• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Mafuriko: Mgawanyiko wa kitabaka shule za kibinafsi zikiendelea na masomo kidijitali

Mafuriko: Mgawanyiko wa kitabaka shule za kibinafsi zikiendelea na masomo kidijitali

NA DAVID MUCHUNGUH

HATUA ya kuahirisha ufunguzi wa shule hadi tarehe isiyojulikana imeibua mgawanyiko wa kitabaka huku watoto kutoka familia maskini, wengi wao wanaosomea shule za umma, wakiendelea bila masomo wenzao kutoka familia tajiri wakisoma kidijitali.

Shule za umma zimeathirika zaidi licha ya serikali kutumia zaidi ya Sh32 bilioni kuzinunulia tableti, vipakatalishi, projekta, vifaa vya kusambaza intaneti na kuzisambazia stima.

Mafunzo

Maelfu ya walimu vilevile wamepokea mafunzo kuhusu matumizi ya vifaa hivyo vya kuwezesha kusomesha kielktroniki.

Hata hivyo, baadhi ya shule za umma za sekondari zimeanzisha madarasa ya kidijitali kwa wanafunzi wao.

Haijabainika ni lini shule zitafunguliwa ingawa taarifa inasubiriwa baada ya bodi za kaunti zinazohusu elimu kuwasilisha ripoti kuhusu hali ilivyo kwa Wizara ya Elimu mnamo Ijumaa, Mei 10, 2024.

Bodi zote za usimamizi zinapaswa kuwasilisha ripoti kuhusu hali ilivyo katika shule zao kufikia hii leo.

Taifa Leo imebaini kuwa shule kadhaa za kibinafsi zimekaidi agizo la serikali kuhusu kutofungua shule kutokana na masuala ya kiusalama yanayosababishwa na mvua kubwa na mafuriko katika maeneo mengi nchini.

Mabasi ya shule yameonekana yakiwachukua na kuwarejesha watoto asubuhi na jioni.

Wanafunzi katika shule zinazotumia mtaala tofauti na zisizofuata kalenda ya mtaala wa kitaifa vilevile wameendelea na madarasa yao huku utata ukiibuka kuhusu iwapo agizo hilo lililenga shule za umma pekee.

Hatua hiyo ya kuahirisha ufunguzi wa shule hadi tarehe isiyojulikana ilitangazwa na Rais William Ruto mnamo Jumatatu.

“Kutokana na mafunzo tuliyopata kufuatia janga la Covid-19, tuliamua kuwashughulisha watoto wetu na tukawafahamisha wazazi. Wazazi wengi wana simu za kisasa au kifaa cha kidijitali ambacho watoto wao wanaweza kutumia kusoma. Idadi ya wanaojitokeza ni karibu asilimia 80. Walimu wako tayari kusomesha bila malipo ya ziada kwa sababu watakuwepo shuleni,” alisema Mwalimu Mkuu kutoka Kaunti ya Nakuru akiomba jina lake libanwe.

Masomo vilevile yanaendelea katika shule zilizofunguliwa kabla ya uahirishaji wa kwanza wa ufunguzi uliotangazwa na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu Aprili 29, 2024.

“Kwa wanafunzi ambao tayari walikuwa wamefika shuleni, usimamizi wa shule utawahifadhi na kuhakikisha usalama wao isipokuwa pale tu hali inaruhusu warejeshwe salama makwao,” alisema Bw Machogu kupitia taarifa iliyotumwa Alhamisi wiki iliyopita.

Wasiwasi

Wazazi waliohojiwa na Taifa Leo walielezea wasiwasi kuhusu utata unaozingira ufunguzi wa shule.

Akizungumza na Taifa Leo, Bw Machogu alisema tarehe za muhula mpya zitarekebishwa ili kufidia muda uliopotezwa.

“Ninahofia kuwa shile zinakawia kufunguliwa. Binti yangu yuko katika Kidato cha Tatu na muda mrefu bila kufanya chochoe unamaanisha ana muda mwingi wa kutangamana na wanarika wenzake na wavulana. Mimba na matumizi ya mihadarati ni hofu halisi wakati huu. Isitoshe, bila tarehe mahsusi za ufunguzi, ni vigumu kupanga iwapo niamwanzishie masomo ya ziada au kama wazazi tuagize shule kuanzisha madarasa ya kidijitali,” anasema mzazi kutoka jijini Nairobi, Phillys Nyambura.

  • Tags

You can share this post!

Kagwe Mungai: Wanaoponda mahusiano yangu ya kimapenzi, kazi...

Sauti ya mnyonge kila kona

T L