Lizzie Wanyoike kuzikwa Gatanga kwa mumewe mnamo Januari 23
NA MWANGI MUIRURI
MAREHEMU Lizzie Wanyoike ambaye ni mwanzilishi wa Nairobi Institute of Technology and Business Studies, aliyeaga dunia Jumapili iliyopita, atazikwa mnamo Januari 23, 2024, katika eneobunge la Gatanga.
Bi Wanyoike aliugua saratani ya mishipa ya uzazi ambayo huwa nadra kwa wanawake lakini ikiwalemea walio na umri wa zaidi ya miaka 63.
Kwa mujibu wa ratiba ambayo ilitolewa rasmi na familia yake ya watoto watatu ambao ni Antony, Stella, na Eric Mburu, mazishi hayo yatafanyika katika shamba la mumewe Bw Mburu Wanyoike ambaye aliaga dunia mwaka wa 2018.
Bw Wanyoike anafahamika kama mkurugenzi wa awali wa Shirika la Maziwa Nchini (KCC) na pia mbunge wa Gatanga kati ya 1992 hadi 1997.
Baada ya kumuoa Lizzie mnamo mwaka wa 1972 na kuishi pamoja kwa miaka 25, waliachana huku Bi Wanyoike akizindua harakati za uwekezaji ambazo kwa miaka mingine 25 hadi kifo chake, zilikuwa zimemjenga hadi kuwa bilionea.
Waliachana mwaka wa 1997 lakini Bi Wanyoike alikuwa akisisitiza kwamba ndoa yao ilisambaratika kutokana na mtazamo wa kiuwekezaji wala sio kwa msingi wa tofauti za hisia za mapenzi kati yao.
“Licha ya kwamba tuliachana, siwezi kamwe nikaongea kuhusu ubaya wowote wa Bw Wanyoike kwa kuwa yeye ndiye alinipa msingi wa uwekezaji na yote niliyo nayo ni kutokana na uhusiano wangu naye,” akasema Bi Wanyoike katika mahojiano na Taifa Leo mnamo Machi 23, 2023.
Kwa mujibu wa familia, maombi ya maandalizi ya mazishi yalianza Jumanne na yataendelea katika boma lake lililoko katika mtaa wa Garden Estate. Misa ya kumuenzi mwendazake itafanyika mnamo Januari 18, 2024, katika Kanisa la Anglikana la St Joseph wa Arimathea katika mtaa wa Thome.