PROF IRIBE: Tanzania wamechapukia makuzi ya Kiswahili kwa juhudi, ila mkabala wa Kenya ni upi?
NA PROF IRIBE MWANGI
Mwezi uliopita niliandika kuwa, “kongamano (la Chama cha Ukuzaji wa Kiswahli Duniani) la 2024 litafanyika nchini Kyuba katika jiji la Havana, kutokana na mwaliko wa Balozi Humphrey Polepole.”
Hili linaonoeka jambo zuri kwa kuwa linaashiria ukuaji wa Kiswahili katika maeneo ya yanayotumia lugha tofauti na Kiingereza.
Kwa hakika, Kihispanyola ndiyo lugha ya pili kwa matumizi duniani. Kuwa na kongamano la Kiswahili Marekani Kusini basi ni jambo la kushabikiwa. Kwamba Balozi Humphrey Polepole wa Tanzania aliahidi kushughulikia baadhi ya gharama vilevile ni jambo la kushangiliwa.
Kenya imo wapi kwa haya yote? Nchi jirani ina vyombo kadhaa mahsusi kwa makuzi, maenezi na ubidhaaishaji wa Kiswahili.
Mbali na mabaraza mawili, (BAKITA na BAKIZA) kuna taasisi (TATAKI) na vyombo vyote vya serikali, yakiwemo mabalozi, viko mbioni kueneza Kiswahili.
Serikali ya Tanzania imejitolea kwa hali, mali, matamshi na vitendo kutumia na kukuza Kiswahili. Kenya tu wapi?
Je, tukiulizwa kiungo kimoja kinachosimamia maswala ya Kiswahili (sio tu kisheria mbali kwa vitendo) tutataja kipi au nani?
Tanzania kuna Katibu wa BAKITA, kuna Katibu wa BAKIZA, kuna Mgonda wa Kigonda cha Kiswahili cha Mwalimu Nyerere (TATAKI) wanaosimamia vyombo vya serikali vinavyojukumikia Kiswahili pekee.
Japo kuna fununu kwamba mchakato wa kuunda Baraza nchini unaendelea, lakini tunajikokota mno ilhali wenzetu wamechangamkia fursa.
Wakinufaika zaidi kutokana na Kiswahili tusije tukajuta, kama wasemavyo wahenga, chelewachelewa utapata mwana si wako!
Naiomba Serikali, na hasa Idara za Turathi, Utalii, Dayaspora, Elimu, Afrika Mashariki na Michezo kuonyesha ari na utashi wa kukuza Kiswahili.