Makala

LOSFOU: Nalenga kumfikia Diamond Platnumz

June 24th, 2020 Kusoma ni dakika: 2

Na JOHN KIMWERE

‘MGAAGAA na upwa hali wali mkavu,’ ni methali inayohimiza wanadamu wasiwahi vunjika moyo kwenye jitihada za kutaka kutimiza malengo fulani maishani mwao.

Pia imethibitishwa na wengi wanaozidi kushangamkia shughuli tofauti kwenye juhudi za kusaka riziki. Miongoni mwao ni msanii anayekuja, Duncan Musyoka Wambua maarufu Losfou, anayeamini ana talanta tosha kutinga kiwango cha wanamuziki maarufu duniani.

Msanii huyu hughani nyimbo zake kwa mtindo wa Afrodance. Katika mpango mzima Losfou amesema amepania kutinga kiwango cha wasanii wakubwa Afrika Mashariki na Afrika kwa jumla kama Diamond Platnumz na Jose Chameleone kati ya wengine.

”Kando na muziki ninamiliki brandi ya kukuza talanta za wasanii chipukizi inayofahamika kama Kipawa Afrika,” amesema na kuongeza kuwa analenga kuibuka maarufu ndani ya miaka michache ijayo.

Chipukizi huyu alianza kujituma katika masuala ya muziki tangia akiwa mwanafunzi wa Shule ya Msingi.

”Napenda muziki ambapo sina budi kutaja kuwa mwanzo wa ngoma nilikuwa nafanya nyimbo za injili kabla ya kugeukia muziki wa kidunia mwaka 2010,” alisema na kuongeza kwamba muziki ndio kitega uchumi kwake.

Alifanya muziki wa injili ndani ya miaka miwili alikojivunia kuachia albamu moja kwa jina Mzazi iliyosheheni fataki sita zikiwamo:’Mzazi,’ ‘Wewe ni Bwana,’ ‘Majukumu,’ kati ya zingine.

Mwimbaji huyu anajivunia kutunga zaidi ya teke 200 lakini amefaulu kurekodi nyimbo 30 pekee kutokana na ukosefu wa fedha. Kwenye muziki wa kidunia mwimbaji huyu anajivunia kuachia albamu mbili ‘Kalunde’ na ‘Bigway,’ ambapo kwa sasa anaendelea kuandaa teke za albamu ya tatu.

Albamu ya Kalunde inashirikisha nyimbo kama:’Kalunde,’ ‘Amua,’ ‘Wendo waku,’ ‘Tina,’ na ‘Penzi lako,’ kati ya zingine. Nayo albamu ya First Love inajumuisha teke kama:’Firstlove,’ ‘Penzi lako,’ ‘Usalama,’ ‘Kiwewe,’ ‘ Masaibu,’ kati ya zingine.

Hivi karibuni ametunga nyimbo kama ‘Clear My way,’ na ‘With You’ ambazo zimefanyiwa kazi na produsa Coin Touch raia wa Uganda mmiliki wa SweetBeats Production ya jijini Nairobi katika mtaa wa Pipeline.

Nyimbo za utunzi wake zilipata mpenyo na kuanza kuchezwa kwenye vyombo vya habari mwaka 2013 pale wimbo wa Penzi lako ulipopeperushwa kupitia K24 TV. Pia ilichezwa na vituo zingine ikiwamo Mbaitu FM, Milele FM na County FC katika Kaunti ya Kitui.

Katika ukanda wa Afrika Mashariki huvutiwa na nyimbo za wasanii wengi tu kama Otile Brown ‘Chaguo la moyo,’ na Aslay ‘Muhudumu,’ ‘Lover Boy,’ ‘Barnaba,’ kati ya zingine. ”Kiukweli namtambua mwimbaji huyo wa Bongo Flava nyimbo anafanya kazi ya kupendeza na kuigwa na wengi,” alisema na kuongeza kuwa anatamani sana pia kufikia kiwango chake. Kadhalika anakiri kuwa anatamani sana kufanya kolabo na mwimbaji huyo endapo atapewa nafasi hiyo.

Anadokeza kuwa muziki wa Kenya unayo nafasi ya kupiga hatua na kifikia kiwango cha wenzao wa Bongo Flava lakini yapo mengi yanayohitaji kushughulikiwa kwa kina.