Kiswahili kitumike bungeni mara kwa mara, si tu wakati ‘tunapochokozwa’ na jirani
KUNA kauli iliyotolewa na Seneta wa Nairobi Edwin Sifuna wiki hii ambayo inapiga darubini matumizi ya Kiswahili bungeni nchini Kenya.
Seneta Sifuna aliwarai maseneta watumie Kiswahili katika Bunge la Seneti ili wabunge wa Tanzania waweze kuwaelewa watakapojadili madai ya wananaharakati Wakenya kuteswa na kufurushwa kutoka nchi jirani ya Tanzania.
Hatua hii ilitokana na mjadala ulioendelezwa katika Bunge la Tanzania kuhusu suala hilo. Wabunge wa Tanzania walitumia Kiswahili kuwasilisha na kujadili hoja zao.
Lengo kuu la lugha ni kuwasiliana. Ujumbe unaweza kumfikia anayelengwa kwa lugha anayoielewa zaidi. Katika muktadha wa Jumuiya ya Afrika, lugha hiyo ni Kiswahili.
Ikumbukwe kuwa Kenya na Tanzania ni wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ambapo lugha ya mawasiliano mapana ni Kiswahili – Prof John Kobia
Hii ndiyo sababu Seneta Sifuna aliwahimiza wenzake watumie Kiswahili ili hoja zao ziweze kueleweka ipasavyo.
Ni muhimu wabunge wa Kenya watumie Kiswahili katika shughuli za bunge mara kwa mara isiwe tu ‘wanapochokozwa’ na jirani.
Wabunge wa Kenya wanaweza kujifunza kutoka kwa wenzao wa Tanzania kuhusu matumizi ya Kiswahili bungeni. Wabunge wa Tanzania wanaionea fahari lugha ya Kiswahili na kuitumia bungeni kwa umahiri mkubwa.
Ni wabunge wachache mno nchini Kenya hutumia Kiswahili bungeni. Kanuni za kudumu za Bunge la Kenya zinatambua Kiswahili kuwa mojawapo ya lugha za kutumiwa bungeni.
Wabunge wana nafasi ya kukuza na kuendeleza Kiswahili kwa kutumia lugha hii mara kwa mara ili wananchi waweze kuwaelewa barabara.
Kauli ya Seneta Sifuna inaashiria kwamba lugha ya Kiswahili ni nyenzo muhimu ya kueleza, kupambanua na kusambaza habari muhimu zenye umuhimu wa kitaifa na kimataifa.