• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Henry Chakava: Lenzi iliyowaweka soko Ngugi wa Thiong’o, Chinua Achebe katika Fasihi

Henry Chakava: Lenzi iliyowaweka soko Ngugi wa Thiong’o, Chinua Achebe katika Fasihi

KIFO cha mchapishaji vitabu Henry Chakava mnamo Ijumaa, kimefunga ukurasa wa mchapishaji wa kipekee, aliyejitosa kwenye sekta hiyo wakati ilikuwa vigumu kwa Waafrika kumiliki mashirika ya uchapishaji.

Kulingana na wasomi wa fasihi waliotangamana na Dkt Chakava, wanamtaja kama lenzi iliyowalea waandishi nguli kama Prof Ngugi wa Thiong’o, Meja Mwangi, Chinua Achebe, Cyprian Ekwensi, Grace Ogot, Marjorie Oludhe Macgoye, na Francis Imbuga.

“Kama isingekuwa ni ushujaa wake kununua shirika la uchapishaji vitabu la Heinemann kutoka kwa Waingereza, pengine ingekuwa vigumu baadhi ya waandishi kupenya katika ulingo wa fasihi na utunzi wa kazi za kubuni,” asema Bw Enock Matundura, ambaye ni mhadhiri, mwandishi wa vitabu na mfasiri.

Bw Matundura anasema kuwa Dkt Chakava alikuwa kama daraja lililowawezesha waandishi hao kujulikana Afrika Mashariki, Afrika na duniani kote.

“Katika miaka ya 1970, kulikuwa na wachapishaji wachache sana waliotaka kuchapisha kazi za waandishi wa Kiafrika. Wengi bado walikuwa na kasumba za kikoloni,” akasema Bw Matundura.

Alisema hali hiyo ilitokana na sababu kuwa, mfumo wa elimu uliokuwepo bado ulikuwa unaegemea masuala ya kikoloni.

Pia, mashirika machache ya uchapishaji yaliyokuwepo yalikuwa yakimilikiwa na wazungu.

Naye Dkt Barack Muluka anamtaja Dkt Chakava kama mtu wa kipekee aliyewapa sauti waandishi wa fasihi ya Kiafrika.

Anasema kuwa yeye ndiye alikuwa kimbilio la mwisho kwa waandishi hao, baada ya kazi zao kukakataliwa na mashirika ya uchapishaji yaliyomilikiwa na wakoloni.

“Ukisikia simulizi za waandishi kama Ngugi wa Thiong’o, alipitia hali ngumu alipokuwa akijaribu kuwasilisha mswada wa kitabu chake cha kwanza ‘Weep Not, Child’ (Usilie Mpenzi Wangu), kwa wachapishaji tofauti. Wengi waliona mswada huo kama ‘tishio’ kwa mfumo wa elimu nchini, ambao bado ulikuwa ukiegemea masuala ya kikoloni,” asema Dkt Muluka.

Wasomi wanasema ni jambo la kusikitisha kuwa licha ya mchango wake mkubwa katika sekta ya uchapishaji vitabu, Dkt Chakava hakuwahi kutambuliwa na serikali ambazo zimekuwepo tangu Kenya ilipojinyakulia uhuru.

Wanasema ingalikuwa vyema ikiwa tawala zilizopita zingalimtambua, kwa kumpa tuzo za utambuzi kama zile huwa wanapewa wanasiasa.

Sifa nyingine inayoelekezwa kwake ni jinsi alivyofaulu kuhimili mabadiliko mengi katika sekta hiyo, kwa mfano ujio wa teknolojia.

Wasomi wanasema kwamba mabadiliko ya kiteknolojia yameyafanya mashirika mengi ya uchapishaji kuvurugika, ingawa hali ilikuwa tofauti kwa shirika la East African Educational Publishers (EAEP), alilolimiliki marehemu.

“Mchango wa Dkt Chakava ni mkubwa sana. Hata kwenye ukongwe wake, bado alikuwa amekwamilia katika sekta ya uchapishaji, kutokana na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwenye ukuzaji wa sekta ya uchapishaji vitabu na elimu kwa jumla,” akasema Dkt Muluka.

  • Tags

You can share this post!

Waziri Murkomen, Kositany wanusurika katika ajali ya ndege

Chopa iliyombeba Murkomen ina historia ya hitilafu ikipaa

T L