Lugha, Fasihi na Elimu

Raila akemea siasa za lugha kinyang’anyiro cha kuwania Uenyekiti wa AUC kikichacha

Na ENOCK MATUNDURA November 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

SUALA nyeti kuhusu nafasi ya lugha katika mustakabali wa bara la Afrika limechipuza, huku kinyang’anyiro cha Uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AU) kikishika kasi.

Akizungumza jijini Addis Ababa nchini Ethiopia mnamo Novemba 10, 2024, aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga, alitoa wito kwa mataifa ya Afrika ‘kuvua majoho’ ya kimaeneo kwa misingi kwamba hali hiyo ni masalia ya taathira za ukoloni.

Uchaguzi wa kumtafuta mrithi wa mwenyekiti wa sasa, Moussa Faki Mahat, ambaye amehudumu tangu Januari 30, 2017, utafanyika Februari 2025. Bw Odinga anamenyana na Mabw Mahamoud Yuossouf (Djibouti), Anil Gayan (Mauritius) na Richard Randriamandrato (Madagascar).

Bw Odinga, ambaye alikuwa akizungumza katika muktadha wa historia ya Muungano wa Afrika alisema, mataifa ya bara hili yamegawanyika kwa misingi ya lugha za waliokuwa watawala wao wa kikoloni – mathalani Anglofoni (Kiingereza), Frankofoni (Kifaransa) na Lusofoni (Kireno).

Kauli ya Bw Odinga ilisadifu mdahalo uliozuka Addis Ababa mnamo Oktoba 2005, kwenye Kongamano la Saba la Kimataifa kuhusu Lugha na Maendeleo. Kongamano hilo la kihistoria lilikuwa la kwanza kuwahi kuandaliwa Afrika, tangu msururu wa makongamano kuhusu lugha yaanzishwe jijini Bangok, Thailand mnamo 1997.

Kongamano hilo lilitalii suala la lugha na jinsi mataifa barani Afrika yametumia lugha zinazozungumzwa ndani ya mipaka yao. Washiriki kwenye mkutano huo waliitathmini hali ya wingi lugha barani Afrika huku wakijiuliza: Wingilugha barani Afrika – ni balaa au neema?