KCSE 2025: Namna ya kujibu swali kuhusu insha ya Kumbukumbu
LEO tuangalie mfano wa swali la insha ya kumbukumbu.
Wewe ni Mkuu wa Chama cha Uhifadhi wa Mazingira katika Shule ya Kumekucha.
Kumekuwa na visa vya wanafunzi kutojali uhifadhi wa mazingira hapo shuleni. Andika kumbukumbu za mkutano mlioandaa kujadili namna mbalimbali za kuhifadhi mazingira shuleni.
KICHWA:
Kiandikwe kwa herufi kubwa. Kitaje neno kumbukumbu. Kisiishie kwa kitone au nukta. Kichwa kionyeshe jina la kikundi, mahali, saa na tarehe ya mkutano huo: Mfano
KUMBUKUMBU ZA MKUTANO WA CHAMA CHA WALINDA MAZINGIRA SHULENI ULIOFANYIKA KATIKA AFISI YA CHAMA TAREHE 7/4/2025 SAA MBILI HADI SAA SITA
MAHUDHURIO:
Majina ya waliodhuhuria na vyeo vyao, jina la mwenyekiti litangulie, lifuatwe na la katibu halafu majina ya wanachama. Kwa mfano:
Wincate Kawira – Mwenyekiti
Alphonce Obara – Katibu
Sofia Mwendwa – Mwanachama
Clement Kipyegon – Mwanachama
Mercy Wambugu – Mwanachama
Benson Kanake – Mwanachama
Baada ya kuandika cheo, alama ya kitone isiwekwe. Cheo kianze kwa herufi kubwa. Majina ya wanachama waliokosa kwa udhuru yawe kama mawili. Mfano:
Waliokosa kwa udhuru
Tabitha Mwilu – Mwanachama
Sammy Wafula – Mwanachama
Neno kumbukumbu lifupishwe ili liwe Kumb. Kitone kiwekwe baada ya ufupisho huo. Koloni iwekwe kabla ya hoja kujadiliwa.
Zaidi ya hoja nane zijadiliwe kwa kina.
Kumb. 1/2025: Kufunguliwa kwa mkutano
Pasiwe na kitone baada ya kila hoja/kumbukumbu iliyoorodheshwa na kupigiwa mstari. Maudhui yafuate kisha mwisho kuwe na thibitisho kwa kuacha nafasi wazi ya mwenyekiti, tarehe, sahihi. Nafsi ya tatu itumiwe, kumbukumbu ni za jopo.
AJENDA:
Kufunguliwa kwa mkutano
Kusomwa na kuthibitisha kumbukumbu za mkutano uliotangulia.
Masuala yaliyoibuka kutokana na kumbukumbu hizo (maudhui 8 na zaidi).
Kufunguliwa kwa mkutano.
Kusomwa na kuthibitisha kumbukumbu za mkutano uliotangulia (hata kama hakukuwa na mkutano awali).
Kupanda miti.
Kuwatuza wanaolinda mazingira.
Kuunda vyama vya kulinda mazingira.
Kuwaadhibu wanaotatiza mazingira.
Kutotupa taka ovyoovyo.
Kuongeza idadi ya majalala.
Kuwa na siku maalumu ya kusherehekea mazingira.
Kufyeka nyasi karibu na mabweni.
THIBITISHO
Mwenyekiti _______tarehe_______sahihi_______
Katibu_______tarehe_______sahihi_______