Msichana aitwa kujiunga na shule ya kitaifa ya wavulana
NA KASSIM ADINASI
HAMU ya kutaka kufaulu maishani na kuinyanyua familia yake kutoka kwa lindi la umaskini ilimfanya msichana Gloria Adhiambo kujitahidi masomoni ambapo alipata alama 389 kwenye Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE 2023).
Lakini Gloria ambaye alisomea katika Shule ya Msingi ya Nyalgunga iliyoko Alego Kaskazini katika Kaunti ya Siaya alishangaa alipopata barua ya mwaliko kujiunga na shule ya kitaifa ya wavulana ya Lenana jijini Nairobi.
Taifa Leo ilifika nyumbani kwa kina huyo msichana wa umri wa miaka 14 na ikajionea namna ambavyo wanapitia katika hali ngumu.
Mamake alikuwa ameanika mahindi machache kwenye vigunzi huku mengine yakiwa maguguta tupu, ishara kwamba hawakupata mavuno mazuri.
Kile ambacho hawaelewi, ni kwamba ilitokeaje akaitwa Lenana wakati ambapo alikuwa amechagua shule za wasichana ambazo ni Alliance Girls, Kisumu Girls, Rang’ala Girls miongoni mwa nyingine.
“Sikujua kwamba shule hiyo ni ya wavulana,” akasema Gloria ambaye sasa hofu yake ni huenda akakosa kujiunga na shule ya kitaifa.
Hata anasema hitilafu hiyo imefanya akose kupata fursa za ufadhili wa elimu.
Msichana huyo alikuwa amejiwekea shabaha ya kupata alama 400 lakini aliridhika na alama 389 alizopata.
Mamake, Bi Margaret Awuor ana wasiwasi mkubwa.
“Binti yangu alifanya kila awezalo kujiunga na shule ya kitaifa lakini sasa huenda hata akakosa nafasi katika shule ya upili,” akasema Bi Awuor.
Mzazi huyo alisema walimuambia mwalimu mkuu wa Nyalgunga aliyeahidi kuwasaidia ili kuona tatizo hilo linarekebishwa.
Mkurugenzi wa Elimu katika Kaunti ya Siaya Bw Mbugua Kabaki alisema hitilafu hiyo itarekebishwa.
“Hiyo ni hitilafu ndogo ambayo itarekebishwa,” akasema Bw Kabaki kwa simu.