PROF IRIBE: Haya maneno ‘skiza’, ‘akuna’, ‘waeza’, ‘iyo’, ‘baadae’ si sanifu, tafadhali!
MNAMO tarehe 15 juma lililopita, aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua (almaarufu Riggy G) alizindua chama chake, Democracy for the Citizens Party (DCP).
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa chama, falsafa ya chama hicho inadhihirika katika kauli mbiu yake ambayo ni “Skiza Wakenya”.
Si mara ya kwanza ambapo neno “skiza” linatumika katika mawasiliano nchini. Hutumika sana! Jambo hili limefanya neno lenyewe kuonekana sanifu na wengi.
Lakini si neno hili pekee, kuna mtindo wa kuandika ambao umeibuka ambapo herufi fulani zinadondoshwa. Nimeona maneno kama vile “akuna”, “aezi”, “adi”, “saaii”, “iyo”, “baadae”, “waeza” na mengine.
Sitaki kusema kuwa maneno hayo si sahihi, lakini nitasema kuwa si sanifu. Nasema hivi nikielewa kwamba matumizi haya ya lugha yanaweza kuwa yanatokana na Sheng ama vimelea vyake.
Jukumu muhimu la lugha huwa kuwasiliana na ni maoni yangu kuwa wafanyabiashara na wanasiasa wanapofanya uteuzi fulani, hufanya hivyo kutokana na uelewa kwamba walengwa watawaelewa vizuri na kwa haraka zaidi maneno fulani yakitumiwa.
Kwa kawaida, uteuzi huu huwa si wa kiholela. Bila shaka nachukulia kwamba waasisi wa kauli mbiu kama hii wanaelewa kwamba neno sanifu ni “sikiza” lakini wamehiari kudondoa irabu “i”.
Ukawaida ambao aghalabu tumeuona ni udondoshaji wa konsonanti lakini katika hali chache kama hii tunaona irabu ikidondolewa. Haya ni masuala ya watafiti wa lugha.
Turejee tena kwenye kauli mbiu “Skiza Wakenya.” Neno “skiza” au “sikiza” hapa linatumika kama nafsi ya pili umoja.
Ni kama anaelekezwa mtu. Je, matumizi hayo ya nafsi yalitokana na uteuzi wa hiari? Ni matumizi yanayofaa kwa kauli mbiu?