• Nairobi
  • Last Updated June 15th, 2024 1:54 PM
Maswali ya KCSE kuhusu mada ya ‘Ngeli za Nomino’

Maswali ya KCSE kuhusu mada ya ‘Ngeli za Nomino’

NGELI ni kundi la nomino za Kiswahili ambalo huchukua viambishi sawa katika upatanisho wa kisarufi.

Maswali kuhusiana na ngeli hujitokeza kwa njia mbalimbali. Kwa mfano, mtahiniwa anaweza kuhitajika kutambua ngeli za nomino kama ilivyokuwa katika mitihani ya 2011, 2014, 2018, 2019, 2022 na 2023.

Swali (f) katika mtihani wa 2011 lilimtaka mtahiniwa kubainisha ngeli ya nomino ‘furaha’ ilhali swali (q) katika mtihani wa 2014 lilimhitaji mwanafunzi kubainisha ngeli ya nomino ‘furaha’ na ‘nyasi’. Nomino ‘furaha’ iko katika ngeli ya I-I ilhali ‘nyasi’ iko katika ngeli ya U-ZI.

Katika mtihani wa 2018 swali (e) mtahiniwa aliulizwa kutaja ngeli za nomino ‘ugwe’ na ‘limau’ na katika swali (i) la mtihani wa 2019, mtahiniwa akaulizwa kutaja ngeli za ‘sukari’ na ‘teo’.

Ngeli ya ‘ugwe’ ni U-ZI nalo neno ‘limau’ liko katika ngeli ya LI-YA. Majibu yaliyotarajiwa kwa swali la mtihani wa 2019 ni I-I (ngeli ya sukari) na U-ZI (ngeli ya uteo).

Vilevile, mtihani wa 2022 ulikuwa na swali la kubainisha ngeli ambapo watahiniwa walihitaji kubainisha ngeli ya nomino: ‘bendera’ na ‘ujana’ [swali (p)]. Mtahiniwa alitarajiwa kutaja kuwa neno ‘bendera’ limo katika ngeli ya I-ZI ilhali neno ‘ujana’ limo katika ngeli ya U-U, pia watahiniwa walioainisha ngeli U kwa nomino ‘ujana’ walituzwa.

Hatimaye, swali (r) la mtihani wa 2023 lilimtaka mtahiniwa kutaja ngeli ya nomino ‘bidii’, jibu lililotaraiwa ni I-I. Watahiniwa waliotaja ngeli ya I-ZI pia walituzwa.

Aidha, mtahiniwa anaweza kuhitajika kutunga sentensi kudhihirisha matumizi ya ngeli fulani. Swali la aina hii hutathmini uwezo wa mwanafunzi kuzingatia upatanisho wa kisarufi wa ngeli husika.

Kwa mfano, 2006 swali (a) na 2016 swali (a) yalimtaka mwanafunzi kutunga sentensi kutumia nomino katika ngeli ya I–I. Maneno kama ‘furaha’, ‘sukari’, ‘chumvi’, ‘mvua’, ‘pombe’ na ‘chai’ yako katika ngeli hii. Mfano wa jibu kwa hivyo ni: ‘Chai ilimwagika sakafuni.’
Vilevile katika swali (i) la mtihani wa 2010, mtahiniwa aliulizwa kutunga sentensi kudhihirisha matumizi ya ngeli ya U-U. Nomino kama ‘ujana’, ‘ujinga’, ‘upole’, ‘werevu’ zingetumika kutungia sentensi.

Swali kuhsiana na ngeli linapomtaka mtahiniwa kutambua viambishi vya ngeli vya nomino fulani, mtahiniwa hutarajiwa kutaja viambishi vya ngeli na wala si mianzio au miundo mbalimbali ya maneno.

Kwa mfano: Andika viwakilishi ngeli vya nomino zituatazo: ‘Chakula’ na ‘kwetu’ [2007 Swali (m)]. Majibu yaliyotarajiwa ni KI-VI na PA-KU-MU mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

Washukiwa watatu wa wizi wauawa Industrial Area

Stanbic yashirikiana na Orion kuboresha mifumo ya huduma za...

T L