Liverpool dhidi ya Man City, WanaArsenal wakiomba droo
NA MWANGI MUIRURI
MASHABIKI wa Arsenal nchini wakiongozwa na Seneta maalum, Karen Nyamu wanasubiri kwa hamu na ghamu jinsi mgaragazano wa Manchester City na Liverpool leo jioni, Jumapili, Machi 10, 2024 katika mtanange wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) utakavyoishia, maombi yakiwa ni wawili hao watoke droo ili timu kipenzi chao isalia juu ya jedwali.
Ngozi itatamba mwendo wa saa moja kasorobo, katika uga wa Anfield.
Kwa sasa, Arsenal almaarufu ndovu ndio imekalia juu ya mti ikiwa na pointi 64, Liverpool ikifuata kwa ponti 63 nao Man City wakiwa na alama 62.
Iwapo Liverpool itashinda na kupaa hadi pointi 66, basi ndovu atashuka hadi chini ya meza kujiunga na wenyeji wa kupigwa Man United na Chelsea.
Na iwapo Man City itashinda na kupaa hadi pointi 65, ndovu atashuka tu hivyo basi maombi yakiwa ni droo kwa timu hizo mbili.
Droo itaweka Liverpool kwa pointi 64 sawa na Arsenal lakini wanabunduki wa mkufunzi Mikel Arteta wabakie tu kidedea kwa ubora wa mabao huku Man City ikiridhika na nafasi ya tatu kwa pointi 63.
Bi Nyamu alisema “hii ni droo kwa kuwa mahasidi wetu wakuu ambao ni Manchester United wanaombea Man City ushindi”.
Nyamu alisema Man U hawajawahi kusamehe Liverpool tangu Machi 5, 2023 ambapo iliwapa aibu ya kudumu kwa kuwatunuku kichapo cha mabao 7-0 kupitia mashuti ya Gakpo kunako dakika ya 43 na 50, Nunez kwa dakika za 47 na 75, Salah akazidisha nduru katika dakika za 66 na 83 naye Firmino akirembesha aibu zaidi katika dakika ya 88.
Celeb wa mwezi Februari 2024 kwa jina Askofu Danson Gichuhi almaarufu Askofu Yohana alisema kwamba kwa sasa roho wote watatu ambao ni yule mtakatifu, wa ibilisi na pia yule mtaka kitu hawajamwelezea kwa uwazi ni nani ataibuka mshindi kati ya Man City na Liverpool.
“Lakini roho binafsi ya Askofu Yohana iko katika beti ya droo. Hiyo itakuwa sare kwa kuwa Arsenal yetu inafaa tu kubakia juu hadi mwisho wa tamati ili tuinue hili taji la EPL ambalo limetuhepa tangu msimu wa 2003/4 ambapo tuliliinua mara ya mwisho,” akasema.
Askofu Yohana alikuwa ametabiri ushindi wa Arsenal dhidi ya Brentford katika mechi ya Jumamosi (Machi 9, 2024) usiku kwa mabao 2-1 na ikaishia kuwa hivyo.
“Hapo roho mtakatifu alikuwa amenifunulia hali kwa uhakika. Lakini kwa hii ya leo kuna wingu la sintofahamu na ndilo natafsiri kuwa itakuwa ni droo,” akasema.
Katika mechi hii kubwa, Liverpool wanaingia katika uga wao wa nyumbani wa Anfield wakiwa wanachechemea kutokana na majeraha tele.
Vijana hao wa meneja wa Jurgen Klopp wana orodha ya Thiago Alcantara, Trent Alexander-Arnold, Stefan Bajcetic, Alisson Becker, Ben Doak, Wataru Endo, Ryan Gravenberch, Curtis Jones, Joel Matip, Darwin Nunez, Dominik Szoboszlai na Mohamed Salah ambao watakuwa nje wakiugua.
Kwa upande wa meneja Pep Guardiola wa Man City, atakuwa na majeruhi Jack Grealish, Jeremy Doku na Matheus Nunes wakiwa nje.
Lakini kuna matumaini kwamba Doku huenda awe tayari kuwajibikia majukumu.
Timu hizo zinakutana huku Man City ikiwa imeibuka na ushindi mara mbili dhidi ya mbili katika mechi tano mtawalia za hivi punde dhidi ya Liverpool na kutoka sare mara moja, hesabu ikiwa ni nguvu sawa.
Lakini karata ya mpira ikiwa matokeo ni moja kati ya ushindi, kupoteza, droo au mechi itamatishwe ghafla, kipenga cha mwisho ndicho huwa cha matokeo ya uhakika.