Lizzie Wanyoike alivyonusurika kifo 1960
NA MWANGI MUIRURI
HUKU taifa likimwomboleza mwekezaji Lizzie Muthoni Wanyoike aliyeaga dunia Januari 14, 2024 akiwa na miaka 73, sio wengi wanafahamu kwamba aliepuka mauti mwaka wa 1960 kutokana na homa ya matumbo.
Baba yake akifahamika kama Peterson Kariuki aliyekuwa chifu wa kikoloni katika Kaunti ya Murang’a, alikuwa amekamatwa na kufungwa jela miaka saba kwa madai ya kushirikiana na kikosi cha kupambania uhuru cha Mau Mau.
“Kipindi hicho tulikuwa tumekusanywa katika kijiji cha kikoloni ambapo mazingara yalikuwa duni na ndipo kakangu, mimi pamoja na dadangu tuliugua homa hiyo hatari,” Bi Wanyoike aliambia Taifa Leo Dijitali katika mahojiano ya kipekee kabla ya mauti kumkumbatia.
Kwenye mahojiano hayo ya Mei 15, 2023 Bi Wanyoike ambaye ni mwanzilishi wa taasisi ya Nairobi Institute of Technology and Business Studies alisema kwamba angekuwa hayati Mungu angekosa kumnusuru.
Aliongeza kwamba dadake aliaga dunia katika harakati hizo za kuugua, lakini yeye pamoja na kakake wakanusurika.
“Mimi ndiye niliathirika zaidi kwa kuwa nililazwa katika hospitali kwa kipindi cha miezi miwili. Nilikuwa najipata nikififia, huku mauti yakiniandama,” akasema.
Aliongeza kwamba alikuwa akijipata akipaa angani huku malaika wakimngoja, japo alikuwa akikatalia uhai wake kwa imani kuu.
“Nilikuwa na miaka tisa lakini nakumbuka jinsi hata nilikuwa nikiota kuhusu maisha ya baada ya kifo. Madaktari walikuwa wakatili tu na kwa wakati mmoja waliniachia dawa za tembe nimeze kivyangu licha ya unyonge wangu,” akasema.
Bi Wanyoike alikumbuka jinsi hakuwa na nguvu za kumeza dawa hizo, akielewa umuhimu wa kuzimeza na ndipo hata alipopoteza fahamu zake, akabakia amezikumbatia kwa mkono wake wa kulia.
“Katika dunia ya kutofahamu, niliota kuhusu joka kubwa lililokuwa likininyemelea lakini kabla linifikie likakumbana na panya. Joka hilo lilishambulia panya huyo na likammeza akiwa mzimamzima na katika taharuki yangu, nikaamka kwa kishindo nikipiga nduru na nikapata madaktari wamenizingira,” akasema.
Alisema kwamba madaktari hao walionekana kushtuka waziwazi kwa kuwa walikuwa wanajiandaa kumtoa kama maiti wakimdhania alikuwa ameshaaga dunia.
“Walipata dawa kwenye mkono wangu, wakanipa nimeze na baada ya siku kadha nilipona na kuondoka hospitalini, nikapata dadangu aliyeaga alikuwa tayari amezikwa,” akasema kwa huzuni.
Bi Wanyoike alisema kwamba kisa hicho cha kuugua kilimfanya awe na huruma nyingi sana kwa wagonjwa “na hadi leo hii huwa silali kabla ya kuwaombea wagonjwa wote na la mno, madaktari waingiwe na utu wa kuhudumia wagonjwa”.
Kando na taasisi hiyo ya elimu, Bi Wanyoike ni mwekezaji katika sekta ya hisa, mashamba, shule ya msingi kwa jina Lizzie Wanyoike Preparatory na pia Mkahawa wa Emory ulioko Jijini Nairobi.
Pia, ni mwanzilishi wa Wakfu wa Lizzie Wanyoike.