KCSE: Haya hapa maswali ya udurusu kutokana na riwaya ‘Nguu za Jadi’
“Hivyo, alitaka kubadili hali hata kama ilimaanisha kukitia kichwa chake kinywani mwa simba.
(Alitaka kuliokoa jahazi lililokuwa likielekea mwambani kwa kasi). Lakini angeliweza vipi kupambana na utandu wa mahasidi hao?”(Uk. 51)
(a) Eleza mbinu za kimtindo zinazojitokeza katika dondoo.
Taswira – Lililokuwa likielekea mwambani.
Jazanda – Kukitia kichwa chake kinywani mwa simba.
Swali balagha – Lakini angeliweza vipi kupambana na utandu wa mahasidi hao?
Nahau – Kuliokoa jahazi.
(b) Eleza sababu za msemaji kutaka kufaulisha kauli iliyotiwa kwenye mabano.
Ufisadi uliokithiri katika nchi ya Matuo. Sagilu hakulipia kodi bidhaa alivyoagiza.
Ukabila na ubaguzi katika ajira – Waajiriwa katika ofisi ya Chifu na serikalini walikuwa Wakule.
Ukosefu wa ajira. Vijana wengi waliokuwa wamefuzu kutoka taasisi za elimu walikosa kazi.
Ukiritimba wa kiuchumi – Sagilu alimiliki nyenzo zote muhimu za kiuchumi.
Unyakuzi wa mali ya umma na ardhi ya Wanamatango – Nanzia alinyakua jengo la kipekee mjini Taria, Skyline Mall. (Uk. 157).
Mshahara mdogo na kufutwa kazi kwa wafanyikazi – Mshahara aliolipwa Mangwasha haukuhudumia familia yake kikamilifu na hatimaye kufutwa kazi bila huruma.
Uharibifu wa mazingira – Viongozi walichimba mchanga na kukata miti bila kujali.
Ukosefu wa elimu miongoni mwa vijana. Mangwasha aliwaona vijana wakizurura mtaani.
Kutelekeza watoto wa kiume walioingilia matumizi ya dawa za kulevya.
Kutumia watoto wa kike katika biashara ya ngono. Sihaba alimiliki danguro lililoitwa Red Beads Lodging aliko watumikiza wasichana wadogo.
Ulanguzi wa mihadarati na matumizi ya pombe haramu – Ngoswe alimiliki mtandao wa ulanguzi wa dawa za kulevya.
Ukware – Sagilu alijihusisha kimapenzi na Sihaba na wanawake wengine kama vile Nanzia licha ya kuwa na mkewe nyumbani.
Utekaji nyara – Lonare alitekwa nyara siku chache kabla ya uchaguzi ili asishindane na Mtemi Lesulia.
(c) Eleza umuhimu wa mrejelewa katika kuijenga riwaya hii.
Mrejelewa ni Lonare.
Ametumika kuendeleza maudhui mbalimbali kama vile utetezi wa haki za kibinadamu na uongozi bora.
Anaendeleza ploti kupitia matukio mbalimbali anayoyatekeleza kama vile kujihusisha na biashara ya usafiri na kugombea kiti cha utemi.
Anawatambulisha wahusika kama vile Sauni na Sagura.
Anajenga sifa za wahusika kama vile Mangwasha kuwa na msimamo thabiti.
Anatatua migogoro iliyokuwepo kabla ya kutwaa uongozi kwa kutoa msamaha na kuhimiza usawa.
Anaendeleza dhamira ya mwandishi ya kuwa uongozi bora huamuliwa na wananchi wenyewe.
Juma lijalo tutashughulikia vipengele muhimu katika utahini wa riwaya.
-Joyce Nekesa, Kapsabet Boys High School