MTIHANI WA KCSE: Namna ya kukabili maswali yanayohusu ufahamu, ufupisho
HATUA ya kwanza katika kukabiliana na swali la Ufahamu ni kusoma kifungu hadi kikuelee na uyajue masuala yanayoangaziwa na kifungu hicho.
Baada ya kukisoma, yasome maswali ya Ufahamu ili utambue masuala yanayoulizwa. Hatua ya tatu ni kurejelea kifungu ukipigia mstari sehemu za kifungu zinazoweza kukusaidia kujibu maswali yaliyoulizwa.
Baada ya kupigia mstari sehemu teule za kifungu, andika nambari ya swali juu ya sehemu hizo ulizopigia mstari ili iwe rahisi kubainisha sehemu inayohitajika kujibu kila swali. Majibu yote yatoke kwenye kifungu. Usiandike masuala yasiyopatikana kwenye kifungu au kurudia kulinakili swali unapotoa jibu.
Unapojibu maswali, makinikia swali ili utambue kama ni swali wazi au funge, mfano wa swali funge ni: Matumizi ya simu bila tahadhari yana athari kwa mtumiaji.
Thibitisha kwa hoja tano kutoka kwenye kifungu [KCSE 2013 swali a]. Swali hili lilimuelekeza mtahiniwa kutoa hoja tano. Swali wazi kwa upande wake halidhihirishi idadi ya hoja unazopaswa kutoa.
Ili kujua idadi ya hoja za kuandika, zingatia alama za swali, kwa mfano ikiwa ni alama sita, basi toa hoja sita.
Unapoeleza maana ya msamiati, unaweza kutoa kisawe au maelezo kwa ufupi. Zingatia matumizi ya neno husika katika muktadha wake kwenye kifungu.
Ikiwa umeulizwa kueleza maana ya semi au methali, unaweza pia kuandika semi au methali sawa au maelezo k wa ufupi.
Akifisha majibu yako ipasavyo. Iwapo unahitajika kutoa zaidi ya hoja moja, ziorodheshe kwa kutumia nambari za Kirumi na usitumie vistari, vishale au vinyota. Iwapo jawabu ni sentensi, basi ianze kwa herufi kubwa na uimalize kwa kitone.
Unapowasilisha majibu, epuka makosa ya hijai na sarufi.
Kuhusu swali la Ufupisho, soma kifungu kwa makini ili kikuelee. Soma maswali ya Ufupisho na utambue iwapo unahitaji kujikita katika aya kadhaa au kifungu kizima.
Dondoa hoja muhimu katika kifungu ulichoulizwa na uziorodheshe kwenye sehemu ya matayarisho. Idadi ya hoja katika sehemu ya utakazoorodhesha ilingane na alama ulizopewa.
Unganisha hoja zako kwenye sehemu iyo hiyo ya matayarisho huku ukizingatia idadi ya maneno uliyopewa. Hakikisha kuwa umenakili hoja zote muhimu.
Iwapo idadi ya maneno uliyotumia imezidi maneno uliyoulizwa kutumia, ondoa tamathali za semi, vivumishi, vielezi, mifano, orodha ya vitu na maelezo.
Hamisha jibu lako la aya moja tu kwenye sehemu ya jibu na usiweke anwani. Usikate hoja zako. Andika idadi ya maneno uliyotumia katika mabano.
Iwapo umeulizwa kutumia maneno 50-60 lenga maneno 60 ila yasipite 69.