Mchapishaji vitabu maarufu, Henry Chakava aaga dunia
NA WANDERI KAMAU
MCHAPISHAJI maarufu wa vitabu nchini kwa muda mrefu, Dkt Henry Chakava, ameaga dunia.
Dkt Chakava,77, ambaye hadi kifo chake alikuwa mwanzilishi na Mwenyekiti wa shirika la uchapishaji vitabu la East African Educational Publishers Limited (EAEPL), alifariki Ijumaa alfajiri, alipokuwa akipokea matibabu katika Nairobi Hospital.
Hilo ni kulingana na taarifa zilizotolewa Ijumaa na Mkurugenzi Mkuu na Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw Kiarie Kamau.
“Dkt Chakava atakumbukwa kama ‘baba wa uchapishaji vitabu’ barani Afrika. Alisimamia mchakato wa ununuzi wa kampuni ya uchapishaji vitabu kutoka Uingereza–Heinemann (East Africa)—na kuibadilisha jina kuwa East African Educational Publishers,” akasema Bw Kamau.
Anafisiwa kwa kuchapisha kazi za waandishi maarufu barani Afrika kama Ngugi wa Thiong’o, Grace Ogot, Francis Imbuga, John Kiriamiti, Meja Mwangi, Marjorie Oludhe Macgoye (wote kutoka Kenya), Chinua Achebe, Cyprian Ekwensi kati ya wengine wengi.
Marehemu alizaliwa Aprili 26, 1946 katika eneo la Vokoli, Kaunti ya Vihiga (wakati huo ikiwa wilaya).