Habari njema kwa waliopoteza vyeti vya masomo kwa mafuriko
NA OSBORN MANYENGO
WAZIRI wa Elimu Ezekiel Machogu amesisitiza shule zitafunguliwa Jumatatu jinsi serikali ilivyotangaza huku akiahidi kwamba Baraza la Mitihani Nchini (Knec) litawapa nakala mpya wote ambao vyeti viliharibiwa na mafuriko.
Akihutubu Ijumaa mjini Kitale wakati wa hafla ya upanzi wa miti, waziri Machogu alisema kuna shule nyingi ambazo vitabu na vifaa vingine viliharibiwa na mvua, akitoa hakikisho serikali itashughulikia hilo na pia kujenga madarasa.
Shule zilizoharibiwa zaidi na mafuriko zimepewa wiki mbili zaidi ambapo inatarajiwa ukarabati utakuwa umekamilika.
Bw Machogu alitoa mwelekeo kuhusu ulipaji wa karo kwa shule za upili kwamba karo ya shule za kitaifa, zile za kimkoa na zile za kaunti ni Sh53,000, Sh53,000 na Sh45,000 mtawalia.
Alisema shule za kutwa masomo ni bure na kwamba serikali inalipia kila mwanafunzi Sh22,240 kwa mwaka.
Aliwatahadharisha wanasiasa kutofuata mambo yanayosambazwa mitandaoni kuhusu uajiri wa walimu kwamba eti kuna barua za kuajiri walimu zinazotolewa sehemu fulani ya nchi.
Alisema huo ni uongo mtupu, na kwamba serikali ikiajiri walimu itatangaza.
Alisema mambo na chakula shuleni, walimu wakuu hukubaliana na wazazi kuhusu mlo katika shule za kutwa.
Alisema ni wajibu mzazi kumnunulia mtoto wake sare ya shule.
“Wazazi wafahamu serikali inawalipia karo katika shule za kutwa hivyo nao kazi yao ni kuwanunulia watoto sare na ikiwa munakubaliana mambo ya chakula cha mchama shuleni, ada isiwe juu sana,” akasema Bw Machogu.
Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya ambaye aliandamana na waziri katika shughuli ya upanzi wa miti, ameitaka serikali kuu kuweka mkataba na serikali za kaunti ili Idara ya Misitu iwe chini ya serikali za kaunti.
Gavana Natembeya alisema idara ya misitu ikiwekwa chini ya serikali za kaunti, kila kaunti itahakikisha imelinda msitu ulio katika eneo lake.
“Misitu inaharibiwa na wale maafisa ambao wanatumwa kusimamia misitu ambao wanakosa kulinda miti maana hawaelewi umuhimu na faida ambazo wananchi wa eneo hilo hupata,” akasema gavana Natembeya.