• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
NGUVU ZA HOJA: Tafsiri na ukalimani zijumuishwe katika mtaala wa shule za upili

NGUVU ZA HOJA: Tafsiri na ukalimani zijumuishwe katika mtaala wa shule za upili

NA PROFESA JOHN KOBIA

UTEKELEZAJI wa mtaala wa Umilisi katika mfumo wa elimu unaendelea ingawa kuna changamoto nyingi.

Wanafunzi wa kikundi cha kwanza katika mfumo huu wameingia gredi ya nane mwaka huu. Wachapishaji vitabu wako mbioni kuandaa vitabu vya gredi ya 9 vilivyoidhinishwa na Taasisi ya Ukuzaji Mitaala ya Kenya (KICD) vitavyotumiwa mwaka ujao.

Macho yote sasa yataelekezwa kwenye maandalizi ya mitaala ya Daraja la juu kwa shule za upili kuanzia Gredi ya Kumi hadi Kumi na Mbili. Huku maandalizi ya mitaala hiyo yakiendelea, ni muhimu wanaohusika kupitia KICD wajumuishe mada za tafsiri na ukalimani katika somo la Lugha ya Kiswahili.

Tafsiri na ukalimani ni taaluma muhimu sana katika ulimwengu wa kiutandawazi ambapo dunia imekuwa sawa na kijiji. Tafsiri ni shughuli ya uhamishaji wa ujumbe ulioandikwa kwa lugha moja na kuuwasilisha kwa lugha nyingine.

Kwa upande mwingine, ukalimani ni uhamishaji) wa ujumbe kutoka lugha moja hadi nyingine (ambayo ni lugha pokezi) papo kwa papo kwa mazungumzo.

Mada za tafsiri na ukalimani zinapaswa kujumuishwa kwenye mtaala wa Lugha ya Kiswahili kwa sababu ni mada zitakazobainisha umilisi wa mwanafunzi katika mawasiliano na uwazaji kwa kina mambo ambayo yanasisitizwa katika mfumo wa Umilisi.

Tafsiri ni wenzo wa kuwasiliana, kwa hivyo hukuza na kueneza tamaduni mbalimbali. Lugha ni wenzo mkuu wa kuhifadhi na kueneza tamaduni za watu ulimwenguni.

Kupitia ujuzi wa tafsiri, wanaohitimu wataweza kupata ajira. Maarifa ya tafsiri huhitajika katika nyanja kama vile uanahabari mathalan magazeti, redio, televisheni na habari za kidijitali.

MAKALA HAYA YATAENDELEA

  • Tags

You can share this post!

Wanafunzi 25 waliokosa KCPE kujiunga na shule za upili

Zakat Kenya, Premier kuchangisha Sh30m kununulia familia...

T L