NYARIKI: ‘Lini’, ‘nani’ na ‘nini’ si vivumishi vya kuuliza
KATIKA kutoa ufafanuzi kuhusu matumizi bora ya baadhi ya vivumishi vya kuuliza, mwandishi fulani wa makala ya lugha alirejelea maneno ‘nani’, ‘nini’ na ‘lini’ kama vivumishi vya kuuliza.
Nilipomaliza kusoma makala hayo, nilimwandikia ujumbe ufuatao (nimenukuu sehemu):
“…. Kuhusu makala yako ya wiki hii, ningependa kuchangia kuwa maneno ‘nani’, ‘nini’ na ‘lini’ si vivumishi kwa kuwa hayatoi maelezo kuhusu nomino bali yanaziwakilisha nomino zenyewe katika tungo. Kwa hivyo, tunapaswa kuyarejelea kama viwakilishi viulizi.”
Niliendelea kufafanua kuwa haiyumkiniki kumwuliza mwenzako: *‘Unasema kitu nini?’ Vivyo hivyo, unapotaka kufahamu jina la mtu humwulizi: *‘Unaitwa mtu nani?’
Ili msomaji wa makala haya aelewe wazi ujumbe niliomwandikia mtaalamu huyo kwa kutumia iktisadi ya maneno, nitabainisha tofauti iliyopo baina ya vivumishi na viwakilishi – maneno ambayo yanakurubiana mno kidhima.
Yamkini baadhi ya walimu huwapotosha wanafunzi kwa kuwaeleza kuwa ‘nani’, ‘nini’ na ‘lini’ ni vivumishi kwa kutoelewa vyema maana na kazi ya vivumishi.
‘Kamusi Elezi ya Kiswahili’ inafasili kivumishi kama kipashio kinachoelezea sifa za kitu au mtu kama vile refu, dogo, baya na zuri.
Ingawa maana hii ni sahihi, imetumia iktisadi – jambo ambalo huenda likatatiza uelewa wa anayekumbana na dhana yenyewe kwa mara ya kwanza.
Kwa hivyo, ninaeleza kuwa kivumishi ni neno linalotoa maelezo zaidi kuhusu nomino au kiwakilishi.
Katika fasili hii, nimetaja dhana ‘nomino’ au ‘kiwakilishi’ – dhana ambazo ni muhimu kuzingatiwa katika kuelewa maana na dhima ya kivumishi.
…YATAENDELEA