Lugha, Fasihi na Elimu

Jinsi suala la haki na sheria limeshughulikiwa katika riwaya ‘Nguu za Jadi’ ya Clara Momanyi

Na JOYCE NEKESA, Kapsabet Boys High School December 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JUMA hili tutaendeleza suala la sheria na haki na kuangazia jinsi lilivyoshughulikiwa katika riwaya tukirejelea kifungu kifuatacho:

Siku iliyofuata, Mangwasha aliwasili kazini kama kawaida. Lakini alipigwa na butwaa alipoingia na kumkuta msichana ameketia kiti chake.

Alimtazama kwa muda. Msichana alimpa barua yake kisha akaendelea kuchapa kazi katika tarakilishi.

Mangwasha aliipokea akaenda katika chumba cha mapokezi. Huko aliketi na kuisoma.

Ilitoka kwa Chifu Mshabaha. Kwa kadri alivyoendelea kuisoma ndivyo alivyozidi kughafilika.

Alipomaliza, alihisi kukabwa koo na kitu asichokielewa. Kitu hicho kilipanda hadi kichwani.

Kilipofika huko, machozi ya moto yalianza kumtiririka njia mbili. Kinywa kilifumba, akashindwa hata kutamka neno.

Alitulia hapo kwa muda. Wafanyakazi wenziwe walimtazama kwa huruma.

(a) Bainisha mbinu za kimtindo zinazojitokeza katika kifungu hiki.

(i) Nahau – …alipigwa na butwaa…, …kuchapa kazi…, kukabwa koo…

(ii) Taharuki – Mangwasha anapomtazama msichana aliyeketia kiti chake kwa muda.

(iii) Chuku – …machozi ya moto yalianza kumtiririka njia mbili…

(iv) Tashihisi – Kitu kumkaba koo…

(b) Bainisha aina za taswira zinazojitokeza katika kifungu.

(i) Mwendo – …alipoingia …, akaenda katika…

(ii) Mguso – …alimpa barua, …kukabwa koo…

(iii) Hisi – …kughafilika…, walimtazama kwa huruma…

(iv) Oni – …walimtazama…

(c) Jadili suala la haki na sheria linavyoshughulikiwa katika riwaya.

Haki haitendeki katika kumpiga kalamu Mangwasha na Chifu Mshabaha baada ya kumtumikia kwa uaminifu.

Viongozi wanatumia mamlaka yao kuvunja sheria; Lesulia anawahakikishia vijana kuwa watakaokamatwa kwa kuvuruga uchaguzi watatoka korokoroni siku ya pili (Uk.128).

Sihaba anakamatwa kwa kuendeleza ufasiki ila anaachiliwa siku hiyo hiyo; haki haitendeki (Uk.85).

Sihaba anakamatwa kwa kusambaza vijikaratasi Matango ila hafikishwi mahakamani; haki haizingatiwi.

Lesulia anapendekeza kiti cha mgombea utemi kwa Chama cha Ushirika kiondolewe kinyume na sheria; Mwamba anatumia mahakama kuzima jaribio hilo.

Mashauri anashirikiana na Sagilu kufisidi vipusa na meno ya ndovu ila wanaposhtakiwa kortini mashtaka yanazimwa hata kabla ya kesi kuanza; haki haifanyiki (Uk.127).

Sheria inatumika kurejesha mali nyingi ya serikali iliyonyakuliwa na Nanzia.

Polisi wanawanasa wafuasi wengi wa Lesulia waliojaribu kutekeleza ulaghai wakati wa uchunguzi na hivyo haki kutendeka (Uk.175).

Umati unamkamata Cheiya kwa kujaribu kuua Lonare; anapelekwa kituo cha polisi na kufungiwa na hatimaye haki inatendeka.

Haki ilitendeka wakati hakimu alikata kauli kuwa serikali igharimike kuwajengea watu wa Matango nyumba zao upya baada ya ushahidi kuonyesha kwamba serikali ndiyo iliyohusika na kuteketeza makao ya Waketwa.