Changamoto za Waboni wakisaka elimu, usasa
JAMII ya Waboni inajua jinsi ya kuendesha maisha ya msituni ambayo wengi huenda wasifaulu kwa jinsi walivyozoea usasa.
Ni jamii ya wachache ambayo tangu jadi inatambulika kutokana na kwamba uchumi wao ni wa pekee, ambapo hujumuisha kuwinda wanyamapori, kurina asali ya msituni na kuchuma matunda ya mwituni.
Jamii ya Waboni hupatikana kwenye vijiji zaidi ya kumi vilivyoko ndani ilhali vingine vikipakana na msitu mkuu wa Boni, Kaunti ya Lamu.
Vijiji hivyo ni Milimani, Basuba, Mangai, Mararani, Kiangwe, Bodhei na Madina, vyote vikiwa eneobunge la Lamu Mashariki.
Vijiji vingine vya Waboni ambavyo vinapatikana Lamu Magharibi ni Bar’goni, Pandanguo na Jima.
Miaka ya hivi sasa Waboni wamekuwa wakijitahidi kuendeleza harakati za kubadili maisha yao kutoka yale ya zamani na yanayoonekana kupitwa na wakati na kuibukia maisha yanayofungamana na karne ya sasa.
Miongoni mwa jitihada hizo ni kubadili kitega uchumi chao kutoka uwindaji wa wanyamapori, kuvuna asali ya msituni na kuchuma matunda ya mwituni na badala yake kuibukia kilimo ilmuradi wajikimu na kuendeleza maisha yao.
Isitoshe, serikali na wadau mbalimbali wamekuwa wakijikaza kuinasua jamii ya Waboni kutoka kwa ukale na kuihimiza kukumbatia usasa.
Jitihada hizo zinajumuisha kuwawezesha Waboni kuifikia elimu.
Ila jitihada hizo zimekuwa zikikabiliwa na vizingiti si haba, hivyo kuwafanya baadhi ya Waboni kuvunjika moyo kabisa njiani hadi wengine kufikia hatua ya kutafakari kurejelea yale yao ya kale ya ‘zilipendwa’.
Je, kwani jamii hii ya walio wachache ya Waboni ni yenye bahati mbaya? Ni changamoto zipi hasa zinazofanya wao kuvunjika moyo wakati wanaposaka kuyafikia maisha ya kisasa?
Taifa Leo ilichambua baadhi ya changamoto hizo. Kwanza, katika kipindi cha karibu miaka 10 iliyopita, jamii ya Waboni imekuwa ikikabiliwa na ukosefu wa usalama unaochangiwa na magaidi wa Al-Shabaab.
Utovu huo wa usalama ulisababisha serikali kufunga shule tano za msingi zilizoko katika msitu wa Boni na ambazo ni Milimani, Basuba, Mangai, Mararani na Kiangwe.
Hatua hiyo ilitokana na walimu waliokuwa wakihudumia shule hizo kutoroka eneo hilo kwa kuhofia usalama wao.
Ni hali iliyoitumbukiza jamii ya Waboni katika giza kwani watoto wao walisalia nyumbani bila kusoma kama wenzao wa maeneo mengine ya Kenya.
Mnamo 2015, serikali kuu ilianzisha operesheni ya usalama kwa jina Linda Boni, lengo kuu likiwa ni kuwasaka na kuwamaliza magaidi wa Al-Shabaab wanaoaminika kujificha ndani ya msitu huo mkuu wa Boni.
Ni operesheni iliyoitumbukiza jamii ya Waboni kwenye mashaka kwani serikali iliwapiga marufuku Waboni dhidi ya kuingia msituni kujitafutia riziki kama ilivyo ada yao.
Serikali na wadau wakajitokeza kuwafadhili Waboni kwa kilimo ila wadudu na wanyamapori wakavamia mashamba yao na kuifyeka mimea yao yote.
Waboni wakibaki hohehahe, tegemeo lao kuu likawa ni misaada ya chakula kutoka kwa serikali na mashirika.
Baadaye serikali na mashirika yaliyokuwa yakifadhili program hizo, ikiwemo lile la msalaba mwekundu yakaacha kuwapelekea Waboni misaada ya chakula na mingineyo ya kibinadamu.
Mwaka 2019, jitihada za serikali kuu za kuzifungua shule za msitu wa Boni zikaanza.
Wakati huo, zaidi ya wanafunzi 400 wa jamii ya Waboni walikuwa wamebaki nyumbani bila kuendeleza masomo yao.
Ni wakati huo ambapo serikali iliamuru shule za msingi za Waboni kufunguliwa na kuhudumia wanafunzi wa chekechea (ECDE) hadi darasa la nne. Wanafunzi wa madarasa ya juu wakihamishiwa shule ya Mokowe Arid Zone iliyoko Lamu Magharibi ambako kuna usalama wa kutosha.
Harakati hizo aidha zilikumbwa na changamoto zingine tele, ikiwemo walimu waliofaa kufundisha wanafunzi wa shule za msiu wa Boni kukosa kufika kwa wakati ufaao kutokana na changamoto za kiusalama.
Walimu hao walitegemea sana lifti kutoka kwa ndege za Jeshi la Ulinzi Kenya (KDF), hasa wale wanaotekeleza operesheni ya kiusalama mstituni Boni.
Ikumbukwe kuwa usafiri wa barabarani msituni Boni ni hatari kwani Al-Shabaab wamekuwa na hulka ya kutega vilipuzi kwenye barabara hiyo na kuishia kuwaua walinda usalama na raia.
Miaka nenda miaka rudi, shule za Waboni hazijakuwa zikihudumu ipasavyo kwani wanafunzi mara nyingi wamekuwa wakikaa muda mrefu majumbani na wazazi wao na hata kukosa kufanya mitihani yao ya muhula kwa kukosa walimu shuleni.
Kwa mfano, tangu shule zifunguliwe kote nchini kwa muhula wa pili karibu majuma matatu yaliyopita, shule nne za msitu wa Boni, ambazo ni Milimani, Mangai, Basuba na Mararani bado hazijafunguliwa kwani walimu hawajaweza kufika eneo hilo kutokana na changamoto za kiusalama.
Ikumbukwe kuwa ndege za KDF kwa sasa zinafanyiwa ukaguzi maalum hasa tangu ajali ya ndege iliyopelekea kifo cha aliyekuwa Mkuu wa Majeshi nchini, Jenerali Francis Ogolla na maafisa wengine tisa wa KDF kutokea mwezi jana.
Hali hiyo imechangia ugumu wa kupata ndege ya jeshi ya kuwasafirisha walimu hao karibu 30 kutoka uwanja mdogo wa ndege wa Mokowe hadi kwenye shule za msitu wa Boni, hivyo kuwaacha wazazi na watoto wao wakihangaika.
“Watoto wetu kukosa elimu kila mara twaona ni mateso. Hilo linaitumbukiza jamii yetu kwenye giza katika kuusaka usasa. Serikali ije na mikakati mipya ya kufadhili vijana wetu kusomea kozi za ualimu na baada ya kuhitimu warudi kwao kuihudumia jamii yao ya Waboni,” akasema Diwani wa Basuba na Msitu wa Boni, Bw Barissa Deko.
Bi Amina Gurba, mkazi wa Mangai, alihoji ni vipi jamii ya Waboni itajinasua kutoka kwa historia ya ‘ushamba’ na kuibukia usasa ikiwa jitihada zao zinazidi kulemazwa kila kukicha.
Kulingana na Bi Gurba, matarajio yao ya awali yalikuwa ni elimu iwe kiokozi cha pekee kwa jamii hiyo.
Matumaini yao yalikuwa ni watoto wao wasome vyema mfululizo, kuhitimu kozi nzurinzuri na kupata kazi, hasa zile za ofisini.
Wanaamini hilo lingefanyika na kufaulu vilivyo basi lingebadili kabisa maisha na taswira inayofungamana na Waboni.
Bi Gurba analalamikia kukatizwakatizwa kwa masomo ya watoto wao kuwa suala linalowavunja moyo njiani na kuwakeketa maini si haba.
“Serikali ilituzuia kuendeleza maisha na desturi zetu za jadi, ikiwemo kuingia msituni kuwinda wanyamapori, kutafuta asali mwitu na kuchuma matunda mwitu. Tulitarajia kwamba tuipate elimu vyema na watoto wetu wasome hadi kufikia upeo, wapate kazi nzuri ila yote yamekuwa ni ndoto za abunuwasi. Tumeachwa njia panda kuhusu mwelekeo wa maisha yetu kama Waboni,” akasema Bi Gurba.
Mbali na ukosefu wa elimu, miundomsingi, hasa usafiri kwenye vijiji vingi vya Waboni ni shida.
Barabara maeneo haya ni zile za vichochoro, mchanga na matope, hivyo ni vigumu kutumika.
Kufika kisiwa cha Lamu ili kujinunulia bidhaa na kurudi msitu wa Boni humgharimu mja fedha zisizopungua Sh12,000, hasa kwa pikipiki.
Wakazi hapa wanalazimika kutumia njia ya usafiri wa baharini kupitia boti na mashua ambao kidogo ni salama.
Ila wanaishinikiza serikali kuwajengea barabara za kisasa, kubuni vituo vya walinda usalama barabarani ili kuwawezesha pia kufurahia maisha kama wakenya wengine.
“Sisi pia ni raia wa Kenya. Serikali imekuwa ikiahidi kwama itajenga barabara zetu na ulinzi kudumishwa ili zipitike. Twashangaa kwamba yote yamekuwa stori tu ilhali serikali ikiendeleza kimya chake na kutuacha kuteseka,” akasema Bw Abdi Ali.
Changamoto nyingine zinazokabili Waboni ni ukosefu wa vituo vya afya vijijini mwao.
Zahanati za Milimani, Mangai, Mararani na Basuba zilifungwa tangu 2016 kufuatia hulka ya magaidi wa Al-Shabaab kuzilenga, kuiba dawa na kisha kuziteketeza.
Juhudi za serikali ya kaunti ya Lamu kuzifufua zahanati hizo hazijafaulu kwani hata madaktari na wauguzi hawako tayari kupelekwa kuhudumia hospitali za eneo hilo.
Hali hiyo imewaacha Waboni kuhangaika kwa kusafiri maeneo ya mbali, ikiwemo Kiangwe, Kiunga na kisiwa cha Lamu kutafuta matibabu.
Maafisa wa utawala wa serikali kuu waliozungumza na Taifa Leo aidha walisema jitihada bado zinaendelea kurejesha hali shwari eneo la Msitu wa Boni.
Naibu Kamishna wa Lamu Mashariki, Bw George Kubai alisema majadiliano yanaendelea kuona kwamba walimu wanaohudumia shule za msitu wa Boni wanasafirishwa hivi karibuni.
“Majadiliano yanaendelea. Changamoto ni ukosefu wa ndege ya kuwapeperusha msitu wa Boni ila hatujakufa moyo. Hivi karibuni walimu watafikishwa msituni Boni. Isitoshe, kunayo mengi serikali inafanya, ikiwemo kuendelea kupigana na magaidi na kurudisha hali shwari msituni Boni na Lamu kwa jumla ili maisha yasonge,” akasema Bw Kubai.