• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Machogu: Wanafunzi waliofika shuleni walindwe na wakuu

Machogu: Wanafunzi waliofika shuleni walindwe na wakuu

NA CHARLES WASONGA

MUDA mfupi baada ya Rais William Ruto kuamuru kuahirishwa kwa ufunguzi wa shule tena, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu amewaagiza walimu wakuu kutowaagiza kurejea nyumbani wanafunzi ambao tayari walikuwa wamefika shuleni ili kulinda usalama wao.

Alisema shule ziwaruhusu wanafunzi kurejea nyumbani tu ikiwa zitakuwa na uhakika kwa watafika makwao salama.

“Wasimamizi wa shule wawaruhusi wanafunzi wasalie shule ikiwa walikuwa wamewasili ili kuhakikisha usalama wao isipokuwa katika hali ambapo watakuwa na uhakika kuwa watakuwa salama wakirejea nyumbani,” Bw Machogu akasema kwenye taarifa fupi Ijumaa.

Baadhi ya wanafunzi wanaosomea shule za mabweni, waliripoti shuleni Jumatatu asubuhi saa chache tu baada ya waziri huyo kutoa taarifa ya kuahirishwa kwa tarehe ya kufunguliwa kwa shule hadi Mei 6, 2024.

Bw Machogu alitoa taarifa hiyo majira ya saa saba za usiku wa kuamkia Jumatatu, akisema serikali ilikuwa imechukua hatua hiyo kutokana na mvua kubwa inayoshuhudiwa kote nchini.

Lakini katika hotuba yake kwa taifa mnamo Ijumaa, Rais Ruto aliagiza Wizara ya Elimu kuahirisha tena tarehe ya kufunguliwa kwa shule kwa muda usiojulikana.

Kiongozi wa taifa alisema serikali ilichukua hatua hiyo baada ya kupokea ripoti kutoka kwa Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa kwamba janga la mafuriko linatarajiwa kuwa baya zaidi siku zijazo.

Hii ni kutokana na kimbunga kwa jina Hidaya kutoka Comoros ambacho kinatarajiwa kupiga sehemu kubwa ya nchi ikiandamana na upepo mkali na mvua nyingi.

“Mvua itaendelea kunyesha kwa wingi na kwa kipindi kirefu katika mwezi huu na hata baadaye. Aidha, huenda Kenya ikakumbwa na kimbunga cha kwanza ambacho kitagonga wakati wowote kuanzia tarehe tano mwezi huu,” Rais akasema.

Bw Machogu pia alizitaka Bodi za Elimu katika Kaunti kuandaa mikutano ya dharura kutathmini hali katika maeneo yao na kuwasilisha ripoti katika afisi yake kufikia Mei 10.

Aidha, alitoa wito kwa bodi za usimamizi wa shule za msingi na za upili za umma kuwasilisha ripoti kuhusu kiwango cha uharibifu wa miundo msingi katika shule zao kutoka na janga hilo la mafuriko.

Aidha, alitaka bodi hizo kupendekeza hatua za kuzuia au kurekebisha athari hizo na kuwasilisha ripoti kwa afisi za elimu katika ngazi za kaunti ndogo kufikia Mei 8, 2024.

“Ripoti hizo ni muhimu katika kushirikisha Hazina za Maendeleo katika Maeneo Bunge (CDF) katika mpango wa ukarabati wa miundo msingi iliyoharibiwa,” Machogu akaeleza.

Aliwashauri Maafisa wa Elimu Nyanjani wanaohudumu katika maeneo ambako shule zinatumika kama hifadhi za watu waliopoteza makazi yao kutokana na mafuriko, kushirikiana na maafisa wa utawala wa kitaifa (NGAO) kutambua maeneo mbadala ya kuwapa hifadhi watu hao.

“Hii itahakikisha kuwa shule hizi zinakuwa tayari kwa shughuli za masomo baada ya changamoto ya mafuriko kupungua,” akaeleza.

Idara ya Hali ya Hewa inakadiria kuwa mvua itaendelea kunyesha kwa wingi sehemu mbalimbali nchini, huku maeneo ya nyanda za chini yakishuhudia mafuriko.

Ni janga hili la mafuriko ambalo limeharibu miundomsingi shuleni yakiwemo madarasa, mabweni, vyoo na ua.

Mnamo Ijumaa, Rais Ruto aliagiza Wizara ya Elimu kushirikiana na hazina za NG-CDF katika ufadhili wa mipango ya kurekebisha miundomsingi ya shule iliyoharibiwa na mvua.

  • Tags

You can share this post!

Arsenal yanyemelea Joshua Zirkzee anayesemekana kumzidi...

Mafuriko: Daraja la Oldonyo Sabuk halipitiki

T L