Lugha, Fasihi na Elimu

JIFUNZE LUGHA: Ni katika mazingira gani ambapo kiambishi ‘ni’ hutumiwa kutoa amri?

Na ENOCK NYARIKI February 19th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MWALIMU Moses Kanyai, mmoja wa maashiki wa safu ya ‘Ndivyo Sivyo’, aliposoma makala yangu yaliyokosoa matumizi ya kiambishi {ni} katika anwani ‘Twendeni Sote….’ alitoa maoni yafuatayo:

‘‘Wakati tunafunza viambishi maalumu, huwa tunasema kuwa {ni} inaweza kutumiwa kuonyesha amri k.m. ‘tokeni!’. Maoni hayo yana ukweli gani?’’

Ingawa nililijibu swali la Bwana Kanyai kwa njia ya arafa, nimeona ni vyema niandike ili kushughulikia utata uliopo katika kutumiwa kwa kiambishi tulichokitaja kutoa amri, rai au himizo.

Nitaanza kwa kunukuu mojawapo ya majibu niliyompa Ndugu Kanyai tulipokuwa tukijadiliana.

“Ingalikuwa kiambishi {ni} katika neno ‘tokeni’ ni cha kutoa rai au amri inavyodaiwa, basi ingalichukuliwa kuwa hata katika hali ya umoja – pale ambapo nafsi ya pili inahusika – kiambishi hicho kingetekeleza dhima hiyo hiyo maadamu kanuni hiyo sharti iwe mtambuko. Hata hivyo, sivyo ilivyo. Haiyumkiniki kusema *‘tokani’ kwa kuwa kiambishi hicho ni cha kutoa amri hata katika mazingira hayo ya hali ya umoja!”

Jambo jingine linaloonesha kuwa kiambishi {ni} katika neno ‘tokeni!’ hakikusudiwi kutoa rai au amri ni uhalisia kwamba hakitokei wakati kiambishi cha nafsi katika hali ya wingi kimeambikwa katika neno hilo. Kwa njia nyingine, haiyumkiniki kusema ‘mtokeni!’

Kwa hivyo, {ni} katika neno ‘tokeni’ hutekeleza dhima ya wingi ilivyo katika vitenzi vyote vilivyo katika nafsi ya pili wingi hasa wakati msemaji hashurutiki kuhusisha viambishi vya nafsi viambata katika vitenzi hivyo.

Nitaifafanua kauli hii zaidi katika sehemu ya pili ya makala haya.

[email protected]

MAKALA YATAENDELEA