Namna ya kujibu maswali elekezi katika Riwaya ya ‘Nguu za Jadi’
JUMA hili naomba tuangazie namna ya kujibu baadhi ya maswali katika riwaya ya Nguu za Jadi.
1. Chambua mbinu za kimtindo zilizotumika katika kifungu kifuatacho.
“ Baadhi yao hata wakasema kuna waliouza wake zao kwa wakuu ili wapate ajira. Mangwasha aliposikia haya, alihisi mkuki wa moto umemchoma kifuani. Moyo ulimwenda mbio.
Alitamani atoke nje ili kukabiliana na lawama hizo zisizokuwa na msingi. Aliwaona watu wale kama jeshi la majeruhi lililokuwa likiramba na kuroromoa majeraha tu bila kutafuta tiba. Watanyanyaswa hadi lini?
Watabaguliwa na kutengwa mpaka lini?
Aliwafananisha Waketwa wenzake na kundi la kondoo lisilokuwa na mchungaji. Kondoo hao wamechapwa viboko. Wametawanyika na kukimbilia wasikokujua.” uk 10.
Sitiari – … alihisi mkuki wa moto umemchoma kifuani…
Jazanda – … kundi la kondoo, mchungaji na … kondoo kuchapwa viboko
Balagha – … hadi lini?… mpaka lini?
Tashbihi – … kama jeshi…
Tashihisi – kukabiliana na lawama…
2. Jadili aina za taswira zilizotumiwa katika kifungu
Taswira sikivu – Mangwasha aliposikia…
Taswira hisi – … alihisi mkuki wa moto…
Taswira mwendo – Moyo ulimwenda mbio …
Taswira oni – … Aliwaona watu…
Taswira mguso – … wamechapwa viboko…
3. Fafanua toni inayojitokeza katika muktadha huu
Toni ya kutamauka/kusikitisha –… aliwafananisha na kundi lisilo na mchungaji…
4. Thibitisha kuwa jamii ya Matuo ni kundi la kondoo lisilokuwa na mchungaji.
Mangwasha alishuhudia vijana wengi wakiwa kwenye viambaza vya maduka bila shughuli maalum kwa sababu ya kutamauka.
Sihaba aliwatumia wasichana wadogo katika ukahaba kwenye majumba yake bila kujali mustakabali wao.
Mangwasha alitambua kuwa vijana wengi wa kiume hufa katika kujaribu kuwa wanaume kwa kukosa dira mahususi ya kuwaelekeza.
Mzazi wa kiume ambaye ndiye dira ya kumwelekeza mtoto wa kiume hayupo au hajulikani; hivyo wavulana hukosa mafunzo muhimu ya maisha.
Mangwasha anatambua kuwa wazazi wachache wa kiume waliopo wametingwa na shughuli nyingi mjini na hawana muda wa kuwafunza wavulana, kinyume na ilivyokuwa kijijini.
Mangwasha anagundua kuwa kuna maandishi machache yanayomfunza mtoto wa kiume ilhali mengi yanamhusu mtoto wa kike.
Mangwasha anatambua kuwa kutelekezwa kwa mtoto wa kiume kumesababisha wanaume wengi mjini kuchakura vyakula mapipani na kuvaa nguo kuukuu.
Mangwasha anashuhudia wasichana wengi mitaani wenye vitoto visivyokuwa na baba.
Mrima anaitelekeza jamii yake kwa kuzamia ulevini na kuisababishia madhila mengi.
Ngoswe na wenzake wanajihusisha na ulanguzi magerezani, shuleni na vyuoni; vijana wanakuwa mazube, wazururaji na wengine kuacha masomo.