Lugha, Fasihi na Elimu

NDIVYO SIVYO: Uhuru alitumia neno ‘utengemano’ kwenye hotuba yake, ila si Kiswahili sanifu

Na ENOCK NYARIKI November 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

KATIKA hafla ya kutawazwa kwa kasisi wa Embu, Mheshimiwa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta alieleza mahudhura kuhusu umuhimu wa kuishi kwa upendo na umoja.

Aliitaja dhana ambayo ijapokuwa ilikinzana na kile alichokusudia kusema, ikipigwa msasa, itazua maana ambayo ni kinyume na aliyokusudia. Hivi ndivyo alivyosema: “Hakuna haja ya kuishi kwa utengemano…”

Neno alilolenga ni ‘utengano’. Nomino hii inatokana na kitenzi ‘tengana’ chenye maana ya kukaa mbalimbali kwa kutoelewana. Profesa Said A. Mohamed anapolitumia katika riwaya ya ‘Utengano’ neno lenyewe linaibua dhana ya kuvunjika kwa ndoa au kufarakana.

Hata hivyo, kwa kulirekebisha neno la mwisho katika usemi wa Mheshimiwa Uhuru Kenyatta, tutaibuka na kitenzi ‘tangamana’ ambacho fasili yake ni ishi kwa umoja bila kubaguana.

Kutokana na kitenzi hicho, inaundwa nomino ‘tangamano’. Tangamano ni hali ya watu kuishi pamoja kwa kuelewana na kushirikiana.

Neno jingine ambalo ni kitate cha ‘tengana’ na ‘tangamana’ ni ‘tengemaa’. Kitenzi hiki nacho kina maana mbili. Kwanza, kaa sawasawa kama ilivyokuwa awali na, pili, tuama kwa vumbi kwenye vitu viowevu kama vile maji.

Kipo kitenzi ‘tengenea’ ambacho ingawa hakijitokezi bayana kwenye kamusi nyingi za Kiswahili, kina maana ya kuwa katika mwelekeo wa kukamilika vizuri.

Kisawe cha kitenzi hiki ni ‘tasawari’. Mtu anaposema kuwa mambo yatatasawari, kauli hii ina maana kuwa mambo yako katika mwelekeo wa kukamilika vizuri au kwenda jinsi ilivyokusudiwa.

Alhasili, maneno ‘tengana’, ‘tangamana’, ‘tengemaa’ na ‘tengenea’ yanatofautiana kimaana. Umakinifu mkubwa unahitajiwa wakati wa kuyatumia katika mawasiliano ili kuwasilisha ujumbe moja kwa moja.