Lugha, Fasihi na Elimu

JIFUNZE KISWAHILI: Je, sahihi ni ‘twendeni sote’ au ‘twende sote’?

Na ENOCK NYARIKI January 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAKALA mojawapo yaliyotoa mwito kwa wapenzi wa lugha ya Kiswahili kuhudhuria kongamano la Kiswahili Kisiwani Pemba (kongamano lenyewe limekwisha kufanyika) yalikuwa na mada ifuatayo: ‘Twendeni sote tuhudhurie…’.

Huenda ikawa vigumu kutambua kosa la sarufi linalojitokeza katika neno la kwanza la anwani mpaka uchunguze dhima ya {tw–} katika neno lenyewe.

Kabla ya kuingazia dhima hiyo kwa nia ya kulisahihisha kosa lililopo, itatujuzu kwanza tuangazie kazi ya kiambishi {e} kinachojitokeza katika neno hilo.

Neno ‘twendeni’ lilivyotumiwa katika anwani limeundwa kwa viambishi vinne vinavyotekeleza majukumu tofauti ya kisarufi. Kiambishi {tw–} ambacho kimsingi kingeendelezwa kama ‘tu’ kusingetokea badiliko la kifonolojia, ambalo nitalitaja baadaye, kinawakilisha nafsi ya kwanza wingi ilhali {–end–} ni mzizi.

Kiambishi {e} kinachotokea baada ya mzizi ni cha kutoa himizo au rai. Kitenzi ‘enda’ ambacho kimo katika kauli ya kutenda kimeundwa kwa mzizi na kiishio. Mzizi wenyewe ni {–end–} ilhali kiishio ni {a}.

Maadamu nimewahi kutaja katika safu hii kuwa ni kawaida kwa vitenzi vingi vya asili ya Kibantu kuishia kwa kiambishi {a}, si lengo langu kulisisitiza suala hilo katika makala haya.

Kabla ya kuongezewa viambishi vya nafsi, aghalabu vitenzi katika kauli ya kutenda vinapotumiwa katika sentensi huelekea kurejelea nafsi ya pili umoja.

Kwa hivyo, kiambishi {a} kinapogeuka na kuwa {e}, hiki cha pili hukusudiwa kutoa rai, himizo au hata kukubaliana na kitendo fulani.

Yaani, katika nafsi ya tatu tunasema ‘aende’; ‘uende’ (ya pili) na ‘niende’ (ya kwanza).

…MAKALA YATAENDELEA