Lugha, Fasihi na Elimu

Mwanafunzi wa sanduku tupu aliyezoa B+ apata mfadhili

January 18th, 2024 Kusoma ni dakika: 3

NA GEORGE ODIWUOR

LEVIS Otieno aligonga vichwa vya habari mwaka 2020 aliporipoti katika Shule ya Upili ya Kanga, kaunti ya Migori kujiunga na Kidato cha Kwanza akiwa na vipande viwili vya sabuni na sanduku tupu.

Picha zake, akisimama kando ya sanduku hilo la mabati, likiwa wazi, zilisambaa zaidi mitandaoni.

Kando yake alikuwa ni mamake, Bi Monica Atieno Odongo, ambaye alikuwa amembeba mwanawe mdogo aliyekuwa na umri wa miezi mitano.

Nyuso za wawili hao zilionyesha kwamba kulikuwa na dosari fulani; labda walihofia kukataliwa na wasimamizi wa shule kwa kukosa kununua mahitaji ya wanafunzi kujiunga na Kidato cha Kwanza.

Levis alikuwa amevalia sweta kubwa kulizidi mwili wake, ambayo alikuwa ameazima kutoka kwa kaka zake wakubwa.

Walikuwa wamesafiri kutoka nyumbani kwao katika kijiji cha Kanjira, Karachuonyo Kaskazini hadi Kanga katika eneobunge la Rongo, Kaunti ya Migori kwa lengo moja–kumwezesha Levis asajiliwe kwa Kidato cha Kwanza pasina kujali hali yake ya umaskini.

Kwa umbali mtu angetambua kuwa mwanafunzi huyo alikuwa tofauti na wenzake.

Vipande viwili vya sabuni na sanduku la mabati ndivyo vitu pekee ambavyo wazazi wake wangemudu kununua kumwezesha kujiunga na Kidato cha Kwanza.

Hii ilikuwa ni kinyume na wanafunzi wengine ambao masanduku yao yalijaa kwani walikuja na mablanketi na mahitaji mengine huku wakiwa na magodoro ya bei ghali, ishara kwamba Levis hakuwa amejiandaa kuendelea na masomo ya shule ya upili.

Bi Atieno alisema alikumbwa na changamoto za kifedha baada ya nyavu zake kuibiwa katika ufuo fulani eneo la Karachuonyo.

“Nilikuwa nimeomba mkopo niweze kuwalipia karo mabinti zangu wawili walioko katika vyuo vikuu. Lakini baada ya kuchelewa kulipa, kampuni hiyo ilituma madalali nyumbani kwangu na kuchukua mali yangu yenye thamani,” akasema.

Ingawa alifahamu kuwa hangemudu kumnunulia Levis mahitaji ya shule, Bi Atieno alikuwa mwingi wa matumaini kwamba siku moja mwanafunzi huyo angefanikiwa na kuwa mtu mwenye manufaa katika jamii.

Levis aliweza kuvuka viunzi hivyo na kuwapa moyo wanafunzi wengine ambao wamekuwa wakiripoti shuleni kutaka kujiunga na Kidato cha Kwanza.

Miaka minne baadaye, Levis aliibuka kuwa mmoja wa wanafunzi waliopata gredi nzuri zaidi katika Shule ya Upili ya Kanga, ambayo ni shule ya hadhi ya kitaifa.

Mvulana huyo alipata gredi ya B+ ya pointi 70 katika matokeo ya Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE 2023).

Matokeo hayo yamemfunguliwa milango zaidi anapojiandaa kukwea mlima wa masomo hadi chuo kikuu.

Ndoto yake ya kuwa mhandisi wa masuala ya kompyuta itatimia hivi karibuni baada ya Chuo cha Moringa kuhiari kumpa ufadhili kamili asomee kozi ya Uhandisi wa Kompyuta.

Maafisa kutoka chuo hicho wakiongozwa na mkuu wa kitengo cha ushirikiano Steve Biko Ochieng walizuru nyumba kwa Levis kumwandaa kwa awamu nyingine ya safari yake ya masomo.

“Tuliona ni bora tumpe Levis udhamini. Udhamini huu utawezeshwa kupitia ushirikiano wetu na Wakfu wa MasterCard,” Bw Ochieng’ akasema.

Chuo cha Moringa School hutoa usaidizi sawa na huo kwa wanafunzi kutoka familia maskini.

Bw Ochieng’ alisema wanasaka usaidizi kutoka mashirika mengine ili kumsaidia Levis atimize ndoto yake ya kuwa mhandisi wa kompyuta.

Aidha, Moringa School itamnunulia kipatakilishi, simu ya mkononi aina ya smartphone na kumuunganisha na intaneti.

“Anaweza kuchagua kusoma kupitia mtandaoni au anaweza kuhudhuria darasa jijini Nairobi. Hata hivyo, tunaomba usaidizi kutoka kwa mashirika mengine ili aweze kuafikia ndoto yake,” Bw Ochieng akasema.

Ikiwa atakubali kusoma kupitia mtandao, Levis atalazimika kutambua shule moja ya karibu kijijini mwake ambako atapata nafasi ya kusomea.

Mvulana huyo anatarajiwa kuhudhuria masomo kwa miezi sita mfululizo ili kupata ujuzi katika nyanja ya kompyuta.

Kimsingi, kozi hiyo husomeshwa kwa muda wa miaka minne lakini Moringa School imeifupisha hadi miezi sita.

Masomo yataanza Februari 26, 2024.

Hii itamsaidia Levis ambaye atakuwa akisoma akisubiri kujiunga na chuo kikuu Septemba 2024.

Mkuu wa Mikataba ya Ushirikiano katika shule ya elimu ya teknolojia ya programu ya Moringa, Steve Biko Ochieng (kushoto), azungumza na mwanafunzi Levis Otieno katika kijiji cha Kanjira kilichoko Rachuonyo Kaskazini mnamo Januari 18, 2024. PICHA | GEORGE ODIWUOR

Bw Ochieng alisema mwanafunzi huyo atasajiliwa katika mpango ambapo atakuwa akipokea malipo baada ya mafunzo.

Mapato hayo yatamwezesha kulipa karo yake katika chuo kikuu.

“Tuko na washirika wengine ambao tutaongea nao wamchukue kama mwanafunzi mfanyakazi (internship),” Bw Ochieng akasema.

Katika matokeo ya KCSE, Levis alipata alama ya A katika somo la Kompyuta.

Matokeo haya yalimpa moyo na mshawasha kusomea kozi ya uhandisi wa kompyuta.

TAFSIRI: CHARLES WASONGA