Lugha, Fasihi na Elimu

Ndani ya shule ya msingi ya umma ya kwanza Ngando aliyofungua Rais

May 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA FRIDAH OKACHI

WADI ya Ngando, eneobunge la Dagoretti Kusini imepata shule ya msingi ya umma ya kwanza iliyofunguliwa na Rais William Ruto mnamo Jumatatu.

Shule ya Msingi ya Lenana itawafaa wanafunzi wengi.

Rais Ruto, alisema serikali ya Kenya Kwanza itaongeza madawati ili usimamizi wa shule hiyo kuongeza idadi ya wanafunzi.

“Nilikuja hapa wakati kulikuwa na janga la shule kubomoka na kuua wanafunzi kadhaa. Niliongea na usimamizi wa Shule ya Kitaifa ya Lenana na wakapeana idhini ya kujenga madarasa 23. Kwa sasa shule hii ina wanafunzi 1,300. Nimeongea na wanafunzi kadhaa ambao wametoka katika shule 10 tofauti,” akasema Dkt Ruto.

Kiongozi wa nchi alikuwa akirejelea tukio ambapo wanafunzi wanane waliaga dunia huku 64 wakijeruhiwa madarasa mawili yaliporomoka shuleni Precious Talent Top School mnamo Septemba 23, 2019.

Mkasa huo ulitokea wakati wa masomo ya asubuhi.

“Kwa kila mtoto atakayejiunga na shule hii kwa mara ya kwanza, nitanunua sare na viatu. Hawa watoto huja hapa na sare kutoka shule tofauti na wengine wanavalia mavazi ya nyumbani ili kupata elimu. Lakini, kabla sare zifike, hawa watoto ni lazima waendelee kusoma,” aliahidi Rais.

Rais alisema kuwa madarasa yaliyojengwa ni machache ikilinganishwa na wakazi wa eneo hilo walio na watoto. Wizara ya Elimu ikilazimika kutoa Sh10 milioni ili kukamilisha sehemu iliyosalia.

“Nafasi iliyopo ni ya wanafuzi wa Gredi ya Kwanza, Gredi ya Pili na Gredi ya Tatu. Bado tuna Gredi ya Nne, Gredi ya Tano na Gredi ya Sita. Tumekubaliana na Wizara ya Elimu, watatupea pesa ili kujenga sehemu zilizosalia,” aliongeza kiongozi wa nchi.

Wakazi wa eneo hilo wamekuwa wakilalamikia kuachwa nyuma kimaendeleo, wengi wakilazimika kuwapeleka watoto katika shule ghali za kibinafsi au kusafiri mwendo mrefu kuwapeleka kujiunga na shule za umma.

Rais William Ruto akiwasili katika Shule ya Msingi ya Lenana. PICHA | FRIDAH OKACHI

Wakati wa sherehe hiyo ya kufungua shule hiyo mpya ya msingi, Dkt Ruto aliahidi kujenga madarasa mengine, mradi ambao unatarajiwa kukamilika kwa muda wa miezi miwili ijayo.

“Nimejitolea kujenga madarasa mengine mapya, na pesa hazitatoka kwa wizara. Nitajenga madarasa 24. Mhadisi ataanza kufanya kazi hiyo leo ili nikirejea miezi miwili ujenzi uwe umekamilika,” alieleza.

Bi Nyairo alisema wana upungufu wa madawati wakisubiri kufadhiliwa na wasamaria wema.

“Hatuwezi kusajili wanafunzi wa Gredi ya Nne kwa kuwa hatuna madawati. Tunasubiri kuona ahadi aliyotoa Rais ikitekelezwa juma lijalo. Viti vikija ndio tutaanza kuchukua wanafunzi wa Gredi ya Nne na Gredi ya Tano,” alisema Bi Nyairo.