Lugha, Fasihi na Elimu

Mhadhiri afichua jinsi Kiswahili kinavyomvunia noti nchini Amerika

April 22nd, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA PETER CHANGTOEK

PROFESA David Kyeu ni mwandishi aliyebobea katika Kiswahili na Kiingereza, lugha ambazo zina umuhimu mkubwa katika fani za elimu na mawasiliano kwa ujumla.

Aidha, yeye ni mtafiti, na ni mhadhiri ambaye amewahi kufunza katika vyuo vikuu mbalimbali, hususan ughaibuni.

Alizaliwa katika eneo la Thika, ambapo wazazi wake walikuwa wakifanya kazi katika kampuni ya mananasi ya Del Monte.

Alisomea Shahada ya Elimu (Kiswahili na Hisabati) katika Chuo Kikuu cha Egerton, 2004, na Shahada ya Uzamili ya Kiswahili, 2007, kutoka chuo chicho hicho.

“Huku shahada yangu ya digrii ikinitayarisha kufunza katika shule za upili, nilipata masomo zaidi ili nifunze katika vyuo vikuu,” asema Prof Kyeu.

Kabla hajaenda Amerika, alihudumu katika shirika la Care International, lililoko katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab.

Baadaye, alipata ufadhili wa masomo, unaojulikana kama Fulbright Scholarship, na kufunza Kiswahili kwa muda wa mwaka mmoja, katika Chuo Kikuu cha Brown.

“Baada ya kulipa mkopo wa elimu ya juu (Helb), nilirejea kusomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin Madison, na kufuzu mwaka 2014,” aeleza.

Profesa David Kyeu aonyesha baadhi ya vitabu alivyoviandika kwenye hii picha akiwa katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley, Amerika. PICHA | HISANI

Kwa sasa, Prof Kyeu anafunza katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley.

“Nimefunza pia katika vyuo vikuu vya Florida, Gainesville, na Touro,” afichua.

Anasema kwamba, ufunzaji nchini Amerika una tofauti ikilinganishwa na Kenya. Kuna tofauti za mifumo ya elimu, mbinu za kufunza, rasilimali madarasani, idadi ya wanafunzi madarasani miktadha ya tamaduni, na nchi zote mbili zina changamoto mbalimbali.

Mbali na kufunza, Prof Kyeu ameviandika vitabu kadhaa vya Kiswahili na Kiingereza. Pia, ameachangia makala katika majarida tofauti tofauti.

Alikichapisha kitabu chake cha kwanza kinachojulikana kama Kibali mwaka 2010, katika matbaa ya Outskirts Publishing Press, Amerika. Isitoshe, ameyaandika majarida kadhaa kwa Kiswahili na Kiingereza. Aidha, amechangia na kuhariri majarida kadha wa kadha, kwa lugha za Kiswahili na Kiingereza.

Miongoni mwa vitabu alivyoviandika ni pamoja na Beginning Swahili Workbook and GuideHomework Exercises, Quizzes, Final Exam and Noun Classes, kilichochapishwa na matbaa ya Outskirts Publishing Press, Colorado, Amerika mwaka 2012.

Kyeu, pia, ni mhariri wa kitabu kinachouzwa katika Amazon, kilichoandikwa na wanawe wawili, kilichochapishwa Desemba 2023, kinachojulikana kama Two Years Abroad: American Kids’ Adventures in Kenya. Kitabu hicho kina hadithi 13, zilizoandikwa na David Kyeu Jr na Sally K Wambua, baada ya kuzuru Kenya kwa muda wa miaka miwili, kuanzia 2019-2021. Kitabu hicho kilichapishwa na Native Book Publishers.

“Kwa muda huo mrefu, hawakuishi tu Kenya, bali pia walijishughulisha na utamaduni na elimu ya nchi,” aeleza Kyeu, ambaye ni baba wa watoto watatu.

Katika mwaka 2021, Prof Kyeu, pamoja na I. Lupogo, K. Mataka, na M. Mtabazi waliandika Asili, Matumizi, na Mtazamo wa Salamu ya ‘Shikamoo’ katika Jamii ya Watumiaji wa Kiswahili (The Origin, Use, and Perspectives of the Greeting ‘Shikamoo’ among Speakers of Swahili) – katika jarida la MULIKA linalomilikiwa na Taasisi ya Utafiti wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Institute of Kiswahili Research, University of Dar es Salaam).

Aidha, Prof Kyeu ni mmoja wa wahariri wa jarida la MULIKA 2017, Toleo Maalum, Makala ya Kongamano la CHAUKIDU 2016 – Institute of Swahili Research, Dar es Salaam.

Pia, yeye ni mwandishi wa ‘Kuwakosoa Wanafunzi Kimawasiliano (Correcting Students Communicatively) – jarida la The Journal of African Languages Teachers Association (JALTA) Language Specific Swahili.

Katika waka 2014, Kyeu alichapisha The Impact of Facebook Chat on Swahili Essay Writing – Current Studies in Comparative Education, Science, and Technology – Volume 1, Ukurasa 34-64.

Aidha, aliandika Technology and Swahili Essay Writing – Russian-American Education Forum: An Online Journal, Volume 6.

Katika mwaka 2012, alichapisha Ubisharazishwaji wa Utahini wa Kiswahili: Mfano wa TOKFL – Journal of African Languages Teachers Association (JALTA) Language Specific Swahili, Volume 1.

Mwaka huo wa 2012, alichapisha kitabu kinachojulikana kama Beginning Swahili Workbook and Guide kilichochapishwa na Outskirts Publishing Press, Colorado, Amerika.

2011, alikichapisha kitabu kinachojulikana kwa jina Swahili Noun Classes: Your Friendly Workbook and Guide ambacho kilichapishwa na Outskirts Publishing Press, Colorado, Amerika.

“Kiswahili huchukuliwa sana kwa makini na wanafunzi nchini Amerika, hasa wanafunzi wanaotaka kufanya utafiti wao katika nchi ambako Kiswahili huzungumzwa, katika Jumuiya ya Afrika Mashariki,” asema.

Anaongeza kuwa baadhi ya wanafunzi hutimiza masharti ya kusomea Kiswahili kwa mwaka mmoja, katika vyuo vikuu.

Anasema kuwa, Kiswahili kina uwezo wa kuzungumwa barani Afrika, huku watumiaji Kiswahili wakitoka Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Malawi, visiwa vya Comoro, Sudan Kusini, Ethiopia, Somalia, Oman, na Yemen.

Aidha, Prof Kyeu anafichua kuwa, Kiswahili hufunzwa katika Chuo Kikuu cha Ghana, kufuatia mkataba baina ya aliyekuwa rais, Kwame Nkrumah na Mwalimu Julius Nyerere, miaka ya sitini.

“Mbali na kuwa lugha ya taifa, Kiswahili ni lugha rasmi katika nchi za Kenya na Tanzania,” adokeza.