• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Njeru Githae achapisha vitabu 15, vyote vikiongea kuhusu masaibu

Njeru Githae achapisha vitabu 15, vyote vikiongea kuhusu masaibu

NA MWANGI MUIRURI

MWANASIASA, balozi Robinson Njeru Githae amechapisha vitabu 15 kwa mpigo na kuvizindua katika hafla iliyopambwa na Dkt Karanja Kibicho ambaye alikuwa Katibu wa Usalama wa Ndani katika utawala wa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta.

Vitabu hivyo vyote 15 viko na vichwa vinavyohusu masaibu.

Si masaibu ya Dedan Kimathi, si ya Wakazi wa Jiji la Nairobi, si ya Mugo wa Kibiru, si yale ya Tom Mboya, si ya Elija Masinde, si yaliyomkaba mke wa Caesar, si masaibu ya Masinde Muliro. Yaani ni masaibu tu!

Dkt Kibicho ambaye alikuwa na ushawishi mkuu na pia aliyedaiwa kuwa ndani ya njama kali ya kumfungia Dkt William Ruto asirithi mikoba ya Ikulu, akisemwa kumpendelea Raila Odinga, kwa sasa huwindwa kiuchumi na kisiasa kama swara na utawala uliopo.

Amekuwa akirejelewa katika mikutano ya kisiasa eneo la Mlima Kenya na wandani wa utawala wa Rais Ruto akihusishwa na mengi yasiyo ya kumjenga huku kwa upande wake akikaa ngumu ndani ya kimya bila ya kuwajibu.

Ni katika hali hiyo ambapo macho na masikio yalikuwa kwake alipojitokeza mnamo Mei 3, 2024, jijini Nairobi kupamba hafla ya Bw Githae lakini kinyume na matarajio ya wengi, akakwepa kuongea ya kusisimua hisia za kisiasa na akaishia tu kuwashawishi Wakenya wapende masomo na wawe wa kusaka busara ya kimaisha ndani ya vitabu.

“Mimi nikiwa mdogo nilikuwa na bidii sana ya kusoma riwaya. Katika ujana wangu, nashuku nilisoma zaidi ya riwaya 1,000,” akasema Dkt Kibicho.

Bw Githae ambaye ni wakili kitaaluma, alizaliwa mwaka wa 1957 katika Kaunti ya Kirinyaga na ambapo alihudumu kama mbunge wa Ndia kati ya 2003 na 2013.

Akiwa mbunge, aliteuliwa kuwa Naibu Waziri katika wizara kadha kabla ya kupandishwa cheo hadi kuwa Waziri wa Fedha kati ya 2011 na 2013.

Mwaka wa 2014 aliteuliwa kuwa balozi nchini Amerika kabla pia ya kuteuliwa kama balozi nchini Austria na hatimaye akahudumu kama katibu maalum katika baraza la Umoja wa Mataifa.

Bw Githae ni nduguye mdogo marehemu Prof Micere Mugo na pia Bi Muthoni Macharia ambaye ni mke wa mmiliki wa kampuni ya Royal Media Services, Samuel Kamau (SK) Macharia.

Katika uzinduzi huo wa vitabu, Jaji wa Mahakama ya Rufaa Mwaniki Gachoka alisema “Wakenya huwa na shida ya kusoma vitabu na ni vyema wengi wakumbatie uraibu wa kusaka mengi ya kunoa bongo ndani ya maandishi ya wengine”.

Alisema bongo zilizokumbatia utamaduni wa kusoma huwa na makali aina yake hasa katika safu ya kijamii ambapo kuishi na watu kunahitaji umakinifu mwingi sana.

Hata aliyekuwa Naibu wa Mkurugenzi wa shirika la ujasusi nchini (NIS) Bw Frank Kiriinya alifika katika hafla hiyo, ikiishia kuwa kama mkutano wa vifaranga vya utawala wa Rais Kenyatta.

Hafla hiyo iliyoandaliwa katika ukumbi wa kanisa la All Saints Cathedral ilifanya Bw Githae kufichua kwamba tangu utotoni alikuwa anapenda kuandika.

“Ni vile tu siasa zilikwamisha taaluma yangu ya uwakili na hata ubalozi kufanya mambo kuwa magumu. Huduma kwa taaluma na siasa iliweka nyota yangu ya uandishi pembeni lakini baada ya kutamatisha huduma hizo mwaka 2023 na nikarejea hapa nchini, nimekimbizana nayo hadi nikainasa na matokeo ni vitabu hivi ninavyozindua kwa sasa,” akasema.

Alisema kwamba ikiwa ubunifu wa uandishi unaweza ukakumbatiwa nchini, unaweza ukawa kitega uchumi kikuu cha kuunda ajira.

“Dadangu Miceere Mugo alinipa motisha ya uandishi lakini kwa kuwa niliingia kwa siasa, sikuweza kujipa uwezo kamili. Lakini sasa nikiwa na miaka ya kustaafu, nimepata muda wa kutosha na matokeo ni haya sasa ambapo ninawaalika mujipe nakala hizi msome kuhusu nyota yangu ya uandishi,” akasema.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mfalme Charles, Malkia watuma rambirambi kufuatia mafuriko...

Mkewe Mwangi Wa Iria ajipata pabaya kwa ufisadi wa Sh351m

T L