GWIJI WA WIKI: Mwalimu Samuel Sinzore
SAMUEL Sinzore Ogonda ni mpenzi kindakindaki wa Kiswahili, mwandishi stadi wa vitabu na mwelekezi mahiri wa mashairi. Kwa mtazamo wake, safari ya kufikia kilelecha cha ufanisi inahitaji ari na bidii ili kuyashinda majabali na dhoruba.
Sinzore alilelewa katika kijiji cha Gidimo kilichoko Gisambai, eneobunge la Hamisi, Kaunti ya Vihiga. Ndiye wa pili kuzaliwa katika familia ya watoto wanne wa marehemu Bw Francis Ogonda Chabaya na marehemu Bi Florence Afandi.
Safari yake ya elimu ilianzia katika chekechea ya Gidimo-Bahai mnamo 1991 kabla ya kupitia katika Shule ya Msingi ya Gidimo (1992-1999) na Shule ya Upili ya Munzatsi, Hamisi (2000-2004).Alihiari kusomea taaluma ya ualimu (Kiswahili/Historia) katika Chuo Kikuu cha Egerton, Bewa la Laikipia (2006-2010), mwezi mmoja baada ya kutupa kozi ya Sayansi ya Mazingira aliyoitiwa kusomea chuoni humo.
Bw Sinzore ana shahada ya uzamili (M.A Kiswahili) kutoka Chuo Kikuu cha Maseno (2013-2019).Mbali na Bw Winston Matere, Bw Nganyi Likunda, Bi Joyce Agalo na Bw Oyasti Matata ambao walimpokeza malezi bora ya kiakademia, mwingine aliyechochea pakubwa kujitosa kwake katika ulingo wa ufundishaji ni aliyekuwa Mwalimu Mkuu wa Shule ya Upili ya Munzatsi, marehemu Bw Philip Sabwa.
Akiwa mwanafunzi wa Egerton, Sinzore alikutana na wahadhiri waliomtandikia zulia zuri la lugha na kumpigia mhuri wa kuwa mshairi shupavu na mwalimu mbobevu huku wakimtia motisha ya kupiga mbizi katika bahari ya utunzi wa vitabu.
Amefundisha Kiswahili katika Friends School Keveye
Miongoni mwao ni Prof Kithuka Musau, Prof Onyango Ogolla, Prof Peter Waweru, Prof Wendo Nabea, Dkt Sheila Wandera na marehemu Prof Aswani Buliba. Alifaulu vyema kwa kupata daraja ya juu (First Class) na akatuzwa kwa kuibuka mwanafunzi bora (Vice Chancellor’s Award).
Bw Sinzore amefundisha Kiswahili katika shule za upili mbalimbali zikiwemo: Ivola (2005-2006); Gahumbwa (2009), Migingo Girls (2009), Bukulunya (2010) na Dr Maurice Dang’ana (2010-2019). Alihamia Friends School Keveye Girls iliyoko Sabatia, Vihiga mnamo 2020.
Bw Sinzore amekuwa mtahini wa kitaifa wa Karatasi ya Kwanza ya Kiswahili (Insha) tangu 2011. Tajriba hiyo pevu anayojivunia imemwezesha kuzuru shule nyingi za humu nchini kwa nia ya kuhamasisha walimu na kuelekeza wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.
Mbali na ualimu, amechangia pia makala katika majarida tofauti ambayo yamechapishwa kimataifa. Isitoshe, ameshirikiana pia na walimu wengine kuandika vitabu mbalimbali vikiwemo: Mwongozo wa Mapambazuko ya Machweo, Jungu Kuu la Insha, Marudio Kabambe ya Bembea ya Maisha na Mapambazuko ya Machweo, Jungu Kuu la Mapambazuko ya Machweo na Bembea ya Maisha, A Pointer-History and Government na kadhalika.
Akiwa mwelekezi wa mashairi, amezoa tuzo mzomzo katika vitengo na kategoria anuwai za mashindano ya tamasha za kitaifa za muziki (KMF).
Anaamini kuwa muziki ni jukwaa muhimu la kuchipuza talanta, kuhimiza amani na kustawisha maendeleo nchini na duniani kote.
Zaidi ya wazazi wake wa kiroho Dkt Ronald Imbayi, Askofu Isaac Wawire na Askofu Thomas Muthee, Bw Sinzore anaistahi sana familia yake inayozidi kuiwekea taaluma yake mshabaha na thamani kubwa. Kwa pamoja na mkewe Bi Maureen Juma, wamejaliwa watoto watatu – Hephzibahope Hadasa, Beula Glory na Prosper Kibali.
Bi Maureen ni mwalimu wa Kiingereza na Fasihi katika Shule ya Upili ya Mudavadi–Madzuu Girls, Vihiga.