Lugha, Fasihi na Elimu

Sababu za ‘E’ kujaa Pwani

January 14th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA WINNIE ATIENO

WALIMU wakuu kutoka ukanda wa Pwani wamehusisha matokeo duni kwenye Mtihani wa Kitaifa wa Kidato cha Nne (KCSE) na hatua ya watahiniwa kutoweka kisha kuja tu kufanya mtihani.

Imebainika kuwa baada ya kujisajili kwa KCSE, baadhi ya wanafunzi hutoroka shule na kukosa vipindi vya masomo kisha kurudi tu na kufanya mtihani. Mkondo huu wa mambo umeshamiri sana katika kaunti zote za ukanda wa Pwani.

Alipojiunga na Shule ya Serani muhula wa pili mwaka 2023, Mwalimu Mkuu Ali Mohamed, alisema kuwa idadi ya watahiniwa ambao walikuwa wamesajiliwa walikuwa 71 lakini waliokuwa wakifika shuleni na kusoma walikuwa wachache.

Bw Mohamed ambaye pia alisomea shule hiyo, alihamishwa huko kutoka shule ya Kwa Bulo inayopatikana eneobunge la Nyali.

Kwa Bulo ilikuwa na wanafunzi 650 lakini akasikitika kuwa Serani ilikuwa na wanafunzi 236 pekee.

“Nilishangaa sana kuwa watahiniwa 30 hawakuwa shuleni na sikuwajua. Nilikuja kuwaona tu wakati wa mtihani. Pia nilifahamishwa kuwa mtahiniwa mmoja alikuwa akizuiliwa kwenye rumande na alikuja tu kufanya mtihani,” akasema Bw Mohamed.

Katika matokeo yaliyotolewa ya KCSE 2023, watahiniwa 32 ambao hawakuwa wakihudhuria masomo walipata E.

Isitoshe wanaomaliza shule Serani na kupata E hawajakuwa wakienda kuchukua vyeti vyao kwa muda wa miaka 10 iliyopita.

“Hawana haja na elimu. Hili jambo linasikitisha sana kama mwalimu mkuu kwa sababu enzi zetu angalau matokeo yalikuwa afadhali,” akaongeza Bw Mohamed.

Aliyekuwa Gavana wa Mombasa Hassan Joho alisomea Serani na kupata D- mnamo 1993.

Serani imekuwa ikishikilia rekodi ya kihistoria ya kutoa watahiniwa wengi wanaopata E na D eneo la Pwani. Ikifahamika sana kwa kung’aa kwenye soka, idadi ya wanafunzi ambao ni wanasoka hodari wamekuwa wakipata D na E na hujitokeza tu shule wakati wa michezo ya soka ya shule za upili.

Katika Shule ya Sekondari ya Bomu, Kaunti ndogo ya Changamwe hali si tofauti kwa sababu wanafunzi 31 walitoweka baada ya kujisajili mwaka 2023. Hawa nao pia walipata D na E.

“Watahiniwa wana marafiki ambao hawakumaliza shule. Wanaambiwa hakuna haja ya kusoma na hakuna kazi. Watahiniwa wangu watano wavulana hata walioa na kupata watoto na waliniambia hawawezi kuwaacha watoto nyumbani na kuja kusoma shuleni,” akasema Mwalimu Mkuu wa Bomu Wilfred Otondi.

Kwenye kaunti za Kwale, Kilifi, Lamu na Tana River, walimu wakuu wengi kwenye mahojiano na Taifa Jumapili walilalamika kuwa watahiniwa baada ya kujisajili, hawajitokezi shuleni na huja tu kufanya mtihani.

“Wengi wao kisaikolojia washaelekeza fikra za kuenda Uarabuni kufanya kazi baada ya KCSE. Hawajali kama watapita au kuanguka mtihani na kama walimu hatuwezi kuwafanyia chochote,” akasema Mwalimu Mkuu mmoja kutoka Kaunti ya Kwale.

Mkurugenzi wa Elimu Ukanda wa Pwani , Bw Lucas Kangongo, alifichua kuwa wakati wa mtihani alitembelea shule mbalimbali na kupata watahiniwa wamelala baada ya kuandika majina yao.

“Nilipowauliza tatizo lilikuwa nini, waliniambia wanataka tu vyeti,” akasema Bw Kangongo.