Makala

Lizzie Wanyoike alivyowindwa na vijana kijijini kama swara

January 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA MWANGI MUIRURI

LIZZIE Wanyoike aliyeaga dunia Januari 14, 2024 alizaliwa katika kijiji cha Gathukiini, Kaunti ya Murang’a mwaka wa 1951 akiwa wa sita kati ya watoto 10 wa mzee Peterson Kariuki na mama Naomi Kariuki.

Familia yao ilikuwa ya wasichana watano na wavulana watano.

Katika kitabu alichokuwa ananuwia kuchapisha kikifahamika kama Staircase, Bi Wanyoike alielezea kwamba maisha yake yalikuwa ya kawaida huku akisaidia katika majukumu ya kulima shamba, kuchuma kahawa na pia kupeleka mahindi kwenye kisiagi.

Anasema kwamba nyanyake –  mzazi wa babake Bi Mariamu Wangari, alimshawishi sana katika maisha yake ya utotoni kutokana na mapenzi yake ya bidii na elimu.

“Nyanyangu alikuwa na ulemavu wa mguu na hakuwa na elimu yoyote. Lakini licha ya kuachwa akiwa mjane baada ya miaka 10 pekee katika ndoa yake, alijizatiti na akakumbatia elimu kwa watoto wake wote na ndipo babangu aliishia kuwa mwalimu,” akasema.

Alisema kwamba kuelimisha watoto katika enzi hizo kulikuwa kunakemewa kwa kuwa wengi walidhania ilikuwa ni njama ya kumuunga mkono mbeberu azidi kutawala taifa hili.

Babake Lizzie, Wanyoike aliishia kuwa mwalimu wa shule ya msingi kitaaluma lakini hatimaye akaajiriwa kama chifu huku naye mamake ambaye pia alikuwa mwalimu akiachana na kazi baada ya kuolewa.

“Hizo zilikuwa zile nyakati ukiolewa, unaacha kazi ya ajira ili uchukue kazi yako mpya kama mke nyumbani wa kuzaa na kutunza watoto,” akasema.

Bi Wanyoike alipata masomo yake ya sekondari katika Shule ya Upili ya Kahuhia iliyoko Murang’a kabla ya kuelekea Nakuru kwa kidato cha tano na sita na hatimaye akajiunga na taasisi ya Kenyatta (wakati huu ikiwa ndiyo chuo kikuu cha Kenyatta) kusomea taaluma ya ualimu na ukarani.

“Katika maisha yangu ya kijijini, wavulana hawakuwa wakipata usingizi na kuchumbiwa ilikuwa ni kawaida, kila mmoja akisema nilikuwa namnyima usingizi kwa sababu ya urembo wangu,” akaandika.

Anasema kilichomnusuru dhidi ya mimba na ndoa za mapema ni historia ya babake kuwa chifu, mama ambaye hakuwa mpole kwa kusisitiza nidhamu na waalimu kumkalia ngumu.

“Kuna visa kadha ambapo nikiwa katika shule ya upili ya Kahuhia walimu walipata barua yangu ya kuchumbiwa na wakaisoma hadharani wanafunzi wengine wakiwa. Nilikuwa nimepewa sifa motomoto za urembo lakini aibu hiyo ilinifanya nikae mbali sana na mapenzi kwa vijana,” akasema.

Babake aliaga dunia 2002 akiwa na umri wa miaka 86 huku naye mamake akiaga 2018 akiwa na miaka 90.

Anasena msingi huo wa malezi ndio ulimpa ari ya kusaka mali na pia kulea vizazi katika sekta ya elimu ambapo ndiye mwanzilishi wa Taasisi ya Nairobi Institute of Technology and Business Studies na pia Lizzie Wanyoike Preparatory School.

[email protected]