• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 6:55 PM
Kinaya cha elimu ‘msawazishaji’ kupalilia umaskini

Kinaya cha elimu ‘msawazishaji’ kupalilia umaskini

NA MWANGI MUIRURI

NI msimu mwingine wa wazazi kuwapeleka watoto wao shuleni.

Huu ni msimu ambao umegeuka kuwa kiini cha mahangaiko makuu ambapo hata mifugo na mazao huuzwa kwa bei za kutupa ndipo karo ipatikane.

Pia wazazi hulazimika kuchukua mikopo, ambapo wanabaki wakilipia riba za juu katika hali inayodhihirisha wazi kwamba elimu, licha ya faida zake kwa jamii, ughali wake hapa nchini umeitia doa.

Elimu ambayo ilipigiwa upatu na waanzilishi wa taifa kama urithi wa kusawazisha watu maskini na matajiri imegeuka kuwa kiini cha umaskini mkuu katika familia nyingi.

Inadaiwa kwamba baadhi ya watu wenye ushawishi huwataka kimapenzi wake wa watu ndipo wawapige jeki na kuwasaidia kulipa karo ya wana wao.

“Tuko na shida kubwa katika taifa hili. Karo imekuwa ya kujaza njaa na mikopo katika familia nyingi huku sekta muhimu zilizokuwa zinawasaidia wazazi kupata karo zikikumbwa na ukosefu wa mapato,” akasema mwenyekiti wa kamati ya elimu katika bunge la Seneti Bw Joe Nyetu.

Nyutu ambaye ni Seneta wa Murang’a, aliambia Taifa Leo kwamba hata hazina za basari ambazo zilikuwa zinafaa kusaidia familia maskini zimevurugwa na watu wasio watakia wengi mazuri.

“Lau fedha ambazo hutengewa harakati za basari katika taifa hili zingetumika vyema, hakuna mwanafunzi hata wa tajiri angekuwa analipa karo. Kila kiongozi wa kuchaguliwa isipokuwa seneta, huwa ana kitita cha basari huku mashirika na kampuni pamoja na wahisani kutoka ng’ambo, wakijaza kibaba chetu cha basari. Inasikitisha kwamba wapo watoto ambao wanatatizika kujiunga na Kidato cha Kwanza,” akasema seneta Nyutu.

Aliyekuwa mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Wasichana ya Nginda Bi Wanjiku Gitu alisema kwamba mwanzoni mwa mwaka “ukiwa mwalimu mwenye utu hata unaweza ukapata msongo wa mawazo hadi uwe na kichaa ama uage dunia”.

“Wazazi hufika ofisini na kukupigia magoti huku wakikulilia kana kwamba wewe ni Mungu. Kilio chao ni ukubali watoto wao wajiunge na masomo nao warejee nyumbani wakatafute karo,” akasema Bi Gitu.

Alifichua kwamba baadhi ya wazazi hujitolea kukuachia vitambulisho vyao vya kitaifa kama mdhamini kwamba watatia bidii kusaka pesa ndipo walipe karo.

“Niliwahi kujionea baadhi ya wazazi wakiamua kukuachaia hatimiliki za vipande vya ardhi,” akaongeza.

Alisema kwamba picha mbaya zaidi ambazo zimekataa kumtoka kwa kichwa ni kuona watoto hao kutoka kwa familia za kipato cha chini wakiwa wamesimama hapo kando wakiwa hata hawana sare za shule na mahitaji mengine kama vile godoro huku wakishuhudia machozi na kupiga magoti kwa wazazi wao.

“Ni vyema viongozi waelewe kwamba hata Mungu hawezi akawabariki wakati picha hizo zinaendelea kujiweka wazi katika shule nyingi hapa nchini. Mzazi huwa ametelekezwa kwa kiwango kikuu na wanasiasa hao wenye uwezo wa kuwasaidia ila tu wanakataa,” akasema.

Bi Gitu alisema hakuna kilichokuwa kikimfedhehesha kama kuona mwanafuzi aliyekuwa ameitwa kujiunga na shule hiyo ya Nginda amekosa kufika kutokana na ukosefu wa karo.

“Ukifuatilia unaambiwa kwamba mtoto huyo alipelekwa kwa shule iliyo karibu na nyumbani kwao kutokana na ufukara wa wazazi. Sekta ya elimu haitakuwa na manufaa kwa taifa hili ikiwa itakuwa tu inaafikiwa na matajiri au waliouza mali yao na kukopa hadi kupigwa mnada kusudi watoto wao wasome,” akasema.

Katika sehemu nyingi za mashinani, watu wa kukopesha pesa huchipuka katika misimu ya watoto kujiunga na kidato cha kwanza, taasisi za elimu ya juu pamoja na vyuo vikuu.

“Utapata kwamba mikopo hiyo hutolewa kwa riba za zaidi ya asilimia 50 ya mikopo nao madalali wakijazana mashinani kununua mazao na mifugo kwa bei za kutupa huku wazazi wakihangaika kusaka wanunuzi kusudi karo ipatikane,” akasema aliyekuwa diwani wa Ichagaki Bw Charles Mwangi.

Aliyekuwa mbunge wa Maragua Bw Elias Mbau ambaye alihudumu pia kama mwenyekiti wa bodi ya hazina ya ustawishaji  maeneo bunge (NG-CDF) alisema kwamba “taifa hili lina rasilimali tosha za kulipia watoto wote karo lakini kikwazo tu ni ufisadi”.

Wazazi na walezi wakiwa na baadhi ya wanafunzi wa kujiunga na shule ya kitaifa ya wasichana ya Kenya High iliyoko Nairobi mnamo Januari 15, 2024. PICHA | BILLY OGADA

Alisema wanasiasa hukataa vitita vyote vya basari vijumlishwe kwa kapu moja na watoto wote wawe wanalipiwa karo “ili waendelee kushikilia kitita hicho kama silaha ya kisiasa”.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Agikuyu Bw Wachira Kiago alisema kwamba haelezi ni kwa nini wanasiasa husisitiza kupeana basari kupitia mikutano ya hadhara huku kukiwa na vyombo vya habari ili waangaziwe katika runinga na redio.

“Isitoshe, watoto walio katika maeneo ambayo hayakupiga kura kwa wanasiasa hao, huwa wanabaguliwa lakini wengine hata wa kutoka maeneo bunge ya mbali wakinufaika kupitia ufisadi,” akasema Bw Kiago.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mkutano wa mahakama na Rais utazaa haramu – Raila

Mackenzie kufunguliwa mashtaka ya mauaji

T L