au maini ya kukaanga, ukiongezea na sharubati ya machungwa au pesheni.