Lugha, Fasihi na Elimu

Msururu wa maswali miigo ya KCSE katika riwaya ya ‘Nguu za Jadi’

Na JOYCE NEKESA September 25th, 2024 2 min read

JUMA hili tutaangazia baadhi ya maswali kutokana na riwaya ya ‘Nguu za Jadi’.

“Aah, si mnajua wale watu ni hatari. Lakini hawatakuwa na nguvu. Njia zao zote nitazifunga.”

(a) Eleza muktadha wa dondoo hili.

Msemaji – Ngoswe

Wasemewa – Mashauri na Lombo

Mahali – Njiani wakitoka hospitalini kumjulia Lonare hali

Kiini – Ni baada ya Lonare kumshauri Ngoswe aachane na ulanguzi wa dawa za kulevya.

(b) Tambua toni ya dondoo hili.

Toni ya kutahadharisha/ kuonya.

(c) Thibitisha namna watu wanaorejelewa walivyokuwa hatari.

Waliwachomea Waketwa makao yao.

Walihusika katika utekaji nyara. Lonare alitekwa nyara.

Waketwa walitishwa ili wahame eneo lao la Matango.

Waliyachafua mazingira kwa kukata miti ovyo kwenye vyanzo vya maji na hivyo kusababisha ukame ulioleta njaa. (Uk. 45).

Mashimo yaliyoachwa bila kuzibwa baada ya kuchimbwa kwa mchanga yalikuwa hatari kwa usalama wa wananchi. (Uk. 46).

Mazingira mabovu Majaani na ukosefu wa usalamu kwa sababu ya kutowajibika kwao.

Waketwa kubaguliwa katika sekta ya ajira.

Wakule kuajiriwa kazi wasizohitimu kama vile kuwa madaktari na marubani hivyo kusababisha maafa mengi.

Unyakuzi wa ardhi pale ambapo mkurugenzi wa ardhi anashirikiana na Mtemi Lesulia kuwanyang’anya Waketwa ardhi yao.

Utabaka ambapo matajiri ndio wenye nchi na maskini kuwa wana wa nchi.

Kuhatarisha maisha ya watoto kwa kuuza maziwa yaliyohifadhiwa kwa sumu. (Uk. 17).

Ulanguzi wa dawa za kulevya ulioathiri vijana.

Umiliki wa madanguro na biashara ya ukahaba ulichangia ufuska.

Ukiukaji wa haki za watoto – Watoto walitelekezwa na wasichana kushirikishwa katika ukahaba.

Tamaa ya uongozi – Mtemi Lesulia yuko tayari kuwadhulumu na hata kuwaua wapinzani wake kwa sababu ya tamaa ya uongozi.

Udanganyifu – Mwanasheria Mafamba anadanganya mahakama kuhusu ujenzi wa soko katika eneo la Matango.

Unyakuzi wa mali ya umma. Majengo makuu mjini Taria yalimilikiwa na Nanzia na Wakule wengine.

Mauaji – Sagilu aliwaua washindani wake wa kibiashara.

Kuvunja ndoa za watu. Sagilu alilenga kuharibu ndoa ya Mangwasha na Mrima.

(d) Jadili namna ambavyo msemaji alikusudia kuzifunga njia za warejelewa.

Msemaji ni Ngoswe.

Warejelewa ni Wakule wakiongozwa na Mtemi Lesulia pamoja na wendani wake wa karibu.

Alikusudia kufichua siri za babake, Mtemi Lesulia.

Kumfanyia Lonare kampeni.

Kushirikiana na Lombo na Mashauri kupinga utawala dhalimu.

Kuacha biashara ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Kumuasi babake kama vile alivyoagiza yeye pamoja na vijana wenzake wavuruge uchaguzi. Ngoswe alikiuka agizo hilo.

Kumkosoa Sagilu alipotaka amuombee msamaha kwa Mashauri baada ya kumla kivuli. Alimkosoa kwa kitendo hicho.

Alishiriki katika kumkamata Sihaba.

Tanbihi: Jadili mikakati waliyotumia watetezi wa haki katika kukabiliana na hali yao ya maisha.