Lugha, Fasihi na Elimu

ELIMU: Jinsi ya kujibu maswali ya insha kutokana na hadithi fupi

Na GRACE OGOYE April 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MTAHINIWA anafaa kujua aina za maswali yanayotahiniwa na aelewe namna ya kuyajibu kikamilifu. Kuna aina mbili za maswali; maswali ya insha na maswali ya muktadha/dondoo.

Maswali ya insha humhitaji mwanafunzi kujadili suala lililoangaziwa akirejelea vitushi kwenye hadithi kama ithibati. Wahusika sharti warejelewe kwa majina waliyopewa na mwandishi.

Katika ‘Harubu ya Maisha’, tunawapata Nilakosi, Mercy na Kikwai. Wanaweza pia kutambulishwa kwa kurejelea mahusiano yao na wengine. Mamake Kikai na mama Mercy ni mifano.

Kuna wale wanaorejelewa kwa vyeo vyao kazini, mathalani Bosi na mhasibu.

Wahusika wanaweza kujitokeza kwa makundi. Kikwai anajumlisha wenzake kazini anapomweleza mama Mercy kuwa wote hawajapokea mishahara yao kwa miezi.

Majina ya mahali yadumishwe. Katika ‘Msiba wa Kujitakia’, jimbo husika linaitwa Matopeni huku kiwanja kulikoandaliwa sherehe ya kumwapiza kiongozi Sugu Junior kinaitwa Mamboleo.

Sehemu pia huenda zikarejelewa kwa majina ya jumla. Kwa mfano, katika ‘Fadhila za Punda’, Lilia alihamishwa kutoka mjini hadi kijijini kwa amri ya Luka, mumewe. Alipopigwa nusura kufa, mama mkwe alimkimbiza hospitalini.

Iwapo swali ni funge, mtahiniwa hubainishiwa idadi ya hoja za kujadili.

Mfano:

Ainisha sifa nne za Sabina. Mwanafunzi anatazamiwa kutaja sifa nne pekee na atoe ithibati kwenye hadithi. Ijulikane kuwa hoja za ziada hazisahihishwi na hivyo hazichangii matokeo bali humpotezea mwanafunzi wakati.

Ikiwa swali ni wazi, ina maana kuwa idadi ya hoja za kujadiliwa haijatajwa. Hivyo, ichukuliwe kwamba idadi ya hoja za kuandikiwa ilingane na idadi ya alama zilizotengewa swali.

Wakati wa kuelezea hoja, mtahini atengee kila hoja aya yake. Sentensi ya kwanza ya aya itaje hoja. Sentensi zinazofuata zitumike kupambanua hoja hiyo. Sentensi inayokamilisha aya irejelee matukio kwenye hadithi.

Mfano:

Eleza dhiki zinazowakumba waajiriwa katika hadithi ya ‘Harubu ya Maisha’. (Alama 10)

Wafanyikazi hushindwa kukimu mahitaji yao wanapokosa kulipwa mishahara yao.

Kikwai hakuweza kuilisha familia yake kwa kukosa fedha za kugharimia ununuzi wa chakula. Haya yanadhihirika inapombidi akakope unga, mayai na mboga kutoka kwa Vaite.

Wafanyikazi huhangaishwa na mishahara inayocheleweshwa kulipwa.

Landilodi wa Nilakosi alitishia kumfungia nyumba kwani mwisho wa mwezi ulikuwa umewadia. Hali hii inamlazimu Nilakosi kuchelewa kufika kazini.

Wafanyikazi huachishwa kazi ghafla bila taarifa.

Bosi anawazia kuikatiza ajira ya Nilakosi japo muda walioafikiana na kuandikiana kandarasi haujakamilika. Ina maana kuwa wafanyikazi huishi wakihofia kubaki bila njia ya kujitegemea.

Tathmini: Zifafanue changamoto nyingine zinazojitokeza katika hadithi hii.